Walter Nguma- Mchambuzi wa Uchumi, Tanzania
Hii leo (Jana) , Julai 15 2021 gharama ya miamala ya fedha kupitia mitandao ya simu nchini Tanzania imepanda baada ya serikali kupandisha tozo ya miamala hiyo.
Sintofahamu kubwa inashuhudiwa hii leo kwa wananchi wa Tanzania ambao wengi wao ni watumiaji wakubwa wa huduma hiyo.
Hali hii imepelekea maswali mengi kwa wananchi na kujiuliza hatma yao kiuchumi itakuwa vipi ikiwa hali ya kiuchumi hivi sasa ni tia maji tia maji kwani uchumi wa nchi hii sasa unakadiriwa kushuka kutoka 7.0% mpaka 4.8% na hivyo wananchi wamebaki kujiuliza nafuu ya maisha kwa hivi sasa kupitia serikali ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wataipata ikiwa kila huduma muhimu kuna ongezeko la tozo?
Mpaka hivi sasa kunaongezeko la tozo kwenye mafuta ya petrolI, dizeli na mafuta ya taa ya kiasi cha shilingi mia moja (100) kwa kila lita moja. Tozo kwenye mita za luku kutokana na jinsi mtumiaji anavyotumia, tozo kwenye kadi za simu.
Bomu hili jipya linawafanya baadhi ya wananchi kung’aka mitandaoni na kusema hakuna haja ya kutumia njia hii katika kutuma fedha na kuona ni afadhali ya kutumia bodaboda au kupakia gari na kupeleka fedha hizo kunakohusika. Ikitokea hivyo, hali hiyo itakuwa hatari kiuchumi kwani itasababisha mzunguko wa fedha kusinyaa.
Athari za tozo hii kiuchumi
Kuzorota kwa biashara za mitandaoni. Ongezeko la tozo hizi kwenye miamala ya simu itapelekea wakati mgumu sana kwa wafanyabiashara wa mitandaoni, kwani watumiaji wa huduma hiyo wataachana au wataondokana na kutumia huduma hiyo kutokana na kuongezeka kwa gharama na hasa ukizingatia watumiaji wengi wanatumia njia ya simu katika kulipia bidhaa wanazonunua kupitia online (mtandaoni).
Mfumuko wa bei za bidhaa na huduma. Kama kuna ongezeko la fedha katika miamala ya simu ni fika gharama za huduma au bidhaa zitaongezeka hasa kwa wale watakaolipia kwa njia ya simu. Hivi sasa kuna hatari ya mfumuko wa bei katika bidhaa mbalimbali pamoja na huduma mbalimbali ikizingatia kuwa kuna ongezeko la tozo kwenye mafuta ya petrol na dizeli na ikizingatiwa kuwa kuna tozo pia kwenye kadi za simu. Hivi sasa mfumuko wa bei upo kwenye tarakimu 3.3% na ongezeko la tozo mbalimbali kunaweza kukapandisha hali ya mfumuko.
Mzunguko wa fedha kudorora. Tozo hizi kama zitapelekea watu kupunguza kasi ya matumizi ya huduma hii katika kutuma na kutolea miamala ya fedha basi ni fika kabisa kutakuwepo na mdororo mkubwa sana wa mzunguko wa fedha na hivyo kuendelea kufanya hali ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja kuendelea kuwa ngumu zaidi maradufu.
Gharama za maisha kuongezeka. Gharama za maisha za watu zitaongezeka hasa ukizingatia kuwa kuna ongezeko la gharama za huduma mbalimbali pamoja na hili la tozo za miamala ya simu wakati pato la mtu mmoja mmoja limeendelea kuwa lile lile na wengine limeshuka kabisa kutokana na athari zilizosababishwa na CORONA (COVID-19)
Kuyumba kwa sekta binafsi. Sekta binafsi hivi sasa bado haiko imara kutokana na vimbunga ambavyo sekta hii imepitia hapo miaka michache iliyopita lakini hivi sasa sekta hii, kwa asilimia kubwa ya tozo zilizoongezwa katika bajeti ya mwaka huu 2021/2022 itapelekea biashara mbalimbali kuyumba, kwani hivi sasa wateja wao wamejipanga kupunguza matumizi (expenditure) na kwa vyovyote vile pale ambapo raia watapunguza matumizi yao ni fika kabisa biashara nyingi zitaathirika kwa ukubwa sana.
Serikali ifanye nini ili kusaidia wananchi kiuchumi?
Punguzo la kodi ya ongezeko la thamani, VAT kutokana na kwamba tayari tozo zilizoongezwa katika makundi tofauti tofauti. serikali wapitie sheria ya VAT ili kuweza kupunguzia wananchi maumivu ya kupaa kwa gharama za kimaisha. Asilimia ya VAT iliyopo hivi sasa ya 18% ukiweka na tozo hizi zilizoletwa kwenye bajeti ya mwaka huu 2021/2022 mwananchi anakuwa na mzigo mkubwa sana kwa mwaka huu mpya wa kifedha 2021/2022.
Tozo za kadi ya simu; serikali ili kuwaondolea maumivu na mzigo mkubwa wa kodi na hivyo napendekeza Serikali kuwafutia wananchi tozo ya kadi za simu angalau inaweza kuwapa nafuu kidogo ya kimaisha.
Serikali itafute namna ya kuweza kupata mapato bila ya kuathiri sana shughuli za wananchi kwani hiyo itasaidia wananchi kuweza kujijenga vizuri kiuchumi hapa nchini Tanzania. Hili linaweza kufanyika kwa ufanisi kwa kufanya tafiti yakinifu juu ya namna ya kuweza kupata vyanzo vipya vya kimapato kuliko kuendeleza kutegemea vyanzo vilevile kila wakati ,huko kutapelekea kudumaza uchumi wa nchi wakati huu wa mdororo wa kiuchumi duniani.
CHANZO CHA HABARI BBC