Tuesday, November 26

Wazazi Tuwaelekeze Watoto Wetu Katika Maadili Mema – Alhaj Othman Masoud.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj Othman Masoud Othman akisalimiana na Viongozi wa Dini na Wananchi alipowasili katika hafla ya ufunguzi wa Madrasatul Tears of Joy ya Magogoni Mikarafuuni Wilaya ya Magharibi “B” Unguja. alipowasili kwa ajili ya ufunguzi wa Madrasa hiyo ilioko mtaa wa magogoni . 

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj Othman Masoud Othman akikata utepe kulifungua jengo jipya la Madrasatul Tears of Joy ya Magogoni Mkarafuuni  Wilaya ya Magharibi “B”Unguja na (kushoto kwake) Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Mahmoud Mussa na (kulia kwake0 Sheikh Dkt. Hikmany.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj Othman Masoud Othman akizungumza na Wanafunzi wa Madrasatul Tears of Joy ya Magogoni Mikarafuuni baada ya kuifungua Madrasa hiyo.
Mwakilishi wa Tears of Joy Zanzibar Sheikh Jaffar Hussein Bapumiya akitowa maelezo ya Ujenzi wa Madrasatul Tears of Joy ya Magogoni Mikarafuuni akitowa maelezo ya kiufundi ya madrasa hiyo wakati wa hafla ya ufunguzi wake.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj Othman Masoud Othman akizungumza na Wananchi wa Wanafunzi wa Madrasatul  Tears of Joy ya Magogoni Mikarafuuni baada ya kuifungua na kutowa nasaha zake kwa Wazee na Wanafunzi wa Madrasa hiyo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Alhaj Othman Masoud Othman akiitikia dua ikisomwa na Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Mahmoud Mussa, baada ya kumalizika kwa hafla ya ufunguzi wa Madrasatul Tears of Joy ya Magogoni Mikarafuuni  Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.

 

Na.OMWR -Zanzibar. 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amewataka wazazi na walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanawasaidia watoto wao kujifunza elimu ya dini kwa lengo la kutengeneza jamii iliyo bora nchini.
Alhaj Othman ameyasema hayo leo (Juni 17),wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa Madrasatul Tears of Joy ya Magogoni Mikarafuuni, iliyojengwa kwa ufadhili wa taasisi ya Tears of Joy kwa kushirikiana na taasisi ya Annur Islamic Centre.
Alhaj Othman, alisema kuwa madrasa ndio msingi wa kuwatayarisha watoto wawe na maadili mazuri na waweze kuwa wenye manufaa kwa dini yao na jamii kwa ujumla.
“Matokeo mbali mbali yanayoshuhudiwa nchini ikiwemo ya wizi, ujambazi, rushwa, uhujumu uchumi na uharibifu wa jamii yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na kukosekana kwa maadili,” alisema Alhaj Othman. Sambamba ujumbe huo aliwasisitiza wazee kutoa ushirikiano mkubwa kwa walimu kwani hiyo ndiyo chachu ya mafanikio ya mwanafunzi.
Hata hivyo Alhaj Othman ameonesha faraja yake kuona bado waislamu wana moyo wa kufanya mambo makubwa na yenye ujira kwa Mwenyezi Mungu, pamoja na kutoa wito kwa waislamu wengine wenye uwezo iwe mtu mmoja mmoja au jumuiya wawe mbele katika kujitolea kwenye mambo ya kheri kwani bado kuna wananchi wengi wanaotafuta fursa hizo.
Pamoja na hayo amesema kuwa serikali kwa upande wake inafanya jitihada ya kuweka sheria na miongozo mizuri ili zakka na wakfu ziweze kuwanufaisha zaidi waislamu nchini.
Kwa upande wake Naibu Mufti Sheikh Mahmoud Mussa Wadi, ambaye pia amehudhuria uzinduzi huo, amewakumbusha wakaazi wa eneo hilo kuitumia ipasavyo madrasa hiyo kwa lengo la kukuza taaluma ya dini nchini.
Naye mwakilishi wa Tears of Joy Zanzibar Sheikh Jaffar Hussein Bapumiya, alisema miongoni mwa malengo makubwa ya taasisi hiyo ni kuisaidia jamii ya Zanzibar katika uchimbaji wa visima, ukusanyaji wa zakka na sadaka na kuzitoa kwa watu wasiojiweza.
Aidha amemuomba Alhaj Othman kuwafikiria kupata sehemu ya kufanya shughuli zao kwa ajili ya kulinda mali na misaada wanayoipata ili kuboresha shughuli za taasisi hiyo.
Tears of joy ni taasisi iliyoanzishwa mnamo tarehe 03/06/2019 na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kwa lengo la kuzisaidia jamii zinazopambana na hali ngumu ya kimaisha ambayo hadi sasa imeshatumia milioni mia tatu sabiini na nane na laki nane katika kusaidia maeneo mbali mbali nchini.