- Ezekiel Kamwaga
- Mchambuzi
Ukimuuliza mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wapi alipo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, kwa sasa, atakwambia yupo katika mojawapo ya mikoa ya Tanzania akifanya shughuli za ujenzi wa chama.
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, hivi karibuni alihojiwa na vituo vya redio, magazeti na televisheni kutoa maoni yake kuhusu bajeti ya serikali iliyotangazwa hivi karibuni.
Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) sasa wanakosoa hadharani baadhi ya kasoro na makosa yaliyokuwa yakifanywa na serikali wakati wa utawala wa Rais John Magufuli ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa chama tawala.
Kama mtu aliyeishi Tanzania kwa miaka mitano iliyopita na akahamia kuishi sayari nyingine na kurejea wakati huu, anaweza kudhani kwamba amehamia katika nchi tofauti na aliyoishi.
Kwa maana ya uhuru wa kuzungumza na kutoa maoni, Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan – walau katika siku zake 100 za kwanza madarakani, imepiga hatua.
Mbowe na Zitto walikuwa mojawapo ya wahanga wa utawala wa awamu ya tano – wakitumia siku nyingi katika korido za mahakama tofauti kwa kesi zao binafsi au za watu wao wa karibu na wakati mwingine; kwa kiongozi huyo wa Chadema, kukaa gerezani kwa takribani nusu mwaka.
Uhuru huo wa maoni umeanza pia kuonekana katika vyombo vya habari.
Katika siku za karibuni, imeanza kuwa kawaida kwa magazeti kuandika katika kuraza zake za mbele habari kubwa za viongozi wa upinzani.
Hata yale magazeti yaliyokuwa yakifahamika kwa kukashifu na kubagaza viongozi wa upinzani nayo yamepunguza makali.
Kwa miaka yote tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania, baadhi ya haya mambo yalikuwa ya kawaida na yalichukuliwa kama utamaduni wa kawaida wa siasa za Tanzania.
Rais Samia alirithi utamaduni tofauti wa kisiasa ulioanza wakati wa Magufuli wa kubana uhuru wa kufanya shughuli za kisiasa na kiharakati ndani ya Tanzania.
Ambacho anakifanya taratibu, ni kuirejesha nchi walau katika zama za hayati Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete – watanguli wa Magufuli katika kiti cha urais.
Mifumo na sheria kandamizi ziko palepale
Katika ripoti ya mwaka 2019 ya taasisi ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu ya Human Rights Watch, Serikali ya Magufuli ilielezwa kwa kina namna inavyotumia sheria zilizopo na kwa kutunga nyingine zenye lengo la kukandamiza uhuru wa kutoa maoni na kufanya shughuli za kisiasa na harakati.
Katika siku 100 za Rais Samia madarakani, hajabadili sheria yoyote wala kuvunja mfumo wowote unaolea ukandamizaji. Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977 ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kuonya inampa Rais mamlaka ya kuwa dikteta akitaka, bado inatumika.
Kikubwa ambacho Rais Samia amebadili ni kutoa kauli zinazoashiria kutokubaliana na unyanyasaji wa raia na haki zao pamoja na kusisitiza utawala wa sheria.
Kitendo cha kumwondoa katika nafasi yake aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya, na kufikishwa kwake mahakamani kwa vitendo vyake viovu akiwa madarakani, kumeonyesha picha kwamba vitendo vya aina hiyo havitavumiliwa wakati wa utawala wake – hata kama hakuna sheria yoyote iliyobadilishwa.
Kwenye serikali ya Magufuli, Sabaya alikuwa mmoja wa viongozi waliokuwa wakichukuliwa kama alama ya utawala usiotaka upinzani wa aina yoyote na unaoamini katika matumizi ya nguvu katika kudhibiti wale wasiokubaliana na mwelekeo wake.
Rais Samia pia alimtoa aliyekuwa Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), Biswalo Mganga, ambaye ofisi yake ilikuwa ikilaumiwa kwa kufungua kesi zisizo na dhamana dhidi ya wapinzani wa serikali na CCM. Ingawa ameondolewa kwa kupewa cheo cha Jaji wa Mahakama Kuu, uwepo wa DPP mpya, Sylvester Mwakitalu, umeleta sura mpya katika mfumo mzima wa Haki Jinai (Criminal Justice).
Samia kubadili Katiba?
Pamoja na nia njema ambayo Rais Samia ameionyesha katika siku zake 100 za kwanza, vyama vya upinzani na wanaharakati wameanza kupigia kelele suala la kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa vile sasa imeonekana kutegemea hisani ya kiongozi mwema si jambo mwafaka tena.
Tayari vyombo vya juu vya maamuzi vya vyama vikuu vya upinzani vya Chadema na ACT Wazalendo vimeshatoa maelekezo kwa viongozi na wanachama wake kuongeza nguvu katika kupigia kelele jambo hilo – huku mrejesho kutoka CCM ukiwa kwamba jambo hilo si kipaumbele kwa sasa.
Samia alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba lililokaribia kupitisha Katiba Mpya ya Tanzania na kuwa kwake Rais kulitarajiwa na wengi kuwa kungeleta msukumo mpya katika jambo hilo.
Mmoja wa mawaziri katika serikali ya Rais Samia aliyezungumza nami kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema uwezekano wa kujiingiza katika suala la Katiba Mpya kwa sasa ni mdogo kutokana na mazingira ya Rais mpya.
“Rais Samia aliingia madarakani bila kutarajia. Kazi yake kubwa ya kwanza ni kuhakikisha CCM inashinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025. Mchakato wa kuunda Katiba Mpya utaigawa CCM na jamii kwa ujumla na kwa sababu si jambo la kusaidia kushinda uchaguzi. Anaweza kuamua kutekeleza hili katika awamu yake ya pili ya uongozi.”
Kikwete alianza mchakato huu kwenye awamu yake ya pili. Mzee Mwinyi alikubali vyama vingi katika awamu yake ya pili ya uongozi na hata Mzee Mkapa alifanya ubinafsishaji kwa nguvu zaidi katika awamu yake ya pili.
“Kama Samia atataka hiba (legacy) yake iwe Katiba Mpya, atafanya hilo katika awamu yake ya pili. Sasa hivi anahitaji kusimika mamlaka yake kama Rais, Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu. Kushinda uchaguzi, kuna mambo madogo ya kufanya kufurahisha wananchi na tayari ameanza kuyafanya,” alisema waziri huyo.
Ni jambo hilo la kusimika urais wake na kutafuta ushindi kwa CCM katika uchaguzi mkuu ujao, ndiyo pia utamfanya Rais Samia kutohangaika kubadili sheria na kanuni ambazo zimekuwa zikikisaidia chama chake kushinda katika chaguzi zilizopita.
Fungate hii itaendelea?
Hadharani, Rais Samia amezungumza kwamba katika serikali yake, hatasita kuteua mtu kutoka vyama vya upinzani kwa sababu yeye ataangalia kwanza maslahi ya nchi kabla ya vyama vya siasa au tofauti nyingine.
Katika teuzi ambazo tayari amefanya, Samia ameshawateua watu kutoka upinzani katika nafasi mbalimbali lakini pia kuwapa fursa watu waliokuwa mwiba kwa CCM katika miaka ya nyuma kabla ya kuhamia chama tawala wakati wa utawala wa Magufuli.
Na ingawa viongozi kama Zitto, Mbowe na Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, wamempongeza kwa baadhi ya hatua ambazo amechukua katika kutanua uhuru wa kisiasa, bado kuna masuala ambayo yanaweza kuharibu hali hii ya ‘fungate’ na utawala wa Samia inayoendelea sasa. Kwa mfano, kuna suala la namna serikali yake itakavyoendelea kushughulika na suala la wabunge 19 wa Viti Maalum kutoka Chadema ambao ingawa chama chao kimewakana, Bunge la Tanzania linaendelea kuwa nao kama wabunge halali.
Kuna pia suala lingine la namna Rais Samia atakavyoruhusu vyama vya siasa kufanya shughuli zao kwa namna ileile ambayo vyama vinataka. Kama uwiano hautakuwa sawa, serikali yake inaweza kuchukua hatua nzito kukabiliana na hilo na huo unaweza kuwa mwanzo wa uhusiano tofauti baina ya pande hizo mbili.
Kwa mujibu wa mmoja wa wandani wa Ikulu ya Tanzania, kuendelea au kumalizika kwa fungate hiyo kutategemea pia namna vyama vya upinzani vitakavyokuwa vikipokea “mkono wa heri” wa Rais Samia wakati wa utawala wake. Kwamba “Kama yeye atakuwa anatoa mkono wa heri na wapinzani wanamkingia ngumi kila uchao, anaweza kubadilika naye kukunja ngumi pia”.
Jambo moja la wazi ni kwamba fungate hii inayoendelea sasa itakuja kumalizika ndani ya muda mfupi au mrefu kutoka sasa. Swali pekee lisilo na jibu ni kwa namna gani fungate hiyo itamalizika.
Kwa sasa, siku 100 za Rais Samia madarakani zinatoa picha kwamba hatakwenda katika njia aliyopita mtangulizi wake. Anaweza kuwa zaidi ya Kikwete kwa kuachia uhuru wa kujieleza au kuzidi.