Sunday, March 16

CRC yawataka watumiaji wa Huduma za maji na Nishati kisiwani Pemba kupeleka matatizo yao mbali mbali yanayowakabili ili kuweza kupatiwa ufumbuzi.

 

NA ABDI SULEIMAN.

WATUMIAJI wa Huduma za maji na Nishati kisiwani Pemba, wameombwa kuliunga kulitumia Baraza la kuwawakilisha Mtumiaji wa huduma za Maji na Nishati Zanzibar (CRC), kwa kupeleka matatizo yao mbali mbali yanayowakabili ili kuweza kupatiwa ufumbuzi.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa baraza hilo Zanzibar Hadia Abdul-rahman Othman, wakati alipokua akiwasilisha mada juu ya kulijua baraza hilo, kwa madiwani wa Wilaya ya Michewenin hafla iliyofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni.

Alisema baraza hilo limekua likipokea matatizo mbali mbali kutoka kwa wananchi, juu ya masuala ya huduma za maji na nishati kwa lengo la kuzitatua ili watumiaji wa huduma hizo kuweza kunufaika nazo.

“Baraza lilishiriki moja kwa moja katika changamoto kubwa iliyokua ikiwakabili wananchi juu ya kilio cha gharama kubwa, juu ya kuingiwa huduma za umeme na sasa mafanikio yameonekana gharama zimekuwa chini”alisema.

Mkurugenzi huyo alisema baraza limeanzishwa chini ya kifungu namba 33 (1) cha sheria ya kuanzishwa kwa ZURA, sheria namba 7 ya 2013 ikiwa na lengo la kuwatete na kusimamia maslahi ya watumiaji wa huduma za maji, umeme, mafuta na gesi ya kupikia (LPG).

Hata hivyo alisema kuanzishwa kwa baraza hilo, linatokana na Takwa la kiulimwengu-Mkataba wa Umoja wa Mataifa (United Nation Charter) 1945, ambapo imetaka uwepo wa Mabaraza ya kulinda maslahi ya watumiaji.

“Kuanzishwa kwa Mamlaka za Udhibiti Duniani tangu mwaka 1948, kwa ajili ya kuwadhibiti watoa huduma mbali mbali kumepelekea kuanzishwa kwa Mabaraza ya watumiaji ili kulinda maslahi yao”alisema.

Aidha alisema hutuba ya Rais wa awamu ya 35 wa Marekani Bw.JOHN KENNEDY aliyoitoa 15/3/1962, ilihimiza juu ya uwepo wa mabaraza ya watumiaji, ambayo ilipelekea kuanzishwa kwa siku ya watumiaji duniani kila ifikapo tarehe hiyo.

Kwa upande wake afisa Elimu na uhamasishaji (CRC) Khamis Ame Mnubi, alisema kumekua na matumizi mabaya ya huduma za maji na umeme zinazofanywa na wananchi, hali inayopelekea baadhi yao kukosa kabisa huduma hizo na kuanza kutoa malalamiko.

“Kwamfano utamuona mtu anafua nguo mferejini maji yanatoka. Unadhani wenzako watakua wanapata huduma hiyo vizuri tukatumia kwa uandalifu hudma zetu ili kuondosha matatizo kwa wananchi kusema huduma haziwafiki au hawapati”alisema.

Hata hivyo aliitaka mamlaka ya maji Zanzibar ZAWA kurekebisha makakati wao wa huduma kwa wateja, ili wananchi waweze kufahamu mkakati wao, kwa Zanzibar mkakati wanao ZECO na baada ya kilio cha muda mrefu.

Mapema akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa baraza hilo Juma Bakar Alawi, alisema baraza hilo limeanzishwa maalumu kwa kuwapa fursa wananchi kutoka maoni yao katika masuala ya huduma za Maji na Nishati.

Kwa upande madiwani wameitaka CRC kuwahimiza makampuni yanayotoa huduma za nishati Zanzibar, kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kufahamu madhara ya huduma wanazotoa.

Walisema kumekuwepo na kapuni nyingi zinatoa huduma zao, ikiwemo utumiaji wa gesi lakini zimeshindwa kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya gesi hizo.