Christian Eriksen alipata mshtuko wa moyo alipoanguka uwanjani akiwa anachezea nchi yake ya Denmark dhidi ya Finland katika mechi za kuwania kombe la Euro 2020, alisema daktari wa timu yake Morten Boesen.
Awali, maafisa walisema kuwa hali ya afya ya kiungo huyo wa kati iliimarika akiwa hospitalini na hata kutuma salamu kwa wachezaji wa timu yake.
Eriksen alianguka muda mfupi kabla ya wachezaji kwenda mapumzikoni katika mechi ya ufunguzi kuwania kombe la Euro 2020 kati ya Denmark dhidi ya Finland Jumamosi.
“Alikuwa amepoteza fahamu kabisa. Tukampatia huduma ya kwanza ya kuhuisha moyo na mapafu (CPR) ili moyo uanze tena kufanya kazi, alikuwa amepata mshtuko wa moyo,” Boesen alisema.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
“Tulikuwa karibu vipi kumpoteza? Siwezi kusema, lakini tulifanikiwa baada ya jaribio la kwanza la kutumia kifaa cha kumfanya aanze tena kupumua, kwahiyo, tuliwahi haraka.
“Hadi kufia sasa, vipimo vilivyofanywa vinaonesha kuwa yuko sawa. Hatuwezi kuelezea kilichochangia kutokea kwa tukio hilo.”
Mchezaji huyo, 29, wa Inter Milan alipewa matibabu ya dharura akiwa uwanjani kabla ya kupelekwa hospitalini.
“Hali yake imeimarika na bado yuko hospitali kwa matibabu zaidi,” taarifa kutoka kwa maafisa wa Denmark ilisema Jumapili asubuhi.
“Asubuhi hii tumezungumza na Christian, ambaye ametuma salamu kwa wachezaji wenzake.
“Timu nzima na wafanyakazi wa timu hiyo ya taifa wamepokea usaidizi wa dharura na wataendelea kuupokea baada ya kutokea kwa tukio hilo.
“Pia tungependa kumshukuru kila mmoja kwa salamu za kumtakia afueni ya haraka.”
Kocha mkuu Kasper Hjulmand alisema kuwa Eriksen alimwambia, hakumbuki kilichotokea katika tukio la yeye kuanguka na kupoteza fahamu, Jumamosi.
Alimnukuu kiungo huyo wa kati akisema: “Nafikiri unahisi vibaya kuniliko mimi. Nahisi kana kwamba niko tayari kwenda kufanya mazoezi sasa hivi.”
Boesen alisema kuwa Eriksen alikuwa amepoteza fahamu wakati yeye anafika uwanjani.
“Nilipomfikia alikuwa amelala upande mmoja, alikuwa anapumua niliweza kuhisi mapigo yake lakini ghafla mambo yakabadilika na tukaanza kumpatia huduma ya kuwezesha moyo kuanza tena kufanya kazi (CPR),” alisema.
“Alipata usaidizi wa haraka sana kutoka kwa timu ya madaktari, wachezaji wenzake na wafanyakazi, na kwa kushirikiana kwa pamoja tukafanya tulichohitajika kufanya na kufanikiwa kuhakikisha Christian ameanza tena kupumua.”
Tukio hilo liliwapa wachezaji wenzake mfadhaiko wa akili huku mashabiki pia wakionekana kushtuka wakati mchezaji huyo anapata matibabu uwanjani.
Lakini je ni kina nani wengine waliowahi kupoteza fahamu uwanjani?

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Fabrice Muamba
Kiungo huyo wa kati wa Bolton Wanderers alipoteza fahamu uwanjani wakati wa mechi ya kuwania kombe la FA mwaka 2012 kwasababu ya kupata mshtuko wa moyo na alikuwa kabisa ni kama amefariki dunia” kwa dakika 78 kabla ya kusaidiwa kuanza tena kupumua. Kiungo huyo wa kati aliyekuwa timu ya England ya under-21 alilazimika kustaafu kucheza soka akiwa na umri wa miaka 24.
Bafetimbi Gomis
Mshambuliaji huyo wa Ufaransa amepoteza fahamu mara kadhaa uwanjani kwasababu za kimatibabu. Amewahi kupoteza fahamua akiwa anacheza na Swansea City, Galatasaray na Al-Hilal.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Marc-Vivien Foe
Huyu ni kiungo wa kati ya Cameroon aliyepoteza fahamu wakati wa mechi ya kombe la shirikisho mwaka 2003. Wahudumu wa afya walijitahidi kuufanya moyo wa mchezaji huyo, 28, kuanza tena kufanya kazi akiwa uwanjani kabla ya kumtoa nje kwa kutumia machela.
Hata hivyo, juhudi zao hazikufua dafu na baadaye akatangazwa kuwa amefariki dunia.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Maelezo ya picha,Jose Antonio Reyes, kushoto na Antonio Puerta, kulia wote walianza taaluma zao katika klabu ya Sevilla
Antonio Puerta
Kiungo huyo wa kati wa timu ya Sevilla alifariki dunia akiwa anafanya mazoezi ya viungo katika mchezo wa kwanza ya Ligi ya La Liga msimu wa mwaka 2007-08 dhidi ya Getafe na ingawa alifanikiwa kuamka na kutoka uwanjani baada ya kusaidiwa na wahudumu wa afya, alianguka tena akiwa chumba cha kubadilisha nguo.
Puerta, mchezaji wa kimataifa wa Uhispania alikimbizwa hospitalini ambako alifariki dunia siku tatu baadaye kwasababu “viungo vyake vingi vilishindwa kufanya kazi” kutokana na mshtuko wa moyo wakati huo akiwa na umri wa miaka umri wa miaka 22.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Cheick Tiote
Miezi minne baadaye baada ya kuondoka Newcastle United, kiungo huyu wa kati alipoteza fahamu wakati anafanya mazoezi na klabu ya China ya Beijing Enterprises. Mchezaji huyo wa Ivory Coast, 30, alifariki dunia akiwa hospitani.

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Miklos Feher
Na Mshambuliaji huyu wa Hungary alikuwa akichezea Benfica ya Ureno dhidi ya Vitoria Guimaraes Januari 2004 alipopiga magoti kwa uchungu kabla ya kuanguka kwa nyuma baada ya kupata mshutuko wa moyo.
Wahudumu wa afya walijitahidi kufanya moyo wake uanze tena kufanyakazi kabla ya kutolewa nje ya uwanja na kukimbizwa hospitali.
Madaktari pia nao walijitahidi kadiri ya uwezo wao kumuwezesha kuanza tena kupumua kwa dakika 90 kabla ya kutangazwa kuwa amefariki dunia.