Saturday, January 18

Waridi wa BBC: Mfahamu Mkuu wa Wilaya ya Temeke Tanzania Jokate Mwegelo

Anne Ngugi BBC Swahili

Maelezo ya picha,Mkuu wa Wilaya ya Temeke nchini Tanzania Jokate Mwegelo

Jokate Mwegelo ni mwanamke mwenye umri wa miaka 34 na licha ya umri wake mdogo ni mkuu wa Wilaya ya Temeke , iliyopo Dar es Salaam Tanzania.

Mbali na hilo pia ni mmoja ya wanawake waliofanikiwa katika medani ya urembo nchini humo baada ya kuchukua nafasi ya pili katika mashindano ya malkia wa urembo nchini Tanzania mwaka 2006.

Anapoulizwa kuhusu swala la urembo yeye hutabasamu tu, akionesha mwanya uliopo kati ya meno yake, hali kadhalika kidoti cheusi kinachoshirikishwa na urembo kilichopo usoni mwake.

Sio vigumu kwa mtu anayemtafuta mkuu huyu wa wilaya miongoni mwa umati kumkosa kutokana na muonekano .

Vilevile bi Joketo ni miongoni mwa vijana maarufu sana nchini humo na sio ajabu kwamba katika mtandao wake wa Instagram ana wafuasi zaidi ya milioni 7.5 ,

Joketo akiwa amevalia sare zake za kazi

CHANZO CHA PICHA,JOKATE MWEGELO

Maelezo ya picha,Jokate akiwa amevalia sare zake za kazi

Ukitaka kugundua ufuasi wake mkubwa subiri anapoposti picha katika mtandao huo.

Lakini ni nini haswa kinachompatia msukumo maishani?

“Mengi ambayo nimeyaafikia katika maisha yangu yametokana sana na kujiamini na pia kuchukua muda wa kujijua mimi ni nani , haingekuwa rahisi kuwahudumia watu iwapo mimi binafsi sijielewei.”anasema Jokate

Jokate Mwegelo aliteuliwa katika nafasi ya ukuu wa wilaya ya Kisarawe kwa mara ya kwanza miaka minne iliyopita na hayati rais John Magufuli.

Wakati wa uteuzi wake alikuwa na umri wa miaka 31 ambapo alikuwa na sifa za kuwa miongoni mwa waigizaji bora nchini humo.

Mkuu wa mkoa wa Temeke nchini Tanzania Joketo Mwegelo

CHANZO CHA PICHA,JOKATE MWEGELO

Maelezo ya picha,Mkuu wa wilaya wa Temeke nchini Tanzania Joketo Mwegelo

Hatahivyo maisha yake yalikuwa yameegemea zaidi kwenye ulimwengu wa burudani na sanaa na ghafla uongozi ukabisha hodi .

Mara ya kwanza alipoteuliwa kuchukua wadhfa huo alihisi kana kwamba hana uwezo wa kusimamia wadhfa mkubwa kama huo. Ila miaka minne baadaye Jokate anaangalia nyuma yake na kufurahikia mno yale ambayo ameweza kuyafikia kwa kipindi kifupi cha uongozi wake.

Mojawapo ya jitihada zake ni upanuzi wa elimu, kupitia kuhakikusha kuna shule za kutosha katika eneo lake la utawala.

“Ari yangu kuu wakati nilitwaa uongozi ilikuwa ni kwa sekta ya elimu, wanafunzi maeneo haya wanakabiliwa na changamoto nyingi ,hasa kwa kuwa wanatembea mbali sana kuelekea shule. Kwa hio kuhakikisha kuwa kuna shule katika maeneo mbalimbali kwangu ni jukumu chanya”anasema Jokate

Sekta nyengine ambayo imeonekana kufanya vyema wakati Jokate akiwa msimamizi wa wilaya ya Temeke ni Chakula.

Jokate Mwegelo

CHANZO CHA PICHA,JOKATE MWEGELO

Sio mara moja au mbili mkoa huo umesheheni sherehe ambazo zinapigia upatu lishe bora na pia kutafuta mbinu ambazo wanawake wananufaika kupitia ujasiriamali wa chakula .

Jokate anasema kuwa Kisarawe ni mojawapo ya maeneo ambayo yanategemea kilimo ambacho ni uti wa mngongo huku wanawake wakiwa wanachangia pakubwa katika sekta hiyo.

Kwake yeye kumuwezesha mwanamke wa kawaida kupitia kuhakikisha ana mazingira bora ya kufanya biashara pamoja na kupata soko la chakula hicho ni kitu cha kujivunia

“Wanawake ndio wenye kuhangaikia maslahi ya jamii kuanzia asubuhi hadi jioni , hivyobasi kumuwezesha mwanamke wa kawaida Temeke ili kujimudu kunaendelea kufanyika , na wanawake pia wameonesha dalili za kuendeleza ujasiriamali “anasema Jokate

Majukumu ya kuwa Mkuu wa Wilaya anasema yalimfanya kuhamia Kisarawe suala lililomfanya kuwasahau marafiki zake wa jadi ili aweze kuwa karibu na wananchi wa eneo hilo kwa lengo la kuelewa matatizo yao na kuwahudumia.

Anasema kwamba uongozi wake katika eneo hilo haukumpatia uzoefu tu bali pia ukomavu zaidi kwasababu eneo hilo lina mchanganyiko wa vijana na wazee ambao wote wamekuwa wakimtegemea kwa maamuzi .

Kutoka kuwa Mlimbwende hadi mkuu wa mkoa wa Temeke Tanzania

CHANZO CHA PICHA,JOKATE MWEGELO

Maelezo ya picha,Kutoka kuwa Mlimbwende hadi mkuu wa mkoa wa Temeke Tanzania

Anaongezea kwamba changamoto za uongozi zinazowakabili wanawake , zaidi ni za kibinafsi kuliko wanazokumbana nazo katika majukumu yao ya kila siku.

Kwa mfano anasema kuwa pale wanawake wanaposusia nafasi hizo za kazi kutokana na kujiona kama wasiobora kuliko wanaume , basi tayari huwa wamejitoa wenyewe .

Siri kuu ya kufanikiwa kwake anasema kunatokana na kujiamini katika hatua zake zote kando na kuwa amepata elimu ambayo inamuwezesha kukabiliana na majukumu .

“Ni kweli kuna baadhi waliouliza ni kwanini mimi niliteuliuwa, ila mimi niliuliza mbona isiwe mimi?”

Tangu nilipoteuliwa sijawahi kuwafikiria baadhi ya watu walionisuta na kuzua kila aina ya maneno.

Anasema kwamba Kumsuta huko kulimpa msukumo na ari mpya ya kuwa bora zaidi.

”Hebu tazama nilipo sasa ,” anasema jokate

Anaongezea kwamba suala jingine ni kuhusiana na wanawake viongozi kushtumiwa kuwa hawashughuliki katika kuwainua wanawake wengine katika nafasi sawia .

“Kuna wale wanaosema kuwa mwanamke ni adui ya mwanamke mwengine, ila mimi siamini hilo, ninaamini kuwa kwa mfano katika nafasi hii niliyo nayo kama mkuu wa wilaya, nimewachochea mabinti wanawake vijana kufahamu kuwa inawezekana wakaafikia nafasi kama hii au zaidi licha ya kwamba , siwezi kumsaidia kila mwanamke”

Mkuu wa MKoa wa Temeke Joketo Mwegelo

CHANZO CHA PICHA,JOKATE MWEGELO

Anasema kwamba amejaribu awezalo kuona kuwa ndoto za wanawake wengi zinatimia.

Wiki hii ameapa na kuwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke baada ya kuhamishiwa wilaya hiyo na Rais Samia Suluhu Hassan katika uteuzi alioufanya mwishoni mwa juma lililopita.

Kwa Joketi, hiyo ni fursa ya kuendelea kuchota uzoefu wa uongozi na kutumia kipawa chake katika kuhudumia jamii.

Je kuna upweke wa kukosa jamii binafsi ?

Mara kwa mara katika mahojiano na mazungumzo yangu naye amekuwa akiliepuka swali hili – Je atafunga ndoa wakati upi?.

Majibu ya Jokate Mwegelo yamesalia kuwa muda wa hayo utakuja kwani ni kitu ambacho amekitamani .

Kwake yeye anatambua nafasi kubwa ya mwenyezi Mungu kumsaidia kuafikia hilo .

Swali jingine nililomuuliza ilikuwa Je, wewe kama mkuu wa Wilaya aliye mwanamke, hukosi upweke wa kukosa familia?

Jokate anajibu akitabasamu kuwa majukumu na malengo ambayo yuko nayo hayampi nafasi ya kuhisi upweke kwani anafahamu kuwa kuna muda na saa wa kufanya kila jambo .

Jokate mwegelo

CHANZO CHA PICHA,JOKATE MWEGELO

Anasema kuwa nafasi ya wanawake huwa kana kwamba tayari imeshachorwa na jamii kuanzia atakapozaliwa , jinsi ataingia kwenye ndoa na majukumu yake mengi akiwa ndani ya ndoa.

Anaongezea kwamba , kwa hilo jamii haijatoa nafasi ilio wazi kama ilivyo kwa wanaume hasa kuhusu masuala ya taaluma .

Anahoji kuwa ndiposa umuhimu wa mwanamke kuolewa na kupata watoto katika wakati Fulani unatiliwa mkazo licha ya malengo na matarajio yake katika siku za usoni .

Mbali na kuwa afisa wa serikali ,Jokate pia ni mjasiriamali ambapo ni mkurugenzi wa kampuni ya Kidoti anayomiliki .

Kidoti ni kamapuni ambayo aliitimua katika kueneza ulimbwende , pamoja na mitindo mbalimbali ya fesheni na kadhalika .

Mwaka 2012 baada ya kufungua kampuni yake ya Kidoti Loving ambayo inauza bidhaa mbali mbali za urembo na hasa nywele , kampuni yake ilifanya vizuri sana na kuanza kuzalisha bidhaa zingine kama vile mabegi ya shule na ndala.

Mwaka 2017, mafanikio hayo yalimfanya kupata tuzo ya malkia wa nguvu katika kitengo cha ubunifu wa biashara.

“Huwezi kunishusha chini kirahisi, najiamini sana na kile Mungu amenipa nafanyia kazi vipaji vyangu na nafanyia kazi taaluma yangu kwa nguvu zote na nina imani thabiti juu ya kile ninafanya kwa jamii yangu” Jokate anasema

Lakini Je Joketo Mwegelo ni nani haswa?

Jokate Urban Mwegelo, aliteuliwa mwaka wa 2018 na Hayati Rais John Pombe Magufuli kuwa mkuu wa wilaya ya Kisarawe iliyopo katika mkoa wa Pwani Tanzania.

Alizaliwa Marekani mahali ambapo wazazi wake walikuwa wanafanya kazi.

Lakini amesoma elimu ya msingi, sekondari na chuo kikuu Tanzania.

Waswahili husema nyota njema huonekana asubuhi, kwani mrembo huyu alianza kuwa kiongozi tangu akiwa shule ya upili.

Safari yake ya urembo ndiyo iliyozaa fursa mbali mbali katika uigizaji na kupelekea kupata tuzo ya mwigizaji bora wa kike kupitia filamu ya Chumo katika tamasha la filamu la Zanzibar International Film Festival mwaka 2011.

Mwaka 2014, alipata tuzo ya mwigizaji bora wa kike katika filamu za Kiswahili kupitia filamu ya Mikono salama.

Na mwaka huo huo aliteuliwa kuwania tuzo ya Mjasiriamali wa mwaka katika tuzo za Africa Youth Awards.

Jokate mwegelo

CHANZO CHA PICHA,JOKATE MWEGELO

Jokate ana shahada ya sanaa katika sayansi ya Siasa na falsafa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Ameingia katika siasa kupitia chama tawala akiwa mmoja wa vijana wa UVCCM.

Baadaye alipata fursa ya kuwa Kaimu Katibu wa Uhamasishaji wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM).

Jokate pia alikuwa miongoni mwa wanachama 450 wa chama tawala cha CCM waliojitokeza kuchukua fomu za kuwania ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA). Hatahivyo hakufanikiwa kupata fursa hiyo.

Kupingwa kwake katika harakati za kisiasa si jambo geni, hasa baada Watanzania kuwa na maoni tofauti baada ya Bi Mwegelo kutangazwa kuwa mkuu wa wilaya ya Kisarawe. Wapo walio mpongeza na walioona kuwa hakustahili.

Hata hivyo anaongeza kuwa ni Mungu tu ndiye anayemsaidia kumpitisha katika mapito mbali mbali ambayo ameyapitia na kumpa nguvu kuweza kupigana kila siku kwani akiona vijana wenzie wanavyo hangaika hujifunza na kutambua kuwa ni sehemu ya maisha.

“Maisha si lele mama, maisha si kwamba kila siku itakuwa ni chokoleti na pipi kuna siku zingine itakuwa tafrani, lakini ndiyo sehemu ya maisha. Wanasema hakuna mafanikio bila changamoto,” anasema