NA KHAMISUU ABDALLAH
WATOTO ni hazina katika taifa lolote lile duniani ambalo linategemewa katika kuchangia maendeleo ya nchi zao kupitia sekta mbalimbali na hata kijamii.
Mtoto ni mtu yeyote mwenye umri wa chini ya miaka 18 ambapo tafsiri hii imetokana na Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, Mkataba wa Afrika kuhusu Haki na Ustawi wa Mtoto, Sera ya Maendeleo ya Mtoto na sheria ya mtoto namba 21 ya 2009.
Katika umri huu mtoto anahitaji malezi bora ili aweze kuishi vizuri, kushirikishwa, kulindwa na kuendelezwa kiakili kwa ajili ya maisha yake ya baadae ya utu uzima.
Watoto pia wana haki za kipekee kwa sababu umri wao mdogo na hali ya utegemezi vinaweza kuwafanya wadhulumiwe na kutendewa vitendo vibaya.
Watoto wote wana haki sawa bila kujali jinsia, rangi, kabila, dini, hadhi au hali ya afya.
Umoja wa mataifa, serikali, wazazi/walezi na jamii kwa ujumla wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanapatiwa haki zao ikiwemo haki ya Kuishi, inayphusu kulinda na kuendeleza uhai wa mtoto ikiwemo kuzuia magonjwa na kupata huduma za matibabu.
Licha ya mambo yote hayo kuwa watoto wanategemewa katika mihimili hiyo lakini pia wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na matukio ya ajali ikiwemo kuungua moto kutokana na wazazi kutokuwa makini katika malezi yao.
Hali hiyo inawafaya baadhi yao kupata ulemavu wa kudumu jambo ambali limekuwa likiisababishia serikali kubeba mzingo kwa kiasi fulani ikiwemo kuwahudumia watoto hao.
Inasikitisha kuona pale wazazi wanapokuwa hawapo makini katika malezi ya watoto wao hasa wale wenye miezi sita hadi mwaka mmoja wengi wao wakiwa wanawake ambao kwa kiasi kikubwa ndio wanaoathirika zaidi na majanga ya moto.
Mwandishi wa makala haya alifika katika hospitali kuu ya Mnazimmoja katika wodi ya watoto walioungua moto na kuwakuta watoto wakiwa na majeraha mbalimbali yaliyosababishwa na moto ikiwemo mafuta, uji na maji ya moto.
Wengi wa watoto hao kwa kiasi kikubwa wameathirika katika kichwa, miguu, mikono, tumboni na mgongo kutokana na majeraha hayo.
Akizungumza na mwandishi wa makala haya Daktari Dhamana Wodi ya Watoto wenye matatizo ya upasuaji ajali na wanaoungua moto, Hospitali kuu ya Mnazimmoja, Hidaya Salum Jabir, alisema watoto wengi wanaoungua moto katika miaka hiyo inatokana na wazazi wao kutokuwa makini na malezi.
Daktari Hidaya, anasema wengi wa watoto hao wameungua kutokana na vitu vimoto ikiwemo maharage, chai na maji ya moto lakini hadi sasa hawajapokea kesi inayohusiana na mafuta ya moto.
Anabainisha kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kesi za watoto kuungua moto zimekuwa zikiongezeka hasa kwa watoto wenye umri huo kwani katika wodi hiyo imekuwa ikipokea watoto saba mpaka 10 ambao wameungua moto.
Aidha anasema kutokana na hali hiyo wameamua kuweka utaratibu kwa wazazi kuhakikisha mtoto anapoungua moto basi kufika vituo vya polisi kwa ajili ya kupatiwa PF3 ili waweze kupatiwa matibabu watoto wao.
“Tunaona hii itatusaidia katika kuona wazazi na walezi wanawalinda watoto wao na majanga ya moto,” anabainisha.
Hivyo, anawaomba wazazi kuendelea kuelimishana juu ya kuwalinda watoto wao na majanga ya moto ambayo yanaweza kuwapelekea kupata madhara mbalimbali ikiwemo ulemavu wa kudumu.
“Ni vyema wazazi kuwa makini wanapokuwa katika shughuli zao za mapishi jikoni na kuwa wangalifu zaidi kuwatizama watoto wao na kuacha tabia ya kuwaacha na watoto wenzao jikoni” alisema.
Sambamba na hayo, asliwasisitiza wazazi na walezi kuweka mbali vitu vya hatari ikiwemo chupa za chai makarai ya mafuta na vitu vyengine ambavyo vinaweza kuwaathiri watoto wao.
Katika hatua nyengine, anawaomba wazazi wanapotaka kuwakosha watoto wao, kuzimua maji kabla ya kuyaweka yakiwa yamoto ili kuwaepusha watoto wao kuungua.
“Inakuaje maji ya moto unayaweka bila ya kuyazimua na unamjua mtoto vitu vya hatari ndivyo anavyopenda kuchezea hivyo wawe makini kwa watoto wao” alisisitiza.
TAKWIMU ZA WATOTO WALIOUNGUA MOTO MWAKA 2018/2020
Aidha kwa mujibu wa takwimu za hospitali kuu ya Mnazimmoja zinaeleza kuwa mwaka 2018 jumla ya watoto 132 waliungua moto.
Aidha zilieleza kuwa mwaka 2019 watoto 72 na mwaka 2020 jumla ya watoto 50 walipokelewa wakiwa wameungua moto wengi wao wakiwa wakike kati ya umri wa miezi sita hadi miaka mitatu.
WAZAZI WA WATOTO WALIOUNGUA MOTO
Fatma Khamis ni mzazi wa mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minne, anasema mtoto wake alikwenda kununua kabaisa kwa jirani yake ndipo alilipatwa na majanga hayo kuangukia katika karai la moto na kupata majeraha kuanzia mkono upande wa kushoto ubavu na mguu.
Aidha anasema alimpeleka hospitali ya Kibweni na kupata matibabu lakini kidonda chake kilikuwa hakiridhishi na kuamua kumpelekea hospitali ya Mnazimmoja.
Anasema alikuwa hatambui kuwa Mnazimmoja ni lazima upate karatasi ya polisi PF3.
“Wakati nishafika mnazimmoja mume wangu aliniletea karatasi na naskuru mtoto waungu alipata matibabu na sasa anaendelea vizuri,” anabainisha.
Akizungumzia suala la ulizi wa mtoto anasema wazazi wanajitahidi katika suala hilo lakini majanga mengi yanawakuta kwa majirani.
Nae Mtumwa Bakar Omar ambae ni mama wa watoto wawili walioungua moto kutokana na uji mmoja akiwa na majeraha kuanzia kichwani hadi tumboni ambae ni mtoto mwenye umri wa miezi 10 na mmoja akiwa na majeraha mguuni walioungua na uji anasema ni nimitihani tu iliyowapata watoto wake.
Anasema wanajitahidi katika suala la kuwalinda watoto lakini mara nyegine inakuwa bahati mbaya.
“Nilikuwa nampikia uji nishamaliza nishauepua kaka yake alimchukua na kumbeba ndipo walipoanguka katika sufuria na kuungua,” anabainisha.
Faizat Twahir ni mtoto mwenye umri wa miezi tisa ambae ameungua na chai kuanzia makalio hadi mguu wa kushoto anasema alipatwa na majeraha hayo baada ya kuweka chupa aliivuta na kumuangukia.
Hivyo wanatumia fursa hiyo kuwaomba wazazi wenzao kuwa makini katika kuwalinda watoto wao hasa pale wanapotoka nje ya nyumba.
MWISHO