Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na kuhutuba katika mkutano wa kujadili uimarishaji wa biashara ndani ya Afrika Mashariki akihimiza umuhimu wa wafanyabiashara kuchangamkia fursa zinazopatikana ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, akimuwakilisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi. uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya verde mtoni jijini Zanzibar.
Washiriki wa Mkutano wa kujadili uimarishaji wa biashara ndani ya Afrika Mashariki wakifuatilia hotuba ya Katibu Mkuu wa (EAC) Dk. Peter Mathuki uliofanyika katika Ukumbi wa Hotel ya Verde Mtoni.
Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwa pamoja na viongozi wengine katika Mkutano wa kujadili uimarishaji wa biashara ndani ya Afrika Mashariki.
Na.Kassim Abdi. – OMPR Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Baraza la Biashara la Afrika Mashariki na Jumuiya ya wafanyabiashara Zanzibar katika kuwaunganisha wafanyabiashara wake.
Rais Dk. Mwinyi alieleza hayo katika hotuba iliosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika kikao cha kujadili uimarishaji wa Biashara ndani ya Afrika Mashariki kikao ambacho kimefanyika katika ukumbi wa Hotel ya Verde iliopo Mtoni.
Alileza kuwa, kufanyika kwa Mkutano huo kutasaidia kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara wa Zanzibar ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kuzitambua fursa zinazopatikana Zanzibar ambazo zitatoa nafasi kwa wafanyabiashara wa Afrika Mashiri kuzichangamkia.
Makamu wa Pili wa Rais alisema Jumuiya za wafanyabiashara zina kazi kubwa ya kuwaunganisha wafanyabiashara, kuonesha fursa pamoja na kuwapatia majukwaa ya kueleza changamoto wanazokabiliana nazo kwa lengo la kuzitarifu mamlaka husika ziweze kuchukua hatua.
“Mkutano huu utatoa tija kwa wafanyabiashara kufahamu fursa za kibiashara na uwekezaji ndani ya Jumuiya yetu sambamba na kupata jukwaa la kuelezea changamoto zao ili ziweze kupatiwa ufumbuzi” Alisema Makamu wa Pili wa Rais
Kupitia Mkutano huo Makamu wa Pili wa Rais alimueleza Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Mhe. Dk. Peter Mutuku Mathuki kwamba wafanyabiashara wa Zanzibar ni waamifu wana uwezo mzuri kutokana na Zanzibar kuwa kitovu cha Biashara Afrika Mashariki kwa Karne nyingi sasa.
Alifafanua kuwa, wazanzibar wanajulikana kwa umahiri na ustadi wao katika sekta ya biashara na ujasiri wa kutanua biashara zao katika Pembe tofauti za dunia hivyo, ujio wa kiongozi huyo kutafungua milango Zaidi ya kuwaingiza wafanyabiashara wa Zanzibar katika nchi sita wanachama wa Jumuiya.
Akizungumzia suala la uwekezaji Mhe. Hemed aliwaeleza wafanyabiasha hao kwamba kwa sasa Zanzibar inadhamiria kuinua uchumi wake kupitia uchumi mpya unaofahamika kama Uchumi wa Buluu(Blue Economy) unaojumuisha Uvuvi wa bahari Kuu, Miundombinu ya Bandari na usafiri, mafuta na gesi, utalii na maeneo mengine.
Alisema Zanzibar imekusudia kutekeleza uwekezaji mkubwa kupitia sekta ya kilimo cha kisasa, Ujenzi wa nyumba za makaazi (Real estate, pamoja na biashara na huduma jambo ambalo litaimarisha maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki.
Nae, Waziri wa Biashara na maenedeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe. Omar Said Shaaban aliwahakikishia wafanyabiashara wa Afrika Mashariki kuwa serikali kupitia wizara anayoisimamia itahakikisha nembo ya ZBS inatambulika ndani Jumuiya hiyo kwa lengo la kuwaondoshea wafanyabiashara wake vikwazo.
Mhe. Omar Said alimshauri Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mikutano yao mingi ya kikanda kuifanyia Zanzibar ili kujenga uwelewa Zaidi kwa wanachama wake waliopo Zanzibar.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dk.Peter Mathuki alisema ziara yake nchini Tanzania imeza matunda kwa kuonana na kubadilishana mawazo na Rais wa Jamuhuri ya Mungano wa Tanzania Mhe. Samia Suhuhu Hassan ambapo Katibu Mkuu huyo alisisitiza lugha ya Kiswahili kupewa kipaumbele kutumika kwa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Lazima Kiswahili tukipe kiupaumbele ikiwezekana itumike hata katika vikao vya Umoja wa Nchi za Afrika (A.U) na ikiwezekana katika vikao vya Umoja wa Mataifa (U.N)” Alisema Dk. Peter
Kuhusu Uchumi wa Buluu ambao serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka kipaumbele Dk. Peter alimueleza Makamu wa Pili wa Rais Kuwa hiyo ni fursa nzuri kwa wanachama wa Afrika Mashariki na aliahidi kwamba viongozi wa Jumuiya wataweka mikakati katika kuichangamkia fursa hiyo.
Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar Ali Suleman Amour alisema sekta binafsi inahitaji kuinuliwa ili kutoa manufaa kwa wafanyabiashara wa Zanzibar ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutokana na fikra nzuri walizonazo wafanyabiashara ikiwemo masuala ya uajasiriamali.