ABDI SULEIMAN.
JUMLA ya Chupa 26 za damu zimekusanywa na kitengo cha Damua salama Kisiwani Pemba, katika bonanza maalumu la uchangiaji damu lililoandaliwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Kusini Pemba Maryam Azani Mwinyi.
Akizungumza na wanamichezo na wananchi mbali mbali, Mbunge huyo wa Viti Maalumu Kusini Pemba, aliwataka akinamama wenzake kujitokeza kwa wingi katika masuala ya uchangiaji wa damu, ili kuokoa maisha ya wagaonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
Alisema bado hospitali zinahitaji sana kupata damu, kwani wagonjwa wamekuwa wakiongezeka huku damu nyingi ikitumiwa na akinamama wakati wakujifungua na wagonjwa wanaofanyiwa upoasuaji.
“Hili jambo ambalo nimelifanya leo ni jambo kubwa sana, kila ambaye ataweza kuchangia damu fungu lake liko kwa mungu, hapoa anaweza kuokoa maisha ya wagonjwa”alisema.
Hata hivyo mbunge huyo aliwashukuru madaktari wa kitengo cha damu salama Pemba, pamoja na wananchi waliojitokeza kuchangia damu, huku akiahidi kuendelea kushajihisha wananchi kuchangia damu kupitia mabonanza mbali mbali anayotarajia kuyafanya.
Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, alisema suala la uchangiji wa damu ni hiyari ila mchangiaji anapata fungu kubwa kwa mwenyezi Mungu, kwani damu hutumika kwa ajili ya kuokoa maisha ya wagonjwa mbali mbali.
Aidha aliwataka wananchi wa mkoa wa kusini kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi, katika mabonanza yanayoanzishwa kwa ajili ya uchangiaji damu, ili kusaidia maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo.
“Bonanza limekuja katika kipindi muwafaka damu hii itakayopatikana itaweza kusaidia wagonjwa hopitali, hivi sasa tunakambi ya madkatari binga damu nyingi inahitajika”alisema.
Akichangia damu katika bonanza hilo, mbunge wa jimbo la Chake Chake Ramadhani Sulieman,alimpongeza mbunge wa viti maalumu wanawake Mkoa wa kusini Pemba, kwa mikakati yame mizuri ya kuhakikisha anasaidia wagonjwa katika suala la damu.
Alisema utoaji wa damu unafaida kubwa kwa mchangiaji, kwani ni sadaka inayoendelea pale itakapotumiwa na mgonjwa, hususana akinamama ndio wanaohitaji damu.
Naye afisa mdhamini Wizara ya Afya Ustawi wa Jami, Jinsia Wazee na watoto Yakub Mohamed Shoka, aliwashukuru wananchi waliojitolea kuchangia damu kupitia bonanza hilo.
Nao wananchi waliochangia Damu, wamewataka wananchi wenzao panapotokea fursa ya kuchangia damu, vizuri kujitokeza kwa wingi kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya mama na mtoto.