Thursday, January 16

Rais Dk Hussein Mwinyi awaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na  Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dk. Hussein Ali  Mwinyi, leo amewaapisha  Makatibu Wakuu mbali mbali aliowateuwa Julai 30, 2021, kushika nyadhifa hizo.

 

Katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu Jijini Zanzibar, Dk. Mwinyi amemuapisha Dk. Omar Dadi Shajak kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar pamoja na Khadija Khamis Rajab  kuwa Katibu Mkuu anaeshughulikia masuala ya Kazi na Uwezeshaji katika Wizara ya Nchi (OR) Kazi, Uchumi na Uwekezaji.

 

Aidha, amemuapisha Dk. Habiba Hassan Omar kuwa Katibu Mkuu anaeshughulikia masuala ya Uchumi  na Uwekezaji katika Wizara ya Nchi (OR) Kazi, Uchumi na Uwekezaji, sambamba na kumuapisha  Dk. Fatma Haji  Khafidh kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na watoto.

 

Vile vile, Dk. Mwinyi amemuapisha Khamis Kona Khamis, (aliemteua Julai 16, 2021) kushika wadhifa wa Mkurugenzi  Tume ya Uchaguzi Zanzibar.

 

Nao, baadhi ya Watendaji  walioapishwa, walisema watashirikiana na watendaji pamoja na wadau mbalimbali katika maeneo yao ili  kuhakikisha  wanafikia malengo.

 

“Nitatumia nguvu na uwezo wangu wote kushirikiana na watendaji wa Tume na wadau mbaIi mbali wa Uchaguzi kufanikisha masuala ya msingi ya Tume hiyo”, alisema Mkurugenzi Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) khamis Kona Khamis.

Alisema majukumu ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kimsingi yameanishwa kisheria, hivyo atajitahidi kusogeza mbele majukumu hayo ili kufikia malengo.

 

Aidha, Katibu Mkuu anaeshughulikia masuala ya Uchumi  na Uwekezaji katika Wizara ya Kazi, Uchumi na Uwekezaji Dk. Habiba Hassan Omar alisema ataimarisha Uwekezaji na kuhakikisha anapunguza changamoto mbali mbali ziliopo ikiwemo urasimu, huku akiunga mkono hatua ya ZIPA kuanzisha ‘One Stop centre’, pamoja na kuainisha umuhimu wa kuendeleza Uwekezaji kwa njia ya ubia (Public Private  Partnership –  PPP).

 

Viongozi mbali mbali walishiriki katika hafla hiyo, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na  Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmed Said, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar Dk. Mwinyi Talib Haji pamoja na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Idrissa Kitwana Mustafa.

 

Wengine  ni pamoja na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaab, Mawaziri, Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama, Meya wa Jiji la Zanzibar  Mahamoud Mussa, Viongozi wa Dini na Vyama vya Siasa pamoja an Wanafamilia.