Tuesday, November 26

Wanaharakati wapitia Sera ya Jinsia na Ujumuishi ya ZEC

Wadau / wanaharakati watetezi wa haki za Wanawake, Vijana na Watoto wamependekeza Tume ya Maadili ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ishirikishe wajumbe wengine kutoka sekta mbali mbali zikiwamo asasi za kiraia ili kuangalia, kujadili, kushauri na kupendekeza utendaji mzuri wa usimamizi wa mchakato mzima wa uchaguzi na mwenendo wa vyama vya siasa.

Maamuzi hayo yamekuja baada ya kufanya utafiti mdogo wa kupitia Sera ya Jinsia na Ujumiushi (Gender and Social Inclusion Policy) ya (ZEC) ya mwaka 2015 na kuona mapungufu yaliyosabisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoshiriki ipasavyo katika mchakato wa chaguzi zilizopita.

Wadau hao ni pamoja na Mtandao wa Jinsia Zanzibar (ZGC), Jumuiya ya Wanawake wenye Ulemavu Zanzibar (JUWAUZA), Chama Cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Jumuiya inayojihusisha na Kupambana na Changamoto zinazowakabili Vijana Zanzibar (ZAFAYCO), Jumuiya ya Vijana Zanzibar (ZYF) na Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ) ambapo walibaini mapungufu mbalimbali ikiwamo   kutokuwa na mwongozo na mpango mkakati wa kuitekeleza sera ya jinsia na ujumuishi ambayo imeundwa maalum kwa ajili ya kuangalia ujumuishi na haki za kijinsia, vijana na watu wenye ulemavu zinazingatiwa katika mchakato mzima wa uchaguzi ili demokrasia siyo tu itendeke bali ionekane kuwa inatendeka.. Hivyo wamependekeza kuwe na mwongozo maalum katika kila hatua ya uchaguzi kuanzia uandikishaji, utoaji wa elimu ya uraia, uteuzi wa wagombea, usimamizi wa uchaguzi, upigaji kura, utoaji wa matokeo na hali ya usalama na kwamba suala la usawa wa kijinsia na ujumuishi liongoze mchakato wote wa uchaguzi kabla, wakati na baada. Wadau pia wamependekeza kuwa ili kuhakikisha usawa wa kijisia na ujumuishi unafikiwa kwa kila ya hatua ya uchaguzi ZEC inapaswa kukutana na wadau wa masuala ya jinsia, vijana na watu wenye ulemavu mara kwa mara ili kuona hali ikoje na kuweka mpango wa utekelezaji ili pia kusaidia katika ukusanyaji wa takwimu kama sera ilivyosema kuwa ZEC itakuwa na mfumo madhubuti wa ukusanyaji wa takwimu  (Systematically Data Collection).

Mwenyekiti wa JUWAUZA Bi Salma Saadat amesema pia katika utafiti wamebaini uwepo wa kamati ya maadili ya ZEC ni wa muda mfupi, huundwa wakati wa uchaguzi na uhai wake humalizika mara tu baada ya uchaguzi kwisha.

Pia kamati hiyo haijawekewa mwongozo wa kushughulikia malalamiko wala haina mwongozo wa kutatua vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wakati wa uchaguzi.

“Kuna wanawake walifanyiwa vitendo vya udhalilishaji wakati wa uchaguzi lakini hawajui waende wapi kupeleka kesi zao, kwa sababu kamati haina mwongozo wa kutatua kesi za mtu mmoja mmoja, kamati inapokea kesi za vyama vya siasa tu kwa mfano kesi ya ACT Wazalendo kuhusu kiongozi wao kupinga kuwapo kwa kura za mapema ambapo alituhumiwa kuvuruga amani,” alisema Bi Salma.

Hivyo wamependekeza sera hiyo iweke mwongozo na mpango kazi ili ikidhi haja kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kushiriki ipasavyo katika mchakato mzima wa uchaguzi kama wapiga kura, wagombea, wafuatiliaji ilani na sera za vyama na hata kuhakikisha kuwa usalama wao unalindwa vyema.

Aidha Wadau wamependekeza Sera ya Jinsia na Ujumishi ya ZEC ipitiwe tena pamoja na kuipangia mpango kazi ili iweze kutekelezeka, wamesema ni vizuri ikawepo kamati ya maadili ambayo ni shirikishi inayozingatia uwiano wa kijinsia na ujumuishi wa makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Vile vile katika mapendekezo wadau wameomba katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ifanyiwe marekebisho ili wanawake waweze kuteuliwa kwenye nafasi ya Makamishna wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, kwa sababu katiba iliyopo sasa haimlazimishi Rais wa Zanzibar kuzingatia usawa wa jinsia wakati wa kuteua Makamishna wa Tume ambapo kwa sasa ZEC ina kamishna mmoja tu mwanamke na sita ni wanaume ikiwa ni sawa na asilimia 14 tu.

“Tunafahamu kuwa mamlaka ya uteuzi wa makamishna siyo wa ZEC kwa kuwa imeainishwa katika Katiba ya nchi kwamba mwenyekiti na wajumbe wengine wawili watateuliwa na rais, ambapo kati ya hao lazima mmoja awe jaji na wajumbe wengine wanne watatoka katika vyama vya siasa.

“Ili kuhakikisha kwamba ZEC inasimamia vyema Sera yake ya Jinsia na Ujumuishi ilisema kwamba mara kwa mara itakua inapendekeza kufanya marekebisho ya katiba ili masuala ya jinsia na ujumuishi yaingie katika katiba na kuifanya sera hii itekelezeke, hivyo tunashauri hatua hiyo ifanywe mapema iwezekanavyo kabla ya uchaguzi mkuu mwingine kwa sababu kumalizika kwa uchaguzi ni mwanzo wa uchaguzi mwingine,” alisisitiza Bi Salma.

 

Dkt. Mzuri Issa

Mkurugenzi,

TAMWA, ZNZ