Na Raya Ahmada.
Wanawake wa shehia ya Kiungoni wilaya ya Wete wamesema kukabidhiwa hati za kumiliki ardhi zao itaondosha umaskini pamoja na migogoro ya kuuzwa kwa mali zao kwa watu wasiowafahamu.
Akizungumza na ZBC Yussuf Omar Khamis amesema ameshuhudia mama yake akilinunua shamba lao kwa mtu mwengine aliedai kuuziwa, ambapo Time Ali Hamad na Halima Ali wamesema hati hiyo itawasaidia kupata mikopo katika taasisi mbali mbali.
Wananchi hao wametowa kauli hiyo ofisi za sheha wa shehia ya Kiungoni baada ya zoezi la kukabidhiwa hati za kumiliki ardhi kwa wanawake nane zilizogharamiwa na jumuiya ya KUKHAWA ambazo zimepimwa kupitia mradi wa MKURABITA.
Mkurugenzi wa jumuiya ya KUKHAWA Khafidh Abdi Said amewataka wanawake hao kuwahasisha wananchi kuchukua hati zao ili waweze kuzitumia katika harakati mbali mbali za kiuchumi na hata kuweka uwazi katika suala la mirathi.
Maafisa kutoka Kamisheni ya Ardhi Yussuf Hamad amewataka wananchi wa Kiungoni kuithamini fursa ya kupima ardhi zao na serikali kwani gharama yake ni ndogo ikilinganishwa na kupima mwenyewe.
ANGALIA VIDEO YA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPO CHINI