Tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ya Ballon d’Or ilihairishwa mwaka jana kwa sababu ya janga la Corona, lakini inarejea tena mwaka huu, huku kukiwa na ushindani wa kawaida tofauti na miaka 10 iliyopita, ambapo ushindani ulikuwa mkubwa zaidi ukiwahusisha zaidi wachezaji wawili Christiano Ronaldo na Lionel Messi.
Kawaida tuzo hii hukabidhiwa kwa mchezaji aliyefanya vizuri zaidi katika mwaka husika.
Sasa baada ya kukamilika kwa mashindano mawili makubwa wiki hii ya Euro 2020 na Copa America, kumetoa mwanga wa wachezaji gani wako kwenye nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo kubwa kabisa binafsi kwenye mchezo wa soka.
Wako wachezaji wengi waliokuwa na msimu mzuri kwenye ligi mbalimbali na kufanya vizuri pia kwenye timu zao za taifa hasa kupitia mashindano ya Copa America na Euro ambayo yameongeza mwanga zaidi wa muelekeo wa tuzo hii ambayo hutolewa kila mwaka.
Ukiacha Christiano Ronaldo aliyekuwa mfungaji bora wa Euro 2020, Kevin De Bruyne aliyetwaa tuzo ya mchezaji bora England ya PFA, Gianluigi Donnarumma mchezaji bora wa mashindano ya Euro 2020 na kipa bora wa Seria A msimu huu, wafuatao ni wachezaji 6 wanaopigiwa chapuo kushinda tuzo hiyo mwaka huu
1: Lionel Messi (Barcelona & Argentina)
Mwezi mmoja uliopita kabla ya mashindano ya Copa America usingefikiria Messi kuwa miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo ya Ballon d’Or, lakini mashindano hayo yamempa nafasi kubwa zaidi.
Alitwaa tuzo hiyo mwaka 2019, lakini anashikilia rekodi ya kutwaa tuzo hiyo mara sita, akimpiku Christiano Ronaldo aliyetwaa tuzo hiyo mara 5.
Messi amekuwa na mwaka mzuri ukilinganisha na wachezaji wengine ingawa si mzuri sana ukilinganisha na miaka yake aliyokuwa bora zaidi huko nyuma.
Kinachompa nafasi zaidi Messi kwenye kutwaa Ballon d’Or ni mafanikio yake akiwa na taifa yake ya Argentina. Kwa miaka 15, Argentina ilisubri kutwaa kombe, huku Messi akisubiri katika maisha yake kutwaa kombe la kwanza kubwa akiwa na timu yake ya taifa.
Amefanikiwa mwaka huu kwa kuipa nchi yake kombe la Copa America kama nahodha wa kweli na yeye kuibuka mfungaji bora wa mashindano na mchezaji bora wa mashindano huku akitoa pasi 5 za mabao.
Katika mwaka 2021 Messi ametupia jumla ya mabao 33 na kutoa pasi za mabao 14. Amekua mfungaji bora namba mbili wa Ligi kuu ya Hispania ‘Laliga’ msimu huu na mabao yake 4 kwenye michuano ya Copa America yameisaidia sana timu yake ya Argentina kutwaa kombe hilo.
Licha ya kushidwa kuisaidia klabu yake ya Barcelona kutwaa Laliga ama ligi ya mabingwa Ulaya mwaka huu, lakini ameisaidia kutwaa Copa del Rey, hali inayomuongezea nafasi zaidi ya kutwaa tuzo hiyo mwaka huu pengine kuliko mchezaji yoyote.
Je atatwaa tuzo hiyo kwa mara ya saba na kuweka rekodi?
2: Jorginho (Chelsea & Italia)
Mara ya mwisho kutolewa tuzo hii, Jorginho alikuwa wa 15 lakini mwaka huu, kiungo huyu wa Chelsea ambaye kwa kasi yake ya kawaida anachukuliwa poa, anapigiwa chapuo la kutosha kutwaa ama kuingia tatu bora kwenye tuzo ya Ballon d’Or.
Mwaka 2021 ulipoanza hakuna hata mtu aliyefikiria kwamba angetajwa katika orodha ya wanaowania tuzo hii mwaka huu lakini umekuwa mwaka wa mafanikio kwa nyota huyu wa kimataifa wa akifunga mabao 7 kwenye ligi kuu England na kutoa pasi mbili za mabao.
Ingawa hakuwa mchezaji bora wa kuisaidia Chelsea kutwaa kombe la Mabingwa Ulaya msimu huu ama Italia ‘the Azzurri’ kutwaa kombe la Euro mwaka huu, lakini alikuwa na mchango mkubwa unaofananishwa na Luca Modric, aliyetwaa tuzo hiyo mwaka 2018 kwa mchango wake kwa timu ya taifa ya Croatia iliyofika fainali ya kombe la dunia mwaka huo.
Tangu kutua kwa kocha Thomas Tuchel kwenye timu ya Chelsea Jorginho amekuwa akionekana kutoa mchango mkubwa katika eneo la Kiungo linaoonekana kuwa imara akisaidiana na Mfaransa Ngolo Kante. Si mfungaji wa bao, si mtoa pasi nyingi za mwisho za mabao lakini mchango wake wa karata ni muhimu na umesaidia kushinda mataji.
Kwa vyovyote vile taji la ligi ya mabingwa ulaya akiwa na Chelsea na la Euro 2020 akiwa na Italia yanampa nafasi zaidi kumpiku Kante ambaye alipewa nafasi zaidi kabla ya kuanza kwa mashindao ya Euro 2020 na yale ya Copa America yaliyomuongezea alama Messi.
3: Ng’olo Kante (Chelsea & Ufaransa)
Kabla ya michuano ya Euro 2020 na ile ya Copa America kuanza wengi wa makocha, waandishi wa habari na wanaofuatilia soka, walikuwa wanamtaja Kante kama anayestahili kubeba tuzo hiyo, akiwa na kiwango bora kwenye ligi na kiwango bora zaidi katika ligi ya mabingwa Ulaya.
Ameisaidia klabu yake ya Chelsea kutwaa kombe la ligi ya mabingwa kwa kucheza mpira wa hali ya juu hasa kuanzia robo fainali, nusu fainali na fainali alipoibuka mchezaji bora wa mechi. Mfaransa huyo alikuwa mchezaji bora kwenye mechi mbili za nusu fainali dhidi ya Real Madrid, na ile ya fainali dhidi ya Manchester City.
Mwaka 2017 na 2018 ilikuwa miaka mizuri kwa Kante, lakini mkwa 2021 umekuwa mwaka mwingine mzuri kwake unaomfanya kuwa miongoni mwa watakaoweza kuingia katika orodha ya watakowania tuzo ya Ballon d’Or.
Ingawa mfaransa huyo mwenye miaka 30 ameshindwa kuisaidia nchi yake ya Ufaransa kufanya vyema kwenye mashindano ya Euro 2020 yaliyomalizika mwishoni mwa wiki kwa kuondolewa na Switzerland, lakini mchango wake kwa Klabu yake ya Chelsea hasa kwenye ligi ya mabingwa unamfanya kupigiwa chapuo.
4: Federico Chiesa (Juventus & Italia)
Kiungo wa pembeni wa Italia, ambaye wakati huu umekuwa na mwaka mzuri katika maisha yake ya soka, licha ya kushindwa kutwaa ubingwa wa Italia mbele ya Inter Milan, lakini alisaidia Juventus kushinda Coppa Italia na Supercoppa Italia.
Licha ya kuwa Juventus imeutema ubingwa wa ligi Scudetto baada ya miaka 9, lakini kwa kiung huyu mwenye umri wa miaka 23, na anayeweza kucheza eneo lote la mbele kushoto kati ama kulia, amepiga soka la uhakika. Ameifungia Juventus mabao 15 katika mashindano yote na kutoa pasi za mabao 11.
Kinachomweka kwenye orodha hii ni kiwango chake kwenye Euro 2020 na kuisaidia timu yake ya taifa ya Italia kutwaa kombe hilo kwa mikwaju ya penati dhidi ya England. Katika mashindano hayo alifunga mabao mawili dhidi ya Austria na Hispania.
Haishangazi kumuona akitajwa tajwa kuwa katika orodha ya watakaowania tuzo ya Ballon d’Or 2021, kutokana na kiwango chake kikubwa mwaka huu akiwa na Juve na timu yake ya Italia.
5: Harry Kane – ( Tottenham & England)
Mshambuliaji huyu wa Tottenham, ni hatari linapofika suala la kufunga mabao. Amekuwa na msimu wa kuburudisha usio na makombe, akitwa kiatu cha dhahabu akifunga mabao 23 katika ligi kuu ya England. Kama haitoshi ametwaa tuzo ya mchezeshaji bora kwa kutoa pasi nyingi za mabao.
Katika historia ya ligi hiyo ni mchezaji wa 3 kushinda tuzo hizo katika msimu mmoja.
Harry Kane ameiongoza pia timu yake ya England kuingia fainali ya Euro 2020 ikiwa ni kwa mara ya kwanza kabisa na fainali kubwa kwa timu hiyo katika miaka 55. Alifunga mabao 4 katika hatua za mtoano baada ya kuanza kwa ukame katika mechi 3 za kwanza za makundi.
Ni nahodha wa klabu na timu yake ya taifa, anachojivunia zaidi ni mafanikio binafsi ya kupachika mabao ingawa hafikiriwi kushinda, lakini anatajwa katika wale watakaoingia 10 bora.
6: Robert Lewandowski (Bayern Munich & Poland)
Bila shaka, huyu ni mchezaji aliye na mafanikio binafsi ya kujivunia zaidi katika ligi za Ulaya msimu huu. Ametwaa tuzo ya the Golden Shoe kwa kupachika mabao mengi zaidi kwenye ligi tano bora Ulaya, kunakomfanya kumsogeza karibu katika orodha ya wanaowania tuzo ya mwaka huu ya Ballon d’Or
Kama mwaka jana, tuzo hizi zisingeahirishwa bila shaka mshambuliaji huyu wa kimataifa wa Poland alikuwa anainyakua bila wasi. Alifanikiwa kutwaa tuzo ya Mchezaji bora wa kiume wa FIFA na kua mchezaji bora wa mashindano ya mwaka huu ya klabu bingwa ya dunia. Kwa uwezo wake wa kupachika mabao kunamrejesha kweye ramani ya tuzo hiyo kwa mwaka 2021.
Amekuwa mfungaji bora wa ligi ya Ujerumani msimu uliomalizika kwa kupachika mabao 41 na kuisaidia klabu yake ya Buyern Munich kutwaa ubingwa wa ligi hiyo na michuano ya klabu bingwa ya dunia.
Kwa ujumla msimu uliomalizika lewandowksi amepachika mabao 48 na kutoa pasi 9 za mabao. Ameifungia pia Poland mabao 3. Huyu jamaa angekuwa na timu ya taifa inayofanya vizuri zaidi, isingekuwa ajabu kumuona tatu bora ya tuzo kila mwaka hasa kuanzia msimu wa 2016/2017 mpaka sasa.