Thursday, January 16

Walimu wakuu wastaafu kuendelea kusaidia jamii katika suala la elimu kwenye maeneo wanayoishi.

BAADHI ya walimu wakuu wa Skuli za Wilaya ya Wete, wakifuatilia kwa makini hafla ya maagano ya walimu wakuu waliomaliza muda wao wa utumishi Serikalini, hafla iliyofanyika ukumbi wa Walimu Mitiulaya.

 

MBUNGE wa Viti Maalumu Wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, akizungumza katika hafla ya maagano ya walimu wakuu waliomaliza muda wao wa utumishi serikalini , hafala iliyofanyika katika kituo cha walimu Mitiulaya Wete.
MBUNGE wa Viti maalumu Wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, akimkabidhi zawadi Mwalimu Mstaafu Ramla Omar Saleh, ambae amemaliza Utumishi wake serikalini wakati wa hafla ya maagano iliyofanyika katika kituo cha walimu Mitiulaya Wete.
AFISA Mdhamini Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salim, akimtolewa wasifu wake juu ya ufanyaji kazi bora na kuhamasisha jamii juu ya suala zima la usafi wa mazingira Kojani, mwalimu Msaatafu Bakari Issa Omar kutoka Kisiwa cha Kojani, wakati wa hafla ya maagano iliyofanyika katika kituo cha walimu Mitiulaya Wete

(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

 

NA ABDI SULEIMAN.

MBUNGE wa Viti Maalimu Wanawake Mkoa wa Kaskazini Pemba Asiya Sharif Omar, amewataka walimu wakuu wa staafu kuendelea kusaidia jamii, katika suala zima la upatikanaji wa elimu kwa watoto kwenye maeneo wanayoishi.

Asiya alisema walimu wastaafu wanaujuzi mkubwa katika ufundishaji, hivyo wasichoke kuwasaidia wanafunzi katika masomo yao, wakati wa masomo ya ziada ili jamii iyendelea kunufaika na matunda yao.

Wito huo aliutoa huko katika ukumbi wa kituo cha walimu Mitiulaya wete, wakati alipokua akizungumza na walimu wa kuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, wakati wa hafla ya kuwaaga walimu waliomaliza muda wao wa utumishi.

Alisema walimu ni kiyoo cha jamii, hivyo bado wanahitajika kuendelea kutumiwa na jamii, kutokana na kuendelea kuwa msaada kwa jamii.

“Walimu wataendelea kuwa na sifa na hali yao kuksaidia wengine, ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na jamii, ikiwemo kukuza suala la elimu katika jamii yao”alisema.

Aidha aliwataka walimu kushirikiana na wazazi katika kusimamia malezi ya wanafunzi kwa kufanya ufuatiliaji kuwaeleza wazazi juu ya mwenendo wa watoto wao ili kuzipatia ufumbuzi changamoto zao ikiwemo suala zima la utoro.

“Kutokana na wimbi la Vitendo viovu kuwa kubwa, imefika wakati wazazi kukosa imani na walimu katika kuwaachia watoto wao, jambo ambalo linatia doa na sekta ya elimu”alisema.

Hata hivyo aliwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao pamoja na kuwa wawazi kwao, juu ya matando maovu yaliyopo ikiwemo utumiaji wa madawa ya kulevya.

Mapema afisa Mdhamini Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Nassor Salum, aliwataka walimu wastaafu kuishi kwa uzalendo, umoja na mashikamano kwa lengo la kuhakikisha wanawasaidia vijana wao wanapokua mitaani.

Afisa EDlimu Mkoa wa Kaskazini Pemba Khamis Said Hamad, aliwataka walimu wakuu wenzake kuwamini viongozi wao na sio kwenda moja kwa moja kwa viongozi wa kubwa wanapokua na matatizo.

“Uongozi hauko hivyo lazima kwanza unapokua na tatizo kufuata ngazi kwa ngazi na sio kukimbilia kwa wakubwa tu, huyo mkubwa baadae anatuuliza sisi wasaidizi wake”a;isema.

Afisa elimu Wilaya ya Wete Riziki Makame Faki, alisema walimu wakuu hao wastaafu walikua ni muhimu sana, hivyo kuondoka kwao masikitiko makubwa kwani walikuwa wakiwategemea katika mambo mbali mbali.

Akitoa neno la shukurani kwa niaba ya walimu wastaafu wenzake, Mwalimu Ramla Omar Saleh, aliwataka walimu ambao wapo kazini kuhakikisha wanafanyakazi kwa upendo, uaminifu kuhakikisha elimu inasonga mbele na wanapata matokeo mazuri.

Akisoma risala ya jumuiya ya walimu wakuu wilaya ya wete, mwalimu Mkuu wa skuli ya Kizimbani msingi Azani Juma Abdalla, amesema wakati wa utumishi wa walimu hao walikuwa watendaji mahiri katika kuleta mabadiliko ya kielimu juu ya kujenga jamii iliyoelimika.