Saturday, January 18

MICHEZO YA MPIRA WA KIKAPU, WAVU YAVUTIA WENGI UMISSETA

Mashabiki wa timu ya mpira wa wavu ya mkoa wa Arusha wakishangilia timu yao wakati ilipopambana na Iringa katika mojawapo ya michezo ya mpira wa wavu iliyochezwa leo ambapo Arusha ilishinda kwa seti 3-0

Mashabiki wa timu ya mpira wa wavu ya mkoa wa Iringa nao wakiishangilia timu yao ambapo timu hiyo ilifungwa na Arusha seti 3-0

Nyota wa mchezo wa leo kati ya Iringa na Arusha Daniel Antony Wambura, ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano kutoka shule ya sekondari ya Longido akipiga spike ya mwisho iliyoiwezesha Arusha kushinda mchezo huo kwa seti 3-0.

 

Na Mathew Kwembe, Mtwara

Ushindani mkali uliopo baina ya mikoa mbalimbali inayoshiriki katika mashindano ya UMISSETA inayoendelea katika viwanja mbalimbali vya Chuo cha Ualimu hapa Mtwara umekuwa kivutio kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia vipaji vya watoto wao.

Karibu michezo yote imekuwa ikivuta hisia za wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia michezon hiyo hususani mpira wa miguu, na katika siku tatu hizi za kwanza kivutio kingine ni mchezo wa mpira wa kikapu (Basketball) na Mpira wa wavu (Volleyball).

Wenyeji Mtwara wamekuwa na sifa ya kipekee ya kuwa na timu bora ya Volleyball ambapo mkoa huo ndiyo mabingwa watetezi wa mchezo huo kwa wasichana na katika mechi za leo Mtwara wavulana imeifunga Tabora seti 3-2, Kagera imefungwa na Mbeya seti 3-0 huku Mara ikifunga Pemba seti 3-0, na kwa wasichana Tanga imeifunga Kigoma  seti 3-0.

Katika mpira wa kikapu kwa wasichana Mwanza imeigaragaza Iringa  magoli 87-6, Geita imeichapa Lindi 27-19,na  Shinyanga imeikung’uta bila huruma Mtwara kwa magoli 20-0.

Katika mchezo wa Netiboli Mara imeifunga Arusha magoli 32-19, Manyara imefungwa na Pwani 20-31, Dar es salaam imeifunga Ruvuma magoli 37-9, Geita imefungwa na Songwe 18-32, Mtwara nayo imefungwa na Rukwa 15-34 na Unguja imekung’utwa na Singida magoli 12-29.

Katika mpira wa soka wasichana Manyara imeichapa Songwe magoli 3-0, Mara imeifunga Mtwara 3-0, Ruvuma na Rukwa zimefungana magoli 3-3 na Mwanza imeifunga Tabora 1-0.

Matokeo ya mpira wa mikono wavulana Lindi imeifunga Simiyu magoli 19-16, Mara imeifunga Dar es salaam 23-17, Singida imefungwa na Unguja magoli 11-37, Tabora imeichabanga Kigoma magoli 24-8.

Kwa upande wa volley ball wasichana Singida imefungwa na Tabora 5-14, Songwe imeichalaza Dodoma magoli 26-4, Rukwa imefungwa na Mbeya magoli 9-24, na Dar es salaam imeifunga Mara 17-11.