NA ABDI SULEIMAN.
VIJANA wa Wilaya ya Chake Chake, wameshauriwa kujiweka tayari kuziendea fursa zinazotarajiwa kujitokeza hivi karibuni, ili kuweza kuondosha changamoto za ukosefu wa ajira unawakubwa vijana.
Ushauri huo umetolewa na Mwakilishi wa jimbo la Chake Chake Bakari Hamad Bakari, wakati alipokua akizungumza na viongozi wa baraza la Vijana Wilaya ya Chake Chake katika mkutano mkuu wake wa kwanza, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Gombani.
Alisema Serikali ya Mapinduzi imejipambanua kwenda na uchumi wa viwanda na uchumi wa buluu, lazima vijana kujiweka tayari kuziendea fursa hizo zitakazotokea katika mambo hayo.
“Hivi sasa tumesikia Pemba tayari kiwanda cha maji kimeanza harakati za ujenzi, wanufaika wakubwa ni vijana ipi haja ya kukaa tayari kuzichangamkia fursa hizo”alisema.
Hata hivyo aliwataka vijana hao kujiwekeza katika harakati zakilimo, kwani viwanda haviwezi kwenda kama hazvna malighafi, lazima tujiekeze katika kilimo ikiwemo cha bahari na kilimo chengine.
Akizungumzia suala la ajira aliwataka kutumia ajira zinazotokana na shuhuli za ujasiriamali, kupitia vikundi vya ushirika kwani ajira za serikali hazitoshi na hakuna serikali yoyote duniani inayoweza kuwajiri vijana wake wote.
Aidha aliwataka vijana kuendelea kudumisha kudumisha, kuenzi na kulea amani na utulivu wa nachi, kwani amani iliyopo bila ya vijana kuiendeleza na kuidumisha, hatuwezi kuwa nayo kundi kubwa lililoko katika jamii ni kundi la vijana.
“Vijana wakiamua kuivunja amani hiyo, basi jamii yote itakosa amani, wajibu ni kuhakikisha tunadumisha amani na utulivu, watu wengi wanafahamu amani inalindwa na polisi na jeshi bali inalindwa na wananchi wenyewe”alisema.
Alifahamisha kuwa wakati wa siasa umekwisha, huu ni wakati wa kufanya kazi kwa pamoja, Serikali ya iliyopo imeshirikisha vyama vya siasa na vipo, kwani wajibu kuhakikisha amani hiyo na wakati ule wa siasa za fitna, majungu, ugomvi ya kisiasa umepita, huu ni wakati wa kukaa pamoja na kushirikiana na kuhakikisha nchi inapiga hatua kimaendeleo.
Hata hivyo alisema vijana wanawajibu wa kuunga mkono serikali SMT na SMZ, ili nchi iweze kufika kule inakotakiwa kwani kuunga mkono huko ni kuhakikisha amani na utulivu inadumu.
Mwenyekiti wa baraza la vijana Wilaya ya Chake Chake Fihimu Abdalla, alisema lengo la mkutano huo ni kuwakusanya na kutatua changamoto zao kwa kujadili yanayowahusu na kuwatatulia.
Alisema hivi karibuni walitembelea mabaraza ya vijana na kugundua kuwa vikundi 58 vimeanzishwa huku asilimia 20 tu ya vikundi ndio ambavyo vimesajiliwa na kutambuliwa.
Alifahamisha kuwa katika vikundi 58 ni asilimia 10% ya vikundi ndio vilivyopatiwa ruzuku za serikali, wakati changamoto kubwa ya vijana ni ukosefu wa soko la kuuzia bidhaa zao, ukosefu wa elimu, ushirikishwaji wa vijana, pamoja na migogoro kwa viongozi wa mabaraza ya vijana wapo wanaotaka kujiuzulu licha ya muda mchache walioingia.