Thursday, January 16

Wanawake Watayarishwe katika Uongozi kabla ya Uchaguzi Mkuu

 

Vyama vya siasa vimeshauriwa kuwatayarisha wanawake katika nafasi ya uongozi mapema kabla ya kufikia kipindi cha Uchaguzi Mkuu ili waweze kugombea nafasi mbali mbali za uongozi.

Ushauri huo umetolewa leo na wajumbe wa Kamati ya Wanaume wa Mabadiliko (Male change agent) katika kikao cha pamoja na maafisa wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ) kilichofanyika Tunguu kwenye ofisi ya chama hicho kutathmini hali ya ushiriki wa wanawake katika uchaguzi mkuu wa 2020.

Wanaume zaidi ya 22 kutoka Unguja na Pemba wakiwemo wafuasi wa vyama mbali mbali, wataalamu wa masuala ya jinsia na viongozi wa dini  wameanzisha mtandao miaka mitatu iliyopita ili kuhamasisha  jamii kumpokea mwanamke kama kiongozi halali kama walivyo wanaume.

Mwenyekiti wa kamati ya wanaume wa mabadiliko bw, Mohammed Jabir Makame amesema mifumo mibaya ya vyama vya siasa  inapelekea wanawake kushindwa majimboni kwasabu hawajatayarishwa na vyama vyao kwa kuwapa nafasi ya kuongoza ndani chama.

 “Wanawake wanapewa nafasi ya kugombea jimbo wakati wa uchaguzi mkuu bila ya kumtayarisha kwanza ndani ya chama chake hivyo sio rahisi kushinda jimboni. Kwanza chama kimtayarishe kwa kipindi cha miaka minne nyuma kabla ya kufika uchaguzi mkuu, kwa kumpa nafasi ya kuongoza ndani ya chama chake” Alisema Makame.

Pia amesema awali wanawake walikuwa na woga wa kugombea nafasi ya majimboni lakini baada ya kuhamasishwa wanawake wengi walijitokeza kugombea katika majimbo katika uchaguzi mkuu wa 2020 ambapo wanawake 435     waliweza kutia nia na wanawake 216  waligombea.

Kwa upande Pemba mwanaume wa mabadiliko bwana Omar Mjaka Ali amesema mbali na utayari wa wanawake lakini pia wamekabiliwa na kikwazo cha kiuchumi hivyo kinapelekea kukosa kushinda nafasi za majimboni kwasababu harakati za uchaguzi zinahitaji fedha kuanzia uchukuwaji wa fomu na mzunguuko mzima wa kampeni.

Aidha wanaume wa mabadiliko wamesema wamejifunza mengi kutokana na harakati hizo za kutoa elimu kwa jamii kumkubali mwanamke kua kiongozi ikiwemo ulinganisho wa sheria, Quran na Hadithi za dini ya kiislam. Wamesema katika juhudi hizo walikua wakitembea na viongozi wa dini ili  jamii ifahamu kwamba dini ya kiislam haikukataza mwanamke asiwe kiongozi.

Takwimu zainaeleza kuwa hadi sasa wanawake katika vyombo vya maamuzi hasa kupitia nafasi za kugombea ni wachache sana ambapo kwa mujibu wa uchaguzi wa mwaka 2020, kwenye udiwani wanawake ni 25 sawa na asilimia 22.72%,  Baraza la wawakilishi ni 8 sawa na asilimia  16%  ubunge ni  4 sawa na asilimia 8%  na Uraisi ni 0.

Mwisho wanaume hao wa mabadiliko wameiomba Chama Cha Waandishi wa Habari  Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA,ZNZ) na wadau wengine kuendelea kutoa fursa za kuwajenga uwezo  wanawake, vijana wakike na kuwapa  hamasa kuingia katika uongozi pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa jamii imkubali mwanamke kwamba wanaweza kuongoza na dini sio kikwazo cha kumzuia asiwe mbunge, mwakilishi wala diwani.

Wanaume wa mabadiliko walifanya kazi  kupitia mpango  wa kuwainua wanawake katika siasa na uongozi (WPEL) unaosimamiwa na Chama Cha Waandishi wa Habari  Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA,ZNZ) kwa mashirikiano na  Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na mambo ya wanawake (UN Women).

Dkt. Mzuri Issa

Mkurugenzi,