Monday, November 25

WAFANYABIASHARA kisiwani Pemba wametakiwa kufuata Sheria na taratibu zinazotakiwa katika kuingiza bidhaa.

AFISA Mdhamini wa Wizara ya afya,Ustawi wa jamii, Wazee,Jinsia na Watoto Pemba Yakoub Muhammed Shoka (wa kwanza kulia), akijumuika na wafanyakazi wa wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi pamoja na wafanya biashara ya Vyakula na Dawa katika dua ya ufunguzi wa jengo la Ofisi hiyo huko Kilimandege Wete, Mwenye koti jeusi ni Mkurugenzi wa Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi Nassir Salum Buheti
BAADHI ya wafanyabiashara ya Vyakula na Dawa wakiwa katika dua ya pamoja ya ufunguzi wa jengo la Ofisi ya Wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi huko Kilimandege Wete,
AFISA Mdhamini wa Wizara ya afya Ustawi wa jamii Wazee Jinsia na Watoto Pemba Yakoub Muhammed Shoka (wa tatu kutoka kulia), akiungana na wafanyakazi wa wakala wa Chakula, Dawa na Vipodozi pamoja na wafanya biashara ya Vyakula na Dawa katika dua ya pamoja ya ufunguzi wa jengo la Ofisi hiyo, huko Kilimandege Wete.

(PICHA NA SAID ABDULRAHMAN PEMBA)

ZUHURA JUMA, PEMBA

WAFANYABIASHARA kisiwani Pemba wametakiwa wafuate Sheria na taratibu zinazotakiwa katika kuingiza bidhaa, ili kuweza kuepusha madhara yanayoweza kutokea kwa watumiaji.
Akizungumza mara baada ya kumaliza dua maalumu kwa ajili ya ufunguzi wa jengo la Wakala wa Dawa na Chakula (ZFDA) Pemba, Afisa Mdhamini Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Yakoub Mohamed Shoka alisema, ni muhimu kwa wafanyabiashara kufuata taratibu za uingizaji na uhifadhi wa bidhaa.
Alisema kuwa, ipo haja kwa wafanyabiashara hao kuchukua bidhaa ambazo hazijapitiwa na muda sambamba na kuzihifadhi katika sehemu nzuri, ili ziwe salama kwa matumizi ya binadamu.
“Tushirikiane pamoja kuhakikisha bidhaa zinazoletwa zinakuwa salama kwa ajili ya kuimarisha afya za wananchi”, alisema Mdhamini huyo.
Aidha, aliwataka wafanyakazi wa kitengo hicho, kufanya kazi kwa umoja na mashirikiano, jambo ambalo litasaidia kufanya kazi kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa ZFDA Pemba Nassir Salum Buhet aliwashukuru wadau wote waliohudhuria dua hiyo na kusema kuwa wamefarajika sana kwa ushirikiano waliouonesha.
“Kwa kweli tumepata faraja kuona wadau wetu na jamii kwa ujumla wamejumuika na sisi kwa pamoja kuja katika dua hii, tunawashukuru sana”, alisema.
Mkurugenzi huyo aliiomba jamii na wafanyabiashara kuzidisha ushirikiano katika utendaji wa kazi zao, kwani wao wanafanya kazi kwa mujibu wa Sheria na kwa lengo la kumlinda mtumiaji asipate madhara kwa bidhaa zilizopitiwa na muda ama zilizokuwa hazikuhufadhiwa vizuri.
“Sisi tunafanya kazi zetu kwa mujibu wa Sheria na sio kwamba tunawakomoa wafanyabiashara wetu,  hivyo tuwe pamoja katika hili na musituone kama tunawaonea, tunamlinda mtumiaji ili asipate madhara”, alisema.
Nao wadau walioshiriki katika dua hiyo walisema ni jambo muhimu katika kujiombea kheri na baraka kwenye utendaji wa kazi zao za kila siku na kuwaombea kwa Allah awape nguvu ya kufanya lile linalotakiwa kwa moyo wa imani na uvumilivu.