NA ABDI SULEIMAN.
SHEHIA ya Makangale ya Wilaya ya Micheweni, imefanikiwa kutekeleza mpango kazi wake wa maendeleo ya jamii kwa asilimia tisini (90%), katika kuondosha kero za huduma ya elimu, afya, kilimo na uchumi jamii.
Hayo yameelezwa Afisa miradi ya Milele Zanzibar Foundation Fatma Khamis, katika ziara ya mafunzo kwa shehia 12 ambazo zimepatiwa mafunzo kupitia mabaraza ya mashauriano ya shehia, juu ya kuandaa mpango kazi wa maendeleo ya jamii katika sekta ya afya, elimu, kilimo na uchumi jamii ili kuondosha kero zinazowakabili wananchi huko Makangale Wilaya ya Micheweni.
Alisema sababu iliyopelekea kufanya vizuri ni kutokana na mipango yao yaliojiwekea, hali iliyofikia Makangale kuongoza katika shehia hizo.
Alifahamisha kutokana na hali hiyo, Milele imeona bora shehia nyengine kufika makangale na kujifunza na kuwa somo kwao na kwenda kuifanyia kazi katika shehia zao.
“Niwazi sasa hizi kamati za mashauriano za mabaraza ya shehia haya, kuongeza bidii katika kubuni miradi itakayo zikomboa jamii zao na kufikia malengo waliyojiwekea, kama walivyofanya wenzetu hawa wa makangale”alisema.
Fatma alisema lengo la kuanzishwa kwa kamati hizo za shehia, ni kupeleka maendeleo yatakayosaidia jamii kujikomboa na umaskini, pamoja na kuhakikisha taasisi nyengine zinaunga mkono katika maendeleo yao.
Kwa upande wake Afisa ufuatiliaji wa miradi ya Milele Zanzibar Foundation, kutoka shehia ya Makangale Hassan Suleiman Khamis alisema siri ya mafanikio hayo ni kuwashajihisha wananchi, kuanzisha miradi na kuwaunganisha na taasisi husika.
Alisema kwa upande wa Elimu wameongeza mambanda ya kusomea skuli ya mnarani na kuongeza huduma katika kituo cha afya kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Micheweni.
“Tumeweza kushirikiana na kuanzisha vikundi vya akina mama na vijana, kwa kuanzisha shughuli mbli mbali za kimaendeleo ambazo zinapatikana katika shehia hiyo”alisema.
Aidha alivitaja vikundi ambavyo vimeanzishwa kuwa ni, Vikundi vya ujasiriamali wa kusarifu mwani, vikundi vya ushoni kwa vijana, vikundi vya uvuvi ili kuwafanya vijana muda wote kuwa bize na harakati za maisha.
Baadhi ya wajumbe wa kamati hizo za mashauriano, kutoka shehia nyengine wamesema ziara hiyo imeweza kuwa kuwafumbua mamcho na kuona elimu hiyo wanaifikisha katika shehia zao.
Jumla ya shehia 12 ambazo zimo katika mradi huo zimeshiriki katika ziara hiyo ikiwemo shehia ya Mkungu, Kangagani, Mkungu, Michenzani, Kigongoni, Msuka, Mtambwe, Mjenzi, Vikunguni, Birikau, Sizini na Makangale.