Sunday, March 16

Licha ya serikali kuanzisha mahakama maalum ya kushughilikia kesi za udhalilishaji Zanzibar bado kunahitajika nguvu na maboresho zaidi kwenye mahakama.

MKURUGENZI wa Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania-Zanzibar Dr.Mzuri Issa, akitoa maelezo mafupi katika mkutano wa kushirikishana kuhusu hatua za utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa kupambana na udhalilishaji Zanzibar 2017/2022 uliofanyika katika ofisi za Tamwa Mkanjuni Pemba
PICHA NO:2. MRATIBU wa TAMWA Zanzibar upande wa Pemba Fat-hiya Mussa Said, akiwasilisha ripoti ya utafiti mdogo wa muonekano na Utendaji wa Mahakama maalumu ya kushughulikia udhalilishaji, kwa wadau kutoka taasisi mbali mbali zinazoshuhulika na masuala ya udhalilishaji Pemba, mkutano Uliofanyika katika ofisi za chama hicho Mkanjuni Pemba.
MKUU wa Idara ya jinsia na watoto Pemba Mwanaisha Ali Massoud, akifungua mkutano wa siku moja kwa niaba ya Afisa Mdhamini Wizara ya afya ustawi wa jamii wazee jinsia na watoto, mkutano uliofanyika katika ofisi za TAMWA Pemba
WADAU kutoka taasisi mbali mbali zinazoshuhulika na masuala ya udhalilishaji wa wanawake na watoto Pemba, wakifuatilia kwa makini uwasilishaji wa ripoti mbali mbali za uzalilishaji, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania/Zanzibar kwa upande wa Pemba.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

NA ABDI SULEIMAN.


WADAU wa kupamabana na vitendo vya udhalilishaji kisiwani Pemba, wamesema licha ya serikali kuanzisha mahakama maalum ya kushughilikia kesi za udhalilishaji Zanzibar lakini bado kunahitajika nguvu na maboresho zaidi kwenye mahakama hiyo ili iweze kufanya kazi kwa ufanisi na kufanikisha lengo la uanzishwaji wake.

Waliyaeleza hayo katika mkutano wa kuwashirikisha wadau kuhusu hatua za utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa kupambana na udhalilishaji ulioambatana na uwasilishaji wa ripoti ya utafiti mdogo wa muonekano na utendaji wa mahakama maalum ya kushughilikia kesi za udhalilishaji Zanzibar uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA Zanzibar.

Said Rashid Hassan kutoka kituo cha huduma za sheria Zanzibar alisema ili kuondosha usumbufu wa kukosekana kwa mashahidi muhimu, mahakama hiyo iweke mfumo ambao utawezesha wataalam wote wanaohitajika katika uendeshaji wa kesi hizo kuwepo mahakamani wakati wote.

“Tutengeneze mahakama ambayo itakuwa inajumuisha wataalam wote wanaohitajika katika uendeshaji wa kesi za udhalilishaji kama vile madaktari na Polisi ili kuepuka hili tatizo la ucheleweshaji wa ushahidi kwa kisingizio cha kukosa ushahidi muhimu ambao unapelekea kesi hizi kuchelewa kutolewa hukumu,” alisema.

Kwa upande wake ACP Fakih Yussuf alisema ili mahakama hizo ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kunahitajia kuwepo mfumo maalum unaowapa fursa maafisa dawati wanaosimamia matukio hayo ili kuwawezesha kuzifuatilia kwa wakati kesi hizo.

“Shughuli za dawati zinaumuhimu wake, zinahitajika kupewa kipaombele maalumu kulingana na umuhimu wake na maafisa wanaoshughulikia na dawati waachwe wafanye kazi hii tu”alisema.

Alisema wakati umefika kwa kitengo cha dawati kupatiwa nyenzo za kuweza kuwafikisha kutekeleza majukumu yao kikamilifu, ili kuondosha msongomano na uzito uliopo kwa sasa.

Aidha aliwataka watendaji wenzake kuongeza nguvu katika masuala ya udhalilishaji, ili isiewe kwa kipindi kifupi na badala yake iwe kwa kipindi kirefu.

Mwakilishi kutoka kituo cha huduma za sheria Zanzibar tawi la Pemba Said Rashid Hassan, alizitaka taasisi zinazohusika kuhakikisha zinawachukulia hatua za kisheria, baadi ya watendaji wao wanaozichezea kesi hizo kwa makusudi.

“Wapo baadhi ya watendaji wanashiriki kwa kiasi kikubwa kuziharibu kesi hizo, vizuri watendaji hawa kushuhulikiwa nao kwani msururu ni mkubwa wa mpaka mtu kutiwa hatiani”alisema.

Afisa Jinsia Wilaya ya Micheweni Bizume Haji Zume, alisema jambo la kusikitisha ni kukosekana kwa nhyumba salama kwa wahanga wanaofanyiwa vitendo vya udhalilishaji, kuweza kukaa pamoja na kunguza kutiwa maneno na familia zao.

Mapema mratibu wa TAMWA Zanzibar, Fat-hiya Mussa Said alisema utafiti huo umejikita katika kutathimini hatua za utekelezaji wa maagizo ya serikali juu ya uanzishwaji wa mahakama hiyo kwa lengo la kukabiliana na vitendo hivyo katika jamii.

“Malengo ya utafiti huu ilikuwa ni kutaka kuona hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa agizo la rais katika kuanzisha mahakama maalum ya kushughilikia kesi za udhalilishaji Zanzibar,”alisema.

Alisema “ripoti imebainisha kwamba jumla ya matukio 278 yaliripotiwa kwenye vituo vya Polisi Unguja na Pemba kuanzia Januari hadi machi ambapo kati ya hayo matukio 203 ni ubakaji, ulawiti 69 na 6 kumuingilia kinyume na maumbile na kati matukio hayo 244 bado yanaendelea na upelelezi huku 44 pekee yakiwa yanaendelea mahakamani.”

Kwa upande wake mkurugenzi wa, TAMWA Zanzibar Dkt. Mzuri Issa aliwataka wadau wa kupamabana na vitendo hivyo kuendelea kuungana pamoja katika ufuatiliaji wa matukio hayo ili kuhakikisha watoto na wanawake wanabaki salama katika jamii.

Alisema utafiti huo utasaidia kutoa mwelekeo wa jinsi ya kukabiliana na matukio hayo ikiwa ni pamoja na kuisadia serikali kufikia malengo ya utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto Zanzibar.

“Mwelekeo wa kidunia kwasasa ni kuhakikisha kwamba hakuna hata mmoja anayeachwa nyuma katika upatikanaji wa haki, hivyo ili hili liweze kufikiwa ni lazima kila mmoja kwa nafasi yake kuwajibika ipasavyo,” alisema Mkurugenzi huyo.

Mkutano huo wa kuwashirikisha wadau kuhusu hatua za utekelezaji wa mpango wa kitaifa wa miaka mitano wa kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na watoto Zanzibar 2017-2022 umewashirikisha wadau kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Wizara ya Afya, ustawi wa jamii, wazee jinsia na watoto, mawakili, pamoja na wajumbe wa mitandao ya kupinga udhalilishaji Pemba.