KHADIJA KOMBO-PEMBA.
Mkuu kitengo shirikishi Kifua kikuu, ukimwi, Ukoma na homa ya ini Pemba Khamis Hamad Ali amesema kitengo kinaamini kwamba ugonjwa wa kifua kikuu bado upo ndani ya jamii hivyo ni lazima wagonjwa waibuliwe ili kupatiwa tiba na kutokomeza kabisa ugonjwa huo.
Mkuu huyo ameyasema hayo huko katika ukumbi wa ofisi za kitengo shirikishi Machomanne Chake Chake katika kikao cha uwasilishaji wa ripoti za utekelezaji kwa kipindi cha mwezi April-June 2021 kwa Asasi za kirai ambazo zinashirikiana na kitengo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu.
Amesema kwa mujibu wa Global fund kupitia WHO wanatakiwa kuibua wagonjwa 1612 kwa mwaka ili kupunguza au kuondoa kabisa ugonjwa huo.
Kwa upande wake Dk Khamis Abubakar amabae ni mratibu wa kifua kikuu na ukimwi Zanzibar amesema NGOs zinategemewa sana katika mapambano ya kifua kikuu kwani wao wana uwezo mkubwa wa kuifikia jamii katika kuijenga uwelewa na kuibua wagonjwa wengi zaidi.
Wakiwakilisha ripoti zao wanajumuiya hao wamesema changamoto kubwa iliyopo ndani ya jamii ni kwamba bado hawajawa na utayari wa kutoa makohozi kwa ajili ya kufanyiwa vipimo hivyo elimu zaidi inahitajika ili kujenga uwelewa zaidi.
NGOs ambazo zinashirikiana na kitengo shirikishi katika mapambano ya kifua kikuu ni pamoja na PPC, JUKAMKUM, MKUPE, ZYF na ZAPHA +