Tuesday, November 26

Zainab:Mwanamke wa kwanza kuwa injinia wa meli

NA KHAMISUU ABDALLAH

UKIWA na malengo yako mara nyingi wanaumme wamekuwa wakikukatisha tamaa lakini mimi sikuvunjika moyo wapo walionambia niache kazi hii wanioe ili niwe mama wa nyumbani.

Hayo ni maneno ya Zainab Ali Abrahmn Rashid ambae ni Injinia pekee mwanamke kwa Zanzibar ambae anafanya kazi katika Meli ya Mt. Ukombozi II.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya anasema alianza kazi ya ubaharia mwaka 2018 mpaka sasa ambapo lengo lake ni kufikia malengo ya kuisadia nchi yake kupitia sekta ya bahari.

Aidha anasema kilichompelekea kuingia katika kazi hiyo ni mapenzi ndani ya nafsi yake kwani yeye mwenyewe binafsi alikuwa anaipenda kazi hiyo na sasa ameweza kuitendea haki.

Anasema bado hajafikia malengo yake aliyojiwekea ikiwa ni kufikia Chief kamili huku akiwa bado anaendelea na masomo yake na kujifunza katika meli mbalimbali.

Zainab anabainisha kuwa kazi yake hiyo imempa mafanikio kadhaa ikiwemo kujuana na watu wengi na hata viongozi kwa upande wa Tanzania bara.

Anazungumzia changamoto anazokabiliana nazo katika kazi yake kuwa anapotaka kufungua kitu kwenye mashine ni lazima apate msaidizi kwani nguvu za mwanamke ni ndogo ukilinganisha na mwanamme.

Changamoto nyengine anabainisha kuwa alipokuwa akifanya kazi katika meli za abiria akiwa Ofisa msaidizi ya Mv. Kepten One pale alipokuwa akifanya kazi kwenye mto na bahari Rufiji ni pale maji yalipotoka ya mto na kuanza kuvuta meli ili kunusuru roho za abiria na mali zao.

“Inatubidi tufanye hivyo kwani tumeshapakia roho za watu jitihada zetu zinahitajika ili kuona abiria na mizigo yao wanafika salama kwani maji ya mto yakitoka ni lazima meli tuivute,” anabainisha.

Zainab akizungumzia kitu ambacho hatokisau maishani mwake kilichomtokezea katika kazi yake anasema ni pale mara ya kwanza anaingia baharini akiwa katika Meli ya Sea Star akielekea kisiwani Pemba mawimbi yalikuwa makali alianza kulia na kukata tamaa kuwa haitaki tena kazi ya Ubaharia.

“Tuliporudi tu kisiwani Pemba nilishuka na kurudi nyumbani, wazazi wangu walinambia utarudi huko huko kwani hiyo ndio kazi yako ulioichagua, umeamua kusoma na nilirudi kwani nilivunjika moyo katika kipindi kile lakini hivi sasa nimeshaizoea,” anasema.

Akizungumzia mabaharia wanaumme kumuunga mkono katika kazi yake anasema kwake yeye ni kubwa kwani asilimia kubwa anaofanya nao kazi ni wanaumme akiwa mwanamke peke yake.

“Mabaharia wanakitu umoja na wanasomo lao hasa wanasoma wanatakiwa kuwa na umoja, ushirikiano, udugu na wanaishi kwa kutegemeana sio kama kazi utaachiwa bali tunaishi kwa upendo wa hali ya juu kwa hili najivunia kwa wenzangu ninapokuwepo kazini,” alibainisha.

Hata hivyo, anasema ameshawahi kufanya jambo la kihistoria katika jamii na haitaweza kumsahau pale alipomzalisha mama kwenye meli bila ya kuwa daktari wakati anahitaji msaada wa kujifungua kipindi hicho wakati yupo kwa muda katika meli ya Seling One ya Bakhresa.

“Dokta alikuwa hayupo na mama alikuwa anataka kujifungua basi nilipata ujasiri na nikatoa msaada mkubwa sana na amiini yule mama mpaka leo anakumbuka hili,” anasema.

Akizungumzia kugoma kwa mabaharia anasema nae ameshawahi kukutana nayo katika meli ya Mv. Sipit One kati ya boss wa meli na wafanyakazi wake lilitokana na kutokuwalipa posho zao kitendo ambacho kiliwafanya wafanyakazi wote kugoma lakini mwisho mambo yalikaa sawa.

Zainab anabainisha kuwa vyombo alivyofanyia kazi Tanzania ni Sea Star ya Wete, Mv. Sipit One ambayo ipo Mafia Nyamisati na sasa yupo katika Meli ya mafuta ya Ukombozi II ambayo ni ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar lakini kwa nje ya Tanzania bado hajafikia.

“Katika kazi yangu nimeshawahi kukutana na viongozi mbalimbali ikiwemo Katibu tawala Mkoa wa Pwani na wasaidiazi wake lakini kwa Zanzinbar bado, Katibu Tawala Mkoa wa Pwani alivutiwa sana na kazi yangu na alifikia mpaka kunilipia Chuo na pesa ya matumizi kutokana na mimi ni mwanamke kupenda fani hii,” anasema.

Akizungumzia wanawake wengi kutovunjika moyo kuingia katika kazi kama hiyo anasema mara nyingi wanawake wanakuwa woga kwenye kufanya chochote ambacho kina hatari katika maisha yao.

Hivyo, anawatoa hofu na kuwataka kujiunga katika sekta hiyo kwani sekta ya bahari inakufanya wewe mwenyewe kuwa na nguvu kujiamini na kupata chochote hafla unaweza kukitatua kwani bahari inakufanya uishi maisha yako mwenyewe.

Anasema sekta ya bahari pia inamlea mtu vizuri kidini, kimila, kitamaduni, kiupendo kwani sekta ya bahari inakufanya uwe na upendo zaidi na jamii kwani unakuwa mtu wa huruma na upendo kwa jamii inayokuzunguka.

“Yupo mwanamke mwengine nae amekuja na kuingia katika fani hii kama miezi mitatu sasa ambae ni mzanzibari pia,” alibainisha.

Anasema jamii inachukulia kazi ya ubaharia ni kitu cha kihuni sana na ndio maana hivi sasa wanamuziki waingizaji kila kitu wanachoigiza na kuimba ni mabaharia inatuuma sana kwani hawajui undani wa ubaharia upoje wanatuvunjia heshima kwa kweli.

Anasema zamani kazi ya ubaharia ilikuwa watu waingia tu bila ya kusoma lakini hivi sasa mtu unasomea unapoteza gharama nyingi alafu mtu anakufanyia masihara kwa kweli tunachukia kudhauriwa kazi yetu.

Anasema wakati anaingia katika kazi hiyo wanawake wenzake walifurahi lakini kundi kubwa la wanaumme lilikuwa likimvunja moyo na kumrudisha nyuma kufikia malengo yake.

“Walikuwa wakinambia wewe hujaona kazi nyengine mpaka kazi hii kwani huwezi kukaa nyumbani ukalea tu watoto na wengine wamefika kunambia wanioe ili niwe mama wa nyumbani,” anasema.

Anasema hivi sasa wanawake wamepata muamko kuingia katika sekta hiyo kwani wapo Makepteni, Navigation na Mainjinia wanawake hata katika ndege.

Akizungumzia serikali kuleta dhana ya uchumi wa bluu hasa katika sekta ya bahari alipongeza serikali kwa kutambua uchumi wa bahari na kuwashauri vijana wa kike na wakiume ambao wanahitajika katika sekta hiyo kujitoa na kuzidi kuipenda sekta ya bahari ili waweze kusaidia serikali ya mapinduzi Zanzibar katika maendeleo ya nchi yao.

Anasema kwa sasa hajaanza kulipwa mshahara kamili kwani anaendelea na masomo huku akiwa anajitolea lakini inawauma kwani wanafanya kazi ngumu hivyo serikali iwafikirie juu ya jambo hilo.

“Nimeshasoma, najitolea halafu unataka kuongeza cheo hulipwi hasa sisi wanawake ambao maisha yetu yanakuwa magumu,” anasema.

Anabainisha kwamba ifahamike kuwa mazingira wanayofanyia kazi ni magumu sana kwani wanafanya kazi katika bahari na hakuna asietambua kuwa bahari ni mama wa mama.

Hivyo aliiomba serikali kuiagnalia sana sekta hiyo hasa katika dhaa ya uchumi wa bluu hasa kwa mabaria kwani watengenezaji uchumi wa buluu ni mabaharia.

“Watuangalie kwani tunarisk sana kwenye posho tunaomba msaada wao kama serikali yetu hasa sisi wanawake ambao sio wengi katika sekta hii, serikali itupe kipaumbele kwani tunajitoa kwa ajili ya kusaidia nchi yetu,” anaomba.

HISTORIA YA MAISHA YAKE

Zainab ni mtoto wa kwanza katika familia ya Ali Abrahaman na bibi Lulu Hassan Mohammed kati ya watoto wanne wanawake wawili na wanaumme wawili ambae ni mzaliwa wa Zanzibar katika kijiji cha Fuoni.

Ameanza elimu yake ya Maandalizi katika skuli ya Magomeni na baadae kujiunga na skuli ya Msingi katika skuli ya Fuoni na kumaliza kidato cha nne katika skuli ya Sekondari Fuoni mwaka 2010.

Baadae alijiunga na vijana katika kikosi cha kujenga uchumi (JKU) mwaka 2015 na alipotoka hapo alijiunga na tasisi ya Mama Shadya Karume ya ZAYADESA na kufanya kazi kwa muda wa miaka miwili.

Anasema baadae aliondoka na kwenda kusoma mapishi na Gardeni Chuo cha Mombasa na kufanya kazi ya mbunifu wa bustani ‘Garden Disainer’ na kuidizaini bustani ya iliyokuwepo Uwanja wa Ndege wa Kimaitafa wa Abeid Amani Karume wakati akiwa kwenye kampuni ya Sugar Satom.

Baadae aliona bado malengo yake hajatimia na kuingia katika sekta ya marine katika Chuo cha Dar esalam Marrine mwaka 2018 na kujifunza kwa vitendo katika meli ya Zan Fast Ferrise na kupata ajira yake ya mwanzo katika meli ya Mv. Sipit One na alipomaliza ajira yake alirudi Chuoni na sasa amepewa meli ya Mt. Ukombozi 11 ambayo ni kubwa.

Zainab ni mama wa watoto wawili akiwemo mwanammke na mwamme.