NA SAID ABRAHMAN.
MKUU wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, amesema suala la vitendo vya udhalilishaji kwa watoto katika Mkoa wake halitofumbiwa macho.
Alisema kuwa masuala yote ambayo yanamuhusu mtoto watayasimamia kwa pamoja, kwani bado kuna baadhi ya wazee wanapinga kutoa ushahidi wa vitendo vya udhalilishaji katika vyombo vya sheria.
Salama aliyasema hayo huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Wete, wakati alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mikoa mawili ya Pemba, katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika.
Alisema kwa sasa wazee hao, ambao hawataki kutoa ushahidi Mahakamani watambue kuwa wako kikaangoni na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Kiukweli Mikoa yetu hii miwili ya Pemba, imejipanga vilivyo ili kuona vitendo vya udhalilishaji kwa wanawake na watoto vinamalizika kabisa, ole wao wale wazee ambao hawako tayari kutoa ushahidi kwenye vyombo vya sheria dawa yao sasa imepatikana,”alisema.
Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wananchi hao, kutoa mashirikiano yao kwa vyombo vya sheria hivyo ni kutekeleza amri ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi Dk. Hussein Ali Mwinyi kupinga vitendo hivyo.
“Ipo haja ya kushirikiana pamoja katika kupiga vita suala la udhalilishaji na tusiziachie jumuia pekeyao tu, ila tunakwenda sambamba ili kuona kwamba suala la udhalilishaji wa kijinsia ndani ya Mikoa yetu linadhibitiwa”,alisema Salama.
Mapema Mkuu huyo wa Mkoa alifahamisha kuwa kila ifikapo tarehe 16/6 ya kila mwaka, ni siku ya kitaifa ya Mtoto wa Afrika ambapo mataifa mbali mbali ya Afrika, huadhimisha siku hii ikiwa ni kukumbuka mauwaji ya watoto zaidi ya 176 yaliyotokea huko Soweto Afrika ya kusini mwaka 1976.
Mapema akimkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Wete Mgeni Yahya Khatib alisema kuwa vitendo vya udhalilishaji vinarudisha nyuma maendeleo ya taifa, hivyo ni wajibu wa wananchi wote kushirikiana pamoja katika kutokomeza vitendo hivyo.
“Niwaombe wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla tushirikiane kwa pamoja, katika kupiga vita vitendo vya udhalilishaji kwa watoto, kwani wao ndio tegemeo la taifa hapo baadae,”alisema Mgeni.
Mkuu huyo wa Wilaya alieleza kuwa vitendo vya udhalilishaji ni vibaya sana, vinachukiza katika jamii bila ya mashirikiano kutoka kwa wananchi na viongozi suala hili halitomalizika.
Nae Ofisa Mdhamini wa Wizara ya afya, Ustawi wa jamii na watoto Pemba Yakoub Shoka, alisema kuwa malezi na makuzi yanahitaji pande mbili (baba na mama) pamoja na jamii inayozunguka.
“Hili litaweza kusaidia pia kupata viongozi walio bora wa hapo baadae ambao wataweza kuliongoza taifa hili, alisema Ofisa Mdhamini huyo.
Hata hivyo Shoka aliwataka wananchi kisiwani Pemba, kupinga vitendo vya udhalilishaji ambapo suala hilo ni gumu na zito na halikubaliki katika jamii.
Nae Ofisa kutoka Idara ya Ustawi wa jamii Pemba Bizume Haji, alieleza changamoto ambazo wanakabiliana nazo katika Ofisi yao ni pamoja na uhaba wa vitendea kazi katika kufuatilia malalamiko mbali mbali kwa wateja wao, jambo linalotokana na ufinyu wa bajeti ya kuendeshea shughuli zao za kila siku katika Ofisi yao.
“Tunashirikiana na jamii kwa kufika Ofisini kwetu kuleta shida zao, kwa ajili ya kutatulia ikiwa ni pamoja na migogoro ya ndoa, madai ya mahari, nyumba, mashamba, pesa taslimu, kutoa huduma za watoto na vitendo vya udhalilishaji,”alisema Bizume.
Nae Mratibu wa SOS Gharib Abdalla Hamad, alieleza kuwa Shirika lake ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyojikita katika kutoa malezi bora kwa watoto, waliopoteza malezi ya familia au walio hatarini kupoteza malezi ya familia na kuwasaidia kupata haki zao za msingi kwa mujibu wa sheria.
Aidha Mratibu huyo alifahamisha kuwa SOS imejikita kusaidia watoto walio katika mazingira magumu zaidi ikiwemo mayatima, watoto wanaojilea, watoto waliotelekezwa, watoto waliozaliwa nje ya ndoa na watoto wanaoishi na wazazi wenye ugonjwa wa kudumu.
Hata hivyo Ghalib alisema licha ya mikakati inayofanywa na SOS kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, katika kudumisha Ustawi wa mtoto, SOS imependekeza kuendelea kuzijengea uwezo kamati za Shehia za kumaliza vitendo vya udhalilishaji, kwa wanawake na watoto kama ilivyoainishwa katika mpango kazi wa mwaka 2017/2022.
Aidha alitakja kuharakishwa kwa Upelelezi wa kesi zinazohusu masuala ya udhalilishaji, ili kuharakisha haki iweze kutendeka pamoja na kuwepo utaratibu wa kuwapatia msaada wa kisaikolojia wahanga wa vitendo vya udhalilishaji, ili waweze kukabiliana na athari za udhalilishaji ikiwemo msongo wa mawazo.
Katika maadhimisho hayo Ujumbe wa mwaka huu ni “Tutekeleze Agenda 2040: Kwa Afrika inayolinda Haki za Mtoto”.