Wednesday, January 15

Maofisa Utumishi wa Taasisi za serikali Pemba wapatiwa mafunzo.

NA ABDI SULEIMAN.

MKUU wa Mkoa Kusini Pemba Matar Zahor Massoud, amesema kuwa maafisa Utumishi wa Taasisi za Serikali wananafasi kubwa ya kuwasaidia wakuu wao katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi zao.

Alisema maafisa hao ndio roho ndani ya Taasisi, hivyo wanapaswa kutambua dhamana na dhima zao katika taasisi, pamoja na kuzifahamu kwa kina sheria na kanuni za utumishi.

Mkuu huyo aliyaeleza hayo wakati akifungua mafunzo ya maofisa utumishi wa taasisi za serikali yaliyoandaliwa na Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Pemba na kufanyika katika ofisi za taasisi hiyo Gombani.

Aidha alisema wakati umefika kwa maafisa hao kubadilika na kuwa washauri wakubwa kwa viongozi, huku wakitambua thamani ya taasisi zao kwa jamii.

“Vizuri katika kazi zetu kufahamu vifaa vyetu tunavyofanyia kazi, ukiwemo mkataba wa huduma kwa wateja na kujuwa sheria kanuni na kiongozo yote ya utumishi”alisema.

Hata hivyo aliwasihi maafisa hao kutokua chanzo cha migogoro ndani ya taasisi zao, badala yake wanapaswa kuwa waunganishaji wa wafanyakazi na wakuu wao wa taasisi.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka maafisa Utumishi kusimamia nidhamu na uwajibikaji kwa wafanyakazi, ikizingatiwa wananafasi kubwa ya kurekebisha sehemu ambazo zikuwa na matatizo.

Mapema akimkaribisha mkuu huyo wa Mkoa, Afisa Mdhamini Ofisi ya Rais Katiba, Sheria, Utumishi wa Umma na Utawala Bora Pemba Halima Khamis Ali, alisema lengo la Mafunzo hayo ni kubadilishana Uzoefu kwa maafisa Utumishi, pamoja na kujuwa taratibu na wajibu wao katika kuhudumia taasisi zao.

Halima alisema maafisa utumishi wananafasi kubwa ya kuwaunganisha wafanyakazi wa taasisi zao, pamoja na kuipatia sifa njema taasisi hizo.

Akiwasilisha mada wajibu wa Afisa Utumishi juu ya kusimamia haki za watumishi, Afisa Rasilimali watu Hamad Juma Hassan alisema uwajibikaji wa Maafisa Utumishi katika wizara na taasisi ni muhimu sana ili kuweza kutimiza haki za watumishi jambo ambalo litapelekea watumishi hao kutekeleza majukumu yaio ipasavyo na kutoa mafanikio katika utumishi na jamii kwa ujumla.

Aidha alisema maafisa utumishi wanawajibu mkubwa wa kusimamia na kuona kila mtumishi ktika taasisi mwenye kustahiki kupata haki anaipata bila ya kuwepo vikwazo vya aina yoyote na kwa wakati.

“Wajibu wa afisa Utumishi anatekeleza wajibu huo kwa kufuata sheria, kanuni, sera na Miongozi ya kiutumishi kama inavyotolewa na Ofisi ya Rais katiba sheria na utumishi na utawala bora”alisema.

Hata hivyo alisema sababu za maafisa utumishi kutosimamia haki za watumishi ni kutokana na ubinafsi wao, kutokujua/kukosa taarifa na uelewa mdogo wa utekelezaji wa miongozi mbali mbali yanayotolewa.

Kwa upande wake Afisa Miundo na Taasisi Rehema Alawi Abdalla, akiwasilisha mada ya mkataba wa huduma kwa wateja, lengo la mktaba huo ni kubadilisha utamaduni katika utumishi wa umma na kuwafanya watumishi kuondokana na utamaduni wa kufanya kazi kimazoea.

Wakichangia katika mkutano huo maafisa Utumishi kutoka taasisi za serikali Pemba, wameitaka Ofisi ya Rais katiba sheria utumishi na utawala bora, kuhakikisha wanapotoa mafunzo hayo kuwashirikisha na viongozi wa taasisi na sio maafisa utumishi peke yao.