Sunday, November 24

Miaka 10 ya Uhuru wa Sudan Kusini: John Garang, ‘Baba wa taifa’ ambaye hakuonja matunda ya uhuru wa nchi

Sudan Kusini ilipata uhuru miaka 10 iliyopita baada ya zaidi ya miaka 20 ya mapigano.Vita hivyo vilianza mwaka wa 1983 wakati maasi yalipozuka kusini mwa Sudan hadi mwaka wa 2005 wakati mkataba wa amani ulipotiwa saini kumaliza vita na kuwapa watu wa kusini mwa Sudan uhuru wa kuamua hatima ya nchi yao.Katika msururu wa makala zetu ya maadhimisho ya miaka 10 ya uhuru wa nchi hiyo tunakupakualia kumbukumbu za harakati za kujitawala,matukio muhimu na watu mashuhuri waliohusika na harakati hizo.Katika sehemu hii ya kwanza tunamuangazia baba wa uhuru wa Sudan Kusini John Garang de Mabior.

Short presentational grey line

Imetimu miaka 16 tangu kifo cha John Garang de Mabior kilichotokea baada ya ajali ya helikopta. Kifo chake kilizua taharuki nchini Sudan na baada ya kuhudumu kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan kwa wiki tatu pekee, kundi la waasi wa SPLM lilikuwa limejikuta katika mtihani mkubwa sana.

Kiongozi aliyetarajiwa kuwapa mwongozo wa kukabiliana na changamoto za kisiasa katika siku zijazo alikuwa hayupo tena. Alitumia miaka mingi kupigana dhidi ya serikali ya Sudan -dhamira yake ikiwa kuleta usawa.

Garang awali hakutaka kugawanyika kwa Sudan na alitumai nchi mpya yenye kuheshimu haki za wote na wananchi kuishi kwa amani kwa kuheshimu tofauti za kila mmoja ingeweza kuwepo katika Sudan mpya. Hata hivyo mapambano yake na mkataba wa amani aliosaini mwaka wa 2005 na serikali ya Khartoum ulikuwa sehemu ya mkondo uliopelekea Sudan Kusini kupata uhuru wake .Uhuru ambao baba huyo wa taifa jipya hakuuona kwa macho kwani mauti yalimkumba miaka sita kabla ya taifa lake kujipatia uhuru .

Wengi hadi sasa hujiuliza, je hatima ya Sudan Kusini ingekuwa ipi iwapo Garang angekuwa hai?

John Garang:Mchumi, Mwanajeshi, Msomi na Kiongozi

John Garang de Mabior alizaliwa Juni 23, 1945 na aliaga dunia Julai 30 2005. Alikuwa mwanaisasa wa Sudan na kiongozi wa waasi wa Kusini mwa nchi yake .

Kuanzia 1983 hadi 2005, aliongoza Jeshi la Ukombozi la Wananchi wa Sudan -SPLA,wakati wa Vita vya Pili vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan, na kufuatia makubaliano ya amani alihudumu kwa muda mfupi kama Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan kwa wiki 3 hadi alipokufa katika ajali ya helikopta. Mchumi kitaaluma, Garang alikuwa na ushawishi mkubwa kwa harakati ambazo zilisababisha msingi wa Sudan Kusini kujipatia uhuru na kuwa nchi miaka sita baada ya kifo chake .

Garang, alizaliwa katika familia masikini kutoka kabila la Dinka katika kijiji cha Wangulei Kaunti ya Twic Mashariki katika mkoa Upper Nile nchini Sudan. Aliachwa yatima akiwa na umri wa miaka kumi, na jamaa zake ndio waliokuwa wakimlipia karo ya shule akisoma katika maeneo ya Wau na kisha Rumbek.

Freshly-minted notes of the new South Sudan pound pay homage to John Garang

CHANZO CHA PICHA,AFP

Maelezo ya picha,Sarafu ya Sudan Kusini inatumia picha ya Garang

Mnamo 1962 alijiunga na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kwanza vya Sudan, lakini kwa sababu alikuwa mchanga sana, viongozi wa harakati hizo walimhimiza yeye na wengine wa umri mdogo kutafuta elimu. Kwa sababu ya mapigano yaliyokuwa yakiendelea, Garang alilazimika kumalizia masomo yake ya sekondari nchini Tanzania. Baada ya kupata ufadhili aliendelea kupata digrii ya Shahada ya Sanaa katika Uchumi mnamo 1969 kutoka Chuo cha Grinnell huko Iowa, Marekani .

Alipewa ufadhili mwingine wa kuendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley, lakini alichagua kurudi Tanzania na kusoma uchumi wa kilimo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akiwa UDSM, alikuwa mwanachama wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha African Revolutionary Front. Walakini, Garang baadaye aliamua kurudi Sudan na kujiunga na waasi.

Mnamo mwaka wa 1970, Garang alikuwa katika moja ya makundi ya wanajeshi wa Gordon Muortat Mayen, kiongozi wa wakati huo wa harakati ya ukombozi wa Anyanya, aliyetumwa kwa Israeli kwa mafunzo ya kijeshi.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilimalizika na Mkataba wa Addis Ababa wa 1972 na Garang, kama waasi wengi, aliingizwa katika jeshi la Sudan. Kwa miaka kumi na moja, alikuwa mwanajeshi na alipanda kutoka cheo cha kapteni hadi kanali baada ya kuchukua kozi ya masomo ya juu ya kijeshi huko Fort Benning, Georgia, Marekani. Katika kipindi hiki alichukua likizo ya masomo ya miaka minne na alipata digrii ya Uzamili katika uchumi wa kilimo kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la Iowa (ISU). Mnamo 1981, alipata PhD katika Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Iowa State (ISU).

Garang'

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Kufikia 1983, Kanali Garang alikuwa akihudumu kama mkufunzi mwandamizi katika chuo cha kijeshi huko Wadi Sayedna kilomita 21 kutoka katikati mwa Omdurman ambapo aliwafunza makada kwa zaidi ya miaka minne. Baadaye aliteuliwa kuhudumu katika idara ya utafiti wa jeshi katika Makao Makuu ya Jeshi huko Khartoum.

Kiongozi wa Waasi

Mnamo 1983, Garang alikwenda Bor, kuwatuliza wanajeshi 500 wa serikali waliokuwa wa Kikosi cha 105 ambao walikuwa wakipinga kuhamishwa hadi kaskazini mwa nchi . Walakini, Garang tayari alikuwa sehemu ya njama kati ya maafisa wengine katika Kamandi ya Kusini kupanga kuhama kwa Kikosi cha 105 ili kujiunga na waasi waliokuwa wakiipinga serikali.

Wakati serikali iliposhambulia Bor mnamo Mei na kikosi kikaondoka, Garang alitumia njia mbadala ya kuungana nao katika ngome ya waasi nchini Ethiopia.

Ramani

Mwisho wa Julai, Garang alikuwa ameleta wanajeshi zaidi ya 3000 chini ya udhibiti wake kupitia Jeshi la Ukombozi la Wananchi la Sudan (SPLA / M), ambalo lilikuwa likipinga utawala wa kijeshi na utawala wa Kiislamu wa nchi hiyo, na kuhimiza vikosi vingine vya jeshi kufanya uasi dhidi ya hatua ya kuanzishwa kwa sheria za Kiislamu kwa nchi na serikali.

William Nyuon Bany na Kerubino Kwanyin Bol wote walikuwa wanachama waanzilishi wa SPLA. Bany aliteuliwa Kamanda wa tatu wa ngazi ya juu baada ya Bol.

Kitendo hiki kilianzisha mwanzo wa Vita vya Pili vya wenyewe kwa wenyewe vya Sudan, ambavyo vilisababisha vifo vya watu milioni moja na nusu katika zaidi ya miaka ishirini ya vita.

Garang alikuwa mtetezi mkubwa wa umoja wa kitaifa: wachache kwa pamoja walikuwa wengi na kwa hivyo walipaswa kutawala. Kwa pamoja, Garang aliamini, wangeweza kuchukua nafasi ya Rais Omar al-Bashir na serikali iliyoundwa na wawakilishi kutoka “makabila yote na dini zote nchini Sudan.” Jitihada yake ya kwanza ya kweli kwa kwa lengo hilo, chini ya usimamizi wake , ilitokea mnamo Julai 1985 na uvamizi wa SPLA kuingia Kordofan.

Kifo cha Garang’

Mwishoni mwa Julai mwaka wa 2005, Garang alikufa baada ya helikopta ya rais wa Uganda- Mi-172 aliyokuwa akisafiria kuanguka. Alikuwa akirudi kutoka mkutano huko Rwakitura na rafiki yake wa muda mrefu rais Yoweri Museveni wa Uganda. Hakuiambia serikali ya Sudan kwamba alikuwa akienda kwenye mkutano huu na kwa hivyo hakuchukua ndege ya rais. Kwa kweli, Garang alikuwa amesema atasalia kijiji cha New Cush wikendi nzima . Kijiji hicho kidogo kilikuwa karibu na mipaka ya Kenya.

Baada ya helikopta hiyo kutoweka kwa zaidi ya masaa 24, rais wa Uganda alijulisha serikali ya Sudan, ambayo iliwasiliana na SPLM kupata habari. SPLM ilijibu kwamba helikopta ya Garang ilikuwa imetua salama kwenye kambi ya zamani ya mazoezi ya SPLA.

Televisheni ya serikali ya Sudan iliripoti hivyo. Saa chache baadaye, Abdel Basset Sabdarat, Waziri wa Habari wa Sudan, alijitokeza kwenye Runinga kukanusha ripoti ya hapo awali kwamba helikopta ya Garang ilitua salama.

garang'

CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES

Baadaye ilijulikana kwamba alikuwa Yasir Arman, msemaji wa SPLA / M, ambaye alikuwa ameiambia serikali kuwa ndege ya Garang ilikuwa imetua salama na nia yake, kwa kufanya hivyo, ilikuwa kutoa muda zaidi wa mipango ya urithi wa ndani ya SPLA, kabla ya kifo cha Garang kutangazwa.

Helikopta ya Garang ilianguka Ijumaa na alitangazwa ‘kutoweka’ Jumamosi nzima. Wakati huu, serikali iliamini kuwa bado alikuwa akisuluhisha mambo yake Kusini mwa Sudan. Mwishowe, taarifa iliyotolewa na ofisi ya Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, ilithibitisha kwamba helikopta ya rais wa Uganda ilikuwa imeanguka katika milima kusini mwa Sudan kwa sababu ya ukungu uliozuia rubani kuona vizuri na kusababisha kifo cha Dk. John Garang DeMabior, wenzake sita na wafanyakazi saba wa Uganda.

Wadadisi wengi wanakubaliana kwamba John Garang alikuwa jiwe kuu la msingi katika vita vya Sudan Kusini vya kupigania uhuru. Bila Garang, watu wengi wa Afrika na hasa Sudan Kusini waliotengwa na kusahaulika hawangeweza kupata sauti na uhuru wa kujiamulia maisha yao na ya vizazi vyao vijavyo