Monday, November 25

Siku 100 za Rais Samia Suluhu: Jinsi Tanzania ilivyorudi katika ulimwengu wa diplomasia

Mara baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kurejea Tanzania kutoka Kenya alikofanya ziara yake ya kwanza ya kiserikali nje ya nchi, mmoja wa mabalozi wastaafu wa Tanzania alimwandikia muandishi wa makala hii ujumbe kupitia simu ya mkononi ukisema; “Ziara yenye mafanikio kidiplomasia kuzidi zote katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.”

Labda mwanadiplomasia yule alikuwa ameweka chumvi kidogo, lakini kwa kutazama na kufuatilia namna safari ile ilivyoripotiwa kwa kina kwenye vyombo rasmi na kupitia mitandao ya kijamii, ilikuwa vigumu kumbishia balozi.

Wakati wa ziara ile, ilikuwa kama vile kila aliyekuwa Tanzania au Kenya alikuwa akijua Rais Samia alikuwa wapi na anafanya nini katika muda wote wa ziara.

Ziara hiyo ilifanyika katika kipindi ambacho uhusiano baina ya Tanzania na Kenya ulikuwa katika kiwango cha chini pengine kuliko katika wakati mwingine wowote kwenye miaka 10 iliyopita.

Uhusiano kati ya Tanzania na Kenya haujawahi kuwa rahisi lakini wakati wa utawala wa Jakaya Kikwete – aliyekuwa akimchukulia Uhuru Kenyatta kama mdogo wake, kulikuwa na namna ya kutatua matatizo hata kwa kutumia ‘mlango wa nyuma.’

Samia na Kenyatta

CHANZO CHA PICHA,IKULU, KENYA

Kuna kipindi wakati wa utawala wa hayati John Magufuli ilionekana kwamba milango yote rasmi na isiyo rasmi ya mawasiliano ilikuwa imefungwa na matokeo yake ikawa ni diplomasia ya piga nikupige.

Kwa vile Kenya ndiye mwekezaji mkubwa zaidi Tanzania miongoni mwa nchi za Afrika, uhusiano baina ya nchi hizi ni wa kimkakati na hatua ya Samia kufanya ziara yake ya kwanza huko na ikapata mafanikio, ilikuwa ni mojawapo ya matukio muhimu kidiplomasia kwake katika siku zake za awali madarakani.

Kurejea katika misingi ya kidiplomasia ya Tanzania

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, mojawapo ya eneo ambalo serikali ya Tanzania ilikuwa imewekeza sana ni katika kutengeneza kada ya watumishi wabobezi wa masuala ya uhusiano wa kimataifa.

Nchi ilipata bahati ya kuongozwa na marais wawili; hayati Benjamin Mkapa na Kikwete ambao waliwahi kuwa mawaziri wa mambo ya nje na wakiamini katika kutengeneza kada ya watumishi wanaokidhi vigezo hivyo.

Magufuli hakuwahi kufanya kazi katika wizara ya mambo ya nje na alikuwa Rais wa kwanza wa Tanzania ambaye hakuwahi kufanya kazi wala kumwona Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, akishughulika na wana diplomasia kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake.

Kimsingi, Magufuli alikuwa akizungumza hadharani kwamba katika kipindi cha takribani miaka 20 ya kuwa waziri katika serikali za Mkapa na Kikwete, alisafiri si zaidi ya mara ya tano kwenda ughaibuni.

Kwa sababu hiyo, diplomasia yake ikawa ya kutazama ndani zaidi ya nchi yake – akipenda kutumia watu aliowaamini yeye kuliko wale waliopikwa kufanya kazi za uhusiano wa kimataifa kwa takribani miaka 20 nyuma.

Museveni na Samia

CHANZO CHA PICHA,IKULU, TANZANIA

Maelezo ya picha,Rais Samia pia emeendeleza mahusiano yaliayoasisiwa na mtangulizi wake Rais Magufuli, mathalani ujenzi wa bomba la mafuta na Uganda.

Alianza kazi kwa kumteua mwanadiplomasia mbobezi, hayati Dk. Augustine Mahiga, kuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika siku zake za awali madarakani lakini mara alipoweka mizizi, akamweka kipenzi chake, Profesa Palamagamba Kabudi, kuwa waziri wa wizara hiyo. Kabudi ni nguli wa masuala ya sheria na hakuwahi kufanya kazi mambo ya nje wakati wowote katika maisha yake kabla ya kupewa uwaziri.

Kihistoria, Rais wa Tanzania ana wizara tatu ambazo zinajulikana kuwa yeye ndiye kiongozi hata kama atampa waziri kuongoza wizara hiyo. Wizara hizo ni Fedha, Ulinzi na Mambo ya Nje. Sera za nchi kiulinzi, kifedha na kidiplomasia hutegemea sana maono ya rais kuliko yale yaliyoandikwa katika sera.

Kwa sababu hiyo, urais wa Magufuli uliakisi mawazo na mtazamo wake kuhusu uga huo – kama ambavyo mawazo na maono ya Mkapa, Nyerere na Kikwete yaliakisiwa pia katika maeneo hayo matatu.

Katika siku zake 100 za kwanza madarakani, Samia tayari ameonyesha kurejesha masuala ya uhusiano wa kimataifa kwa wanadiplomasia. Kwanza, alimteua mwanadiplomasia mbobezi, balozi Liberata Mulamula, kuwa waziri na baadaye akamteua mbobezi mwingine, balozi Lazaro Sokoine, kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

Ndani ya siku 100 za kwanza, Samia amefanya uteuzi wa mabalozi uliopongezwa na wengi kwa kuwapa nafasi vijana waliolelewa na kufunzwa na vyema kwenye eneo hilo na marais wawili wastaafu Mkapa na Kikwete.

Baadhi ya vijana hao wapya waliopewa ubalozi na Samia – kuashiria kwamba watapewa vituo vyao vya kazi baada ya kukamilika kwa michakato ya kidiplomasia ni; Togolani Mavura, Macocha Tembele, Elsie Kanza, Mindi Kasiga, Caesar Waitara, James Bwana na Robert Kahendaguza.

Kama kuna ujumbe ambao Rais Samia ameutoa katika siku zake 100 za kwanza za urais ni kwamba masuala ya uhusiano wa kimataifa yatafanywa na kuongozwa na watu waliosomea na kukulia katika eneo hilo.

Nafasi ya Tanzania kidiplomasia

Tanzania ilikuwa na bahati ya mambo mawili wakati wa muungano ulioitengeneza nchi hiyo; mosi Tanganyika kuongozwa na Julius Nyerere ambaye alikuwa na upeop mkubwa wa mambo ya nje wakati anaingia madarakani na Zanzibar kuwa na kiongozi wa aina ya Abeid Karume, ambaye ujanani kwake alifanya kazi ya ubaharia na hivyo kuifahamu dunia.

Waziri Mulamula na Balozi wa Marekani Tanzania

CHANZO CHA PICHA,WIZARA YA MAMBO YA NJE

Maelezo ya picha,Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Bi Liberata Mulamula ni moja ya wanadiplomasia wabobevu nchini humo.

Lakini, Tanzania ilipata pia bahati ya kuwa na viongozi wa aina ya Abdulrahman Babu, Salim Ahmed Salim na wengine ambao tayari walikuwa wameingia katika mitandao ya umajumui wa Afrika na uhusiano na viongozi wa kimataifa hata kabla ya Muungano.

Nyerere, kwa mfano, alikuwa tayari kuungana na Kenya kutengeneza Shirikisho la Afrika Mashariki yeye akiwa Balozi wake Umoja wa Mataifa (UN) na kumwachia Jomo Kenyatta urais wa Shirikisho hilo. Huo ulikuwa ni mfano wa imani yake katika masuala ya diplomasia.

Kwa sababu hiyo, pamoja na umasikini wake wa rasilimali na madhila mengine ya ukoloni mkongwe, Tanzania ilijijengea jina kubwa duniani kwa sababu ya sera zake za kutetea Waafrika, Ukoloni na kujikwamua kiuchumi miongoni mwa nchi zinazoendelea.

Nyerere aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Nchi za Kusini, Mkapa aliwahi kuongoza Tume ya Utandawazi Duniani na Kikwete bado anateuliwa katika masuala mengi ya kidiplomasia ikiwamo utatuzi wa mgogoro wa Libya na masuala ya maji duniani.

Huko nyuma, kulikuwa na dhana kwamba wakati wa mikutano ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) baadaye AU na UN, wajumbe wa nchi za dunia walikuwa wakirudi ukumbini kusikiliza wakati ilipotangazwa mjumbe wa Tanzania anakwenda kuzungumza.

Pengine hii ndiyo Tanzania ambayo Rais Samia anataka kuirejesha.

Kwanini diplomasia ni muhimu?

Rais Samia

CHANZO CHA PICHA,IKULU, TANZANIA

Maelezo ya picha,Mara baada ya kuingia madarakani mwezi Machi, Rais Samia alieleza bayana kuwa kufufua mahusiano ya kimataifa ilikuwa ni ni moja ya kipaumbele chake.

Tangu aingie madarakani, tayari Rais Samia ameshafanya mikutano kwa njia ya mtandao na karibu viongozi wote wa taasisi za kimataifa kwenye maeneo ya uchumi, uhusiano wa kimataifa na fedha.

Kuliko katika wakati mwingine wowote, dunia sasa inakabiliwa na changamoto ambazo namna bora zaidi ya kukabiliana nazo ni kwa ushirikiano kupitia nchi na nchi na kupitia jamii ya kimataifa.

Namna ya kukabili matatizo kama ugaidi, magonjwa ya aina ya Uviko 19, tabia nchi na mengine ambayo ndiyo changamoto za kizazi cha sasa cha dunia yanaweza tu kutatuliwa kupitia mahusiano haya na diplomasia.

Kwa nchi masikini kama Tanzania, namna pekee ya kupiga hatua ni kutumia diplomasia vema katika uhusiano na taasisi nan chi nyingine. Kuna msemo wa wahenga unaosema; “Kama unataka kwenda haraka, tembea peke yako. Kama unataka kwenda mbali, nenda na wenzako”.

Pengine hiyo ndiyo falsafa inayoongoza utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan