Monday, November 25

Tanzania yathibitisha wimbi la tatu la Corona

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amethibitisha kwamba kuna viashiria vya wimbi la tatu la virusi vya Corona nchini humo.

Akizungumza leo jijini Dar es salaam katika mkutano wake na Maaskofu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania(TEC), Rais Samia amesema zipo ishara ndani ya nchi hiyo kwamba janga hilo lipo.

‘Kama tunavyojua duniani sasa hivi kuna wimbi la 3 la Corona, tumetoka kwenye wimbi la kwanza Tanzania tumeingia tumeingia, limekwenda limekwenda limepungua kidogo tumeingia wimbi la pili, tumekwenda na sasa wimbi la tatu’.

Rais Samia alisema ‘Ishara ndani ya nchi tayari zinaonekana, tayari tuna wagonjwa ambao wemeshaonekana kwenye wimbi hili la tatu’, alisema Rais Samia akirejea pia kukumbusha ziara yake katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam ‘kama mnakumbuka siku niltembelea Hospitali ya Mwanyamala, kuna wodi Daktari mfawidhi alikuwa anaingiza akanambia humu kuna wagonjwa wenye matatizo ya kupumua, nikamwambia embu kuwa muwazi, nikamwambia Covid? akanambia eeh Covid, wakati wapiga picha walikuwa wameshatangulia, nikawaambie nyie tuokeni haraka’.

Pamoja na kueleza uwepo wa wimbi hilo la tatu, Rais Samia alitaka kuchukuliwa kwa tahadhari dhidi ya wimbo hilo la tatu la maambukizi ya virusi hivyo vya corona.

  • Unaweza pia kusikiliza:

Video content

Video caption: Corona: Madaktari wasema ripoti kuisaidia Tanzania kukabiliana na maradhi

‘Kwa hiyo ni kusema kwamba hili jambo bado lipo, tusijiache bado lipo, tuchukue tahadhari zote, na tunawaomba sana vio wa dini,mlisema hili kwa sauti kubwa kwa waumini wetu ili tujiepushe na vile vifo vya makundi’, alisema Rais Samia.

Kwa upande wao mbali na kumpongeza Rais Samia katika jitihada zake za kupambana ugonjwa huo na kuleta maendeleo, Rais wa Baraza hilo la Maaskofula Kanisa Katoliki, Gervas Nyaisonga alitaka kuboreshw akwa sera mbalimbali ili kusaidia utoaji wa huduma mbalimbali zikiwemo za afya na elimu.

Kwa zaidi ya mwaka sasa, Tanzania haijatoa takwimu zozote za wagonjwa wala vifo vitokanavyo na maambukizi ya virusi vya Corona, huku Rais aliyepita, John Magufuli alieleza kukamilizika kwa virusi hivyo nchini humo kutokana na njia mbalimbali zilizotumika ikiwemo kufanya Maombi.

Tangu aingie madarakani mwezi Machi mwaka huu kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Magufuli, Rais Samia, amekuwa mstari wa mbele kushughulikia suala hilo, ikiwemo kuunda kamati maalumu ya kuthamini ugonjwa huo.

Mpaka April mwaka 2020, taarifa rasmi ilionyesha Tanzania ilikuwa na wagonjwa 509 wa corona, vifo 21 na waliopona 183.