Thursday, January 16

Makundi maalumu wapewe elimu ili kusaidia mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.

NA ZUHURA JUMA, PEMBA

KAMATI za kupambana na vitendo vya udhalilishaji Wilaya za Pemba zimesema, ipo haja ya kutoa elimu kwa makundi maalumu ikiwemo sehemu za maskani, ili kusaidia mapambano dhidi ya vitendo hivyo.

Wakizugumza wakati wa kuwasilisha ripoti ya robo mwaka katika Ukumbi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA) Mkanjuni Chake Chake Pemba ilisema, kwenye maskani kuna watu wenye tabia tofauti, hivyo ni vyema na wao wakapewa elimu ya GBV.

Wanakamati hao walisema kuwa, ipo haja ya kutoa elimu kwenye maskani kutokana na kuwa wanakaa watu wa rika tofauti na wenye tabia tofauti, jambo ambalo litawasaidia katika mapambano dhidhi ya udhalilishaji.

“Kwanye maskani kuna watumiaji wa dawa za kulevya, kuna na wenye tabia nyengine, hivyo tuelekeze nguvu huko kwa kutoa elimu, ili wapate uwelewa na watatusaidia kusambaza elimu hii kwa wengine”, walisema.

Massoud Abdalla Massoud kutoka Wilaya ya Mkoani alisema, elimu zaidi inahitajika kwa jamii kwa kupita kila shehia na kutoa vipeperushi, hali ambayo itafanikisha sana kwani itafikia wananchi wote.

Kwa upande wake Siti Ali Faki kutoka Wilaya ya Wete alisema kuwa, ili kesi hizo zimalizike na kupata hukumu kwa haraka, ni vyema Jeshi la Polisi liharakishe upelelezi sambamba na mahakama kuleta hakimu mkaazi kisiwani Pemba.

Nae mwalimu Mkuu skuli ya Mtambwe Kusini Mussa Juma alieleza kuwa, udhalilishaji ni vita inayohitaji mapambano ya hali ya juu, hivyo jitihada za makusudi zinahitajika ili kuhakikisha wanadhibiti.

“Jamii inakata tamaa, kesi zinakaa muda mrefu hazijamaliza, watu wanaacha kazi zao na wakaamua kuripoti na kufuatilia kesi ila hakuna linalokuwa, kuna kesi katika shehia yetu ni mwaka wa tatu haijamaliza na wala hawaulizwi kitu”, alisema.

Akizungumzia suala la mashahidi Asha Juma Omar kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii Wilaya ya Micheweni alisema, mashahidi wanajitahidi kufika mahakamani ingawa wanapokenda mara kadhaa wanaambiwa hakimu hayupo, hivyo husababisha kutokwenda wanapoitwa tena.

“Wakati mwengine tunatoa pesa zetu mifukoni ili kuwapa hamasa ya kwenda mahakamani, lakini shahidi ataitwa zaidi ya mara tatu hakimu hayupo, hivyo wanakuwa hawana nauli ya nenda rudi na hali zetu ni duni jamani, tuwahurumie”, alisema.

Alisema kuwa, changamoto nyengine ni kutoroka kwa watuhumiwa hali ambayo inakwamisha kesi hizo kupata hukumu na kusababisha watoto kufanyiwa vitendo hivyo kila siku.

Alieleza kuwa, kati ya kesi za udhalilishaji walizopokea, kesi sita (6) ni za ujauzito ambazo zimeripotiwa kwa kipindi cha miezi mitatu katika Wilaya ya Micheweni.

Mratibu wa Kituo cha Mkono kwa Mkono Wilaya ya Micheweni Nassor Said Amour alisema kuwa, ili kufanikiwa katika kuutokomeza udhalilishaji, kunahitajika ushirikiano mkubwa kwa jamii na wanaharakati wa kupambana na vitendo hivyo.

“Kwa kweli tunafika pahala tunavunjika moyo kutokana na baadhi ya watu kwamba wapo vizuri kusema tu na sio kutekeleza kwa vitendo, unajitahidi kupambana lakini wenzako wanakurudisha nyuma, naomba tushirikiane jamani”, alisema Nassor.

Aidha alisema kuwa, kumekuwa na tabia ya walimu kuwapiga vibaya wanafunzi, hivyo wachukue juhudi ya kuwaadabisha na sio kuwapiga kupita kiasi, kwani ni kuwadhalilisha na hatimae kupata madhara.

Afisa Mawasiliano kutoka TAMWA Pemba Gaspary Charles alieleza kuwa, ni wakati sasa wa kuelimisha jamii zaidi, ili mahakimu wasipate mwanya wa kuyaondoa mashitaka kwa kisingizio cha kukosekana kwa mashahidi.

Mkutano huo wa kuwasilisha ripoti ya robo mwaka, imezishirikisha kamati za udhalilishaji za Wilaya Pemba, lengo ni kuweza kuboresha kwa ajili ya kupambana na vitendo hivyo.