NA ABDI SULEIMAN.
KATIBU Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni na Michezo Zanzibar, Fatma Hamad Rajab amekabidhi shilingi Milioni Moja (1,000,000/=) kwa uongozi wa kikundi cha Riziki haina mja cha mjini Ole kwa ajili ya ujenzi wa banda la kufugia kuku wa kisasa.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya fedha hizo, katika shamba la kikundi hicho kilichopo makaani mjini Ole, Wilaya ya chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema fedha hizo ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati alipofanya ziara ya kutembelea vikundi mbali mbali vya vijana na kuona changamoto zianzo wakabili.
Alisema fedha hizo zitaweza kuwasaidia katika ujenzi wa banda la kufugia kuku wao wa kisasa, kwani vijana hao changamoto kubwa kwao ni banda hilo.
Alisema vijana hao baada ya kuona wameshanufaika na kilimo cha aina mbali mbali, ndipo walipolazimika kuingia katika ufugaji wa kuku wa kisasa, ambapo kwa hatua ya kwanza wameweza kufuga kuku 150, kitu kinachoonyesha kwamba bado wanaendelea kuwa wabunifu.
“Kwakweli hawa vijana wanaonyesha juhudi kubwa na ubunifu wa hali ya juu, tuliwapatia Green House wamezitumia vizuri sasa wameingia katika ufugaji, hii ndio moja ya ajira kwa vijana”alisema.
Aliwataka vijana hao wa mjini ole kuhakikisha wanaendeleza umoja na mshikamano wao, ili kuona wanafikia malengo yao ya kujiajiri wenyewe, huku serikali ikiahidi kuwasaidia kila fursa itakapopatikana.
Naye afisa Mdhamini Wizara hiyo Pemba Salum Ubwa Nassor, aliwapongeza vijana hao kutokana na juhudi zao wanazozionyesha, huku wizara ikiendelea kuwa nao bega kwa bega ili kuona mafanikio yanapatikana.
Alisema baraza la vijana mjini Ole nimiongozi mwa mabaraza ambayo yamepiga hatua kubwa kimaendeleo, hivyo aliahidi kuwapatia wataaalamu wa mifugo ya kuku ili kuwafunza vijana hao ufugaji bora na wakisasa.
Afisa Vijana Wilaya ya Chake Chake Stara Khamis, alisema licha ya vijana hao kubuni mradi wa ufugaji wakuku wa kisasa, lakini umeonesha kuwa na changamoto kubwa kwa vijana hao, jambo ambalo linahitaji msaada kutoka serikalini ili wafikie ndoto zao.
Aidha afisa huyo aliomba kupatiwa chakula cha kukua hao, dawa, pamoja na huduma mbali mbali ili wawezee kukuwa vizuri na kuingia wengine motisha wa kufuga.
Naye msimamizi wa vijana hao sheha mstaafu wa mjini Ole Khamis Shaaban, alisema kwa hatua ya kwanza wameanza na kuku 150 ila kwa sasa wamebakia na kuku 136 baada wengine kufariki kwa maradhi.
Alisema ilikuwa kilio chao kikubwa ni upatikanaji wa banda la kufugia kuku hao, kwani sasa wameshakua na banda limekua dogo la mwanzo hali inayopelekea kutafunana.