RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameiomba Serikali ya Qatar kuwashajiisha Wawekezaji wa nchi hiyo kuja nchini kuwekeza katika sekta za Utalii, Uvuvi pamoja na mafuta na Gesi.
Dk. Mwinyi ametoa ombi hilo Ikulu jijini Zanzibar, alipozungumza na Balozi wa Qatar nchini Tanzania Hussain Ahmad Al Humaid, aliefika kujitambulisha.
Amesema tayari Zanzibar imeanzisha Sera maalum kwa ajili ya kuendeleza Uwekezaji, ikiwa ni hatua ya kuimarisha uchumi wake.
Rais Dk. Mwinyi aliiomba nchi hiyo kuangalia uwezekano wa kuisaidia Zanzibar katika uimarishaji wa sekta za Maji, Afya pamoja na elimu.
Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi mbili hizo, na kubainisha umuhimu wa hatua hiyo kuendelezwa katika sekta binafsi.
Aidha, Dk. Mwinyi alisema kuwepo kwa safari za Ndege kati ya Zanzibar na Qatar ni fursa muhimu ya kuendeleza biashara kati ya nchi mbili hizo, na kuiomba Qatar kuweka mazingira bora ya soko la bidhaa mbali mbali.
Katika hatua nyengina, Dk. Mwinyi alimshukuru Balozi huyo kwa utayari wake wa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kuwashajihisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja nchini kuwekeza.
Aidha, aliiomba Serikali ya Qatar kutoa taarifa za ujio wa wana familia ya Kifalme katika shughuli za kitalii mapema iwezekanavyo, ili waweze kupata hadhi wanazostahili.
Vile vile aliitakia mafanikio mema nchi hiyo katika maandalizi ya Kombe la Dunia yanayoendelea, ambapo fainali zake zitafanyika mwaka 2022.
Nae, Balozi Humaid aliahidi Serikali ya Qatar kukuza uhusiano na kuendeleza ushirikiano uliopo katika yake na Zanzibar katika sekta mbali mbali za kijamii, ikiwemo elimu, maji na Afya.
Alisema nchi hiyo imekuwa ikitoa watalii wengi wanaozitembelea nchi mbali mbali duniani ikiwemo Zanzibar, miongoni mwao wakitoka katika Familia ya Kifalme.
Aliahidi kubeba dhima ya kuwashajihisha wawekezaji wa nchi hiyo kuja nchini kuwekeza, ikiwa hatua ya kukuza ushirikiano uliopo.
Aidha, alimuomba Mwenyezi Mungu kuondokana na ugonjwa wa Corona unaoikabili Dunia hivi sasa, ili nchi hiyo iweze kukamilisha maandalizi yanayoendelea ya Kombe la Dunia.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar