Thursday, January 16

JAMII INA JUKUMU LA KUWASAIDIA WATOTO YATIMA- MAMA ZAINAB KOMBO

Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Zainab Kombo Shaib, amesema ni jukumu la watu wote ndani ya jamii, kusaidia ipasavyo huduma kwa watoto yatima na wenye mahitaji maalum hapa Zanzibar.
Mama Zainab aliyasema hayo leo alipotembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha Magomeni Wandras mjini Unguja, familia yenye  watoto wanne walemavu iliyopo kiboje Wilaya ya kati na Pongwe Mwera Wilaya ya Magharibi Unguja.
Amesema watoto hao wanamahitaji makubwa yakiwemo ya makaazi chakula,malazi, na mahitaji mengine ya msingi ikiwemo hududuma za elimu, huku familia zao zikikosa uwezo wa kutoa huduma hizo.
Mama Zainab ametoa wito kwa wadau na wanajamii hasa wenye uwezo kutoka ndani na nje ya Tanzania, kujitolea kusaidia ipasavyo mahitaji ya watoto hao ili waweze kupata huduma muhimu za kibinaadamu na waweze kuishi vyema kama binaadamu wengine wote .
Aidha amewahimiza  viongozi mbali mbali kuunga mkono juhudi za serikali na taasisi mbali mbali, kuhakikisha kwamba wanawatembelea watoto wa aina hiyo ili kuona changamoto mbali mbali za mahitaji yao na waweze kuwasaidia.
Mama Zainab alitanabahisha kwamba watoto yatima na wenye mahitaji maalum ni wazi wanamazingira magumu ya kuishi kwa kukosa huduma bora za msingi  na kwamba kupatiwa misaada kutawapa nafuu ya maisha yao.
Akitoa mfano wa familia yenye watoto walemavu wanne  ya huko kiboje Gana, ambao  kwasa wanalala chumba kimoja na mama yao mzazi kutokana na ukosefu wa makaazi, amesema “kuna haja kubwa ya jamii kuiona changamoto hii na kuisaidia familia hii, kwani jambo hili sio zuri hata kimaadili hasa ukilinganisha watoto hawa ni wa kiume na wengine wana umri zaidi ya miaka 25,kulala na mama yao sio busara”.
Aidha Mama Zainab, alitoa wito kwa kila mwenye uwezo, kuguswa moja kwa moja na tatizo hilo na kuhakikisha kwamba wanatoa msaada wa mahitaji  kwa familia za aina hiyo.
Katika ziara hiyo  Mama Zainab alitembelea Kituo cha Faraja kilichopo Magomini wandaras, Familia ya watoto wanne walemavu wa akili ya kiboje pamoja na Familia  yenye mtoto mlemavu huko Mwera Pongwe,  kuwafariji na kutoa misaada mbali mbali  ya chakula, sabuni , mahitaji mengine na fedha taslimu kupitia Jumuiya ya kuwasaidia watoto yatima na wenye mahitaji maalum ya  ZAYOTH.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar