Thursday, January 16

KAMISAA wa Sensa ya watu na Makazi Zanzibar amekutana na wadau wa sensa Mkoa wa Kaskazini Pemba.

NA ABDI SULEIMAN.

 

KAMISAA wa Sensa ya watu na Makazi Zanzibar, Balozi Mohammed Ali Hamza amekutana na wadau wa sensa Mkoa wa Kaskazini Pemba na kuwataka kila mmoja kwa mujibu wa nafasi aliyonayo, kuhakikisha anatumia nafasi yake kuihamasisha jamii kushiriki katika zoezi hilo.

 

Akizungumza na wadau wa sensa kwa nyakati tofauti, Balozi Hamza alisema sensa ni muhimu katika kufanikisha maendeleo ya nchi, kwani inaiwezesha Serikali kutambua nguvu kazi pamoja na kutambua jinsi ya kutumia raslimali zilizopo kulingana na utoaji wa huduma za kijamii.

 

Alisema huduma zote za maendelo ya jamii na kiuchumi katika nchi, zinahitaji kujulikana kwa idadi sahihi ya wananchi, ndipo tutakapojua mahitaji ya nguvu kazi, pamoja na kutumia malighafi zako vipi.

 

Aidha balozi huyo alifahamisha kuwa sense hiyo itawezesha pia serikali kujuwa huduma zake itaweza kuzitoa vipi, hivyo zoezi hilo la sense ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi na nchi yoyote duniani.

 

Alisema Tanzania imekua ikifanya sense hiyo ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya sense ya kimataifa, ambapo hufanya kwa kufuata viwango vya kimataifa.

 

“Sisi nchi lazima tufanye sense hii ili tuweze kujuwa idadi ya wananchi wetu, katika kupanga mambo mbali mbali ya maendeleo ya taifa”alisema.

 

Kwa upande wao maafisa kutoka Idara ya Takwimu Zanzibar, walisema sensa ya mwaka huu ni tofauti ya miaka iliyopita, kwani inatumia njia ya kidigital hali ambayo itaepusha wananchi kuhebiwa zaidi ya mara moja.

 

Msimamizi mkuu wa zoezi la kutenga maeneo ya kuhesabia Zanzibar Ahmad Hamza Mohammed, alisema wanatarajia kuweka teknolojia wakati wa zoezi hilo la sense litakalojulisha eneo husika.

 

“Mwaka huu hakutakua na sababu ya mtu kuhesabiwa mara mbili, kutokana na vifaa tutakavo tumia kwani ukiingia katika eneo ambalo sio lako basi kifaa kitakupigia alam hapo utajuwa umeingia eneo sio na hutoweza kufanya kazi”alisema.

 

 

Nae afisa habari kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Salama Njani Khamis, alisema jukumu lao ni kuhamasisha wananchi ili waweze kushiriki kikamilifu na kupata matokeo chanya ya sense hiyo.

 

“Sense ni gharama kubwa lazima wa gharamike sana kwa nguvu zetu, ili tuweze kupata takwimu sahihi zitazowezesha kuweza kupanga mipango ya maendeleo kwa miaka kumi inayokuja”alisema.

 

Nao wakuu wa Wilaya ya Micheweni na Wete wameahidi kutoa ushirikiano ili zoezi hilo liweze kufanikiwa, huku wakiwataka wananchi kuwa tayari kuhesabiwa wakati utakapofika.

 

Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Mohamed Mussa Seif (Mkobani), alisema watahakikisha watazungumza na vyama vya siasa, kamati za ulinzi ili kuona sense hiyo inafanikiwa.

 

Sensa ya watu na makazi inatarajia kufanyika wiki ya mwisho ya mwezi wa nane mwakani, ambapo itatanguliwa na sensa ya majaribio itakayofanyika baadaye mwezi huu.