NA BAKAR MUSSA,PEMBA.
WAANDISHI wa habari wametakiwa kuwa makini na utayari katika kupokea na kuihabarisha jamii juu ya habari za Covid 19 na chanjo zake ili kuitowa hofu kutokana na ugonjwa huo kuitikisa Dunia hadi sasa.
Ushauri huo umetolewa na Dk, Mwadini Ndosi kutoka Uingereza wakati akitowa taaluma kwa waandishi wa habari wa Vyombo mbali kwa njia ya mtandao Zoom, juu ya ugonjwa huo na usalama wa chanjo yake.
Alisema ugonjwa wa Covid 19 upo Duniani ambao unasababishwa na virus na sio laana kama inavyodhaniwa na tayari umeshawapata watu wa mataifa mbali mbali wakiwemo waliohai na wengine waliopoteza maisha yao.
Alieleza kutokana na hilo tayari imeelezwa kuwa zaidi ya watu wapatao million 3.7 duniani kote walishafariki kwa ugonjwa huo kwa taarifa za wiki moja iliopita.
Dk, Ndosi, alisema virusi hivyo vimekuwa vikishambulia kwa haraka sana ambavyo viko vya aina mbali mbali kama vile Alpha vilivyoshamulia sana Uingereza, Beta, ulishamubulia Afrika Kusini na kupoteza watu wengi, Gemma –Brazil, Delta vilivyoshamuliwa nchini India ambako watu kadhaa waliambukizwa na wengine kupoteza maisha yao.
Alifahamisha kudhibiti ugunjwa huo ni muhimu zaidi kuliko kutibu kutokana na athari zake kuwa nyingi hivyo mataifa mbali mbali yamefanya utafiti wa Chanjo yake na baadhi yake kuthibitishwa na kuwa
ziko salama kwa afya ya binaadamu.
“ Tayari Duniani kumeshapatika chanjo 15 lakini kati ya hizo ni 5 tu ambazo kwa sasa zimeshathibitishwa kufanya kazi na kutokana na tafiti mbali mbali zilizofanyika zimeonekana ziko salama kwa maisha ya watu,”alisema Dk, Ndosi.
Alisema Covid 19 haina tiba kutokana na kwamba , kinga yake haidumu,inaathiri sehemu ya maisha ambapo kinga za msingi ni kujitenga (lockdown) ambayo ni kinga ya jumla na muhimu.
Aliwataka Waandishi wa habari kuulezea umma juu ya hali halisi ya ugonjwa huo na chanjo zake kuwa ni salama kutokana na kwamba hata chanjo ikithitishwa kutumika huwa imeshafanyiwa utafiti wa kina na mamlaka husika sio zaidi ya awamu tatu hadi nne.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa USaid,la Marekani ,Kate soomvong siri, aliwapongea Marais wote wa wawili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar kwa kujitowa hadharani kuulezea ugunjwa huo wa Covid 19 na chanjo zake kwa wananchi wanaowaongoza.
Alisema chanjo zilizothibitishwa ni salama na zinafanya kazi hivyo waandishi wanawajibu wa kuungana na viongozi wao wa nchi kuwaeleza wananchi ukweli wa jambo hilo.
Hata hivyo mkufunzi kutoka Internews , Ali Haji Mwadini wakati akiwasilisha mapendekezo 19 ya kamati maalum ya Covid19 ilioundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alisema ni wajibu wa waandishi kufanya kazi zao kwa kuelekeza nguvu zao kwenye ripoti hiyo.
Alieleza kuwa waandishi wa habari wanayodhima kubwa ya kuwapatia taarifa sahihi wananchi juu ugonjwa huo na kuwapa fursa ya kuuliza ili kupata habari sahihi kuhusiana na Covid19 na chanjo zake ili kuwatoa hofu waliokwisha kuijenga mioyoni mwao.
Aliwataka kuandika na kutayarisha habari zenye uhakikika kwa maslahi ya jamii juu ya ugonjwa huo na wachapuze kuwaonana na viongozi wa Serikali ili taarifa sahihi ziweze kupatikana.
“ Waelezeni wananchi utafiti iliofanywa na taasisi kubwa za kimataifa kuhusiana na Chanjo ya Covid 19 na usalama wake ili waondowe hofu walionayo,”alisema Ali.
Hata hivyo alisema waandishi wanapaswa kuelewa kuwa mapendekezo yaliotolewa na kamati hiyo sio ya utekelezaji wamtu mmoja mmoja badala yake watumie kalamu zao kueleza hali ya ugonjwa huo ulivyo kwa ukweli na uwazi ili upate kufahamika.
Nae Mkufunzi Daniel Mwingira , wakati akiwasilisha mada juu ya wajibu wa Vyombo vya habari na Covid 19, alisema waandishi wanalo jukumu la kuhakikisha hanari wanazozitowa kuhusu Covid 19 wamezifanyia utafiti na kuziandika kwa usahihi na kwa wakati ili kuepuka kuandika habari za
uzushi.
Alieleza kwenye takwimu za Covid 19 ni lazima wawe amakini sana kwa kutafuta kwenye mamlaka zilizoruhusiwa kisheria na kuzihakiki zinausahihi wa kiasi gani kabla ya kuzieleza kwa jamii .
“ Jaribuni kuuliza takwimu za Covid 19 kutoka kwa watalamu husika ili muweze kujenga mtazamo mzuri kwa jamii kwa vile hili jambo ni muhimu sana kwa wananchi kutaka kufahamu kuliko kuchukuwa takwimu kwenye mitandao ambazo nyengine haziko sahihi,”alieleza.
Alisema ni vyema kuwa waangalifu wanapoandika habari za Covid19 na takwimu zake kwani uapatikanaji wa takwimu sahihi kutaiwezesha Serikali kuchukuwa hatuwa stahiki kwani iko mitandao maalumu ambayo mukiingia mtapata takwimu sahihi na zilizothibitishwa.
Aliitaja mitandao hiyo kuwa ni pamoja na WHO,International Organisation, Vyuo vikuu vya tafiti mbali mbali, Serikali , taasisi za takwimu nk.
Daniel, alisema kuwa mwandishi anapoandika habari za uzushi sio tu kuupotosha Umma bali anajivunjia heshima yake na chombo chake kwa ujumla na kukosa kuaminiwa na wasikizaji wake na kukitia hasara kubwa.
Alieleza ni lazima waandishi wa habari kuwa tayari kutowa taarifa sahihi za Covid 19 na Chanjo zake ili kujenga ushawishi mkubwa kwa wananchi na sio kuandika habari za kuwajengea hofu.
Alisema kuna haja kwa waandishi wa habari kuiomba Serikali kutowa ushirikiano na vyombo vyao na kuwa tayari kupata habari za kweli na uwepo wa Covid 19.
Nae, Shaaban Maganga kutoka Internews akifunga mafunzo hayo aliwaomba washiriki wote kuyafanyia kazi mafunzo waliopata kwa kuandika habari kwa weledi na kuwa tayari kuihoji Serikali juu ya Covid 19 ili wananchi wajuwe uwepo wake na usalama wa chanjo hizo.
Hata hivyo alisema ana imani waandishi watazitumia kalamu zao vizuri kuihabarisha jamii kujikinga na Ugonja huo kwani Tanzania haitokuwa salama kwa vile nchi za jirani uko ugonjwa wa Covide 19 japo kwa kiwango kidogo.