Mhubiri Josephat Gwajima, ambaye pia ni mbunge wa Kawe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa wiki kadhaa sasa amekuwa akipinga hadharani chanjo za Ugonjwa wa Virusi vya Korona (Uviko-19).
Mbunge huyo amekuwa akisema chanjo hizo si salama bila kutoa ushahidi wowote, na kuwahimiza wengine wamfuate.
Waziri wa Afya Dorothy Gwajima alikuwa ameliagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kupambana na Kukabiliana na Rushwa (Takukuru) kumkamata na kumhoji mhubiri huyo athibitishe kauli zake.
Mkuu wa polisi Simon Sirro hata hivyo alisema anahitaji maelekezo kwa njia ya maandishi kutoka kwa waziri.
Awali, Naibu Waziri wa Afya Godwin Mollel alikuwa pia amesema Gwajima huenda akaadhibiwa iwapo hatathibitisha madai yake.
Aliitwa na kufika mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka Jumatatu.
Video zake kwenye YouTube na Instagram zimetazamwa na mamia ya maelfu ya watu mtandaoni. Wanaofuata akaunti zake waliongezeka pia kipindi hicho.
Baadhi ya madai ya Gwajima ni yapi na je, kuna ukweli wowote?
Chanjo ya corona haibadili DNA na kufanya watu mazombi
Askofu Gwajima amekuwa akidai kwamba chanjo za corona zimeundwa kwa kutumia teknolojia ya m-RNA na kwamba zinaweza kubadilisha mfumo wa binadamu.
Amekuwa akidai kwamba chanjo hizo zina uwezo wa kubadilisha msimbojeni au chembe za urithi yaani DNA.
Hakuna ushahidi wowote kwamba chanjo za corona zina uwezo huo. Chanjo hizo hazina chembe hai na hazijifungamanishi na jeni za aliyechanjwa na husambaratika wiki chache baada ya mtu kuchanjwa.
Isitoshe, chanjo zinazotumia teknolojia ya m-RNA ambazo zimeidhinishwa kufikia sasa ni chache – ni Pfizer na Moderna.
Chanjo za Sinovac na Sinopharm zimetengenezwa kwa kudhoofishwa kwa kirusi cha corona, ambayo ni moja ya njia za zamani za kuandaa chanjo.
Chanjo za Johnson & Johnson na AstraZeneca zimetengenezwa kwa kutumia mojawapo ya virusi vinavyosababisha mafua kubeba maelezo ya kirusi cha corona. Huzifanya baadhi ya seli za binadamu kutoa protini zinazofanana na protini za corona na hivyo kuamsha mfumo kinga mwili na kutoa kinga. Virusi vinavyotumiwa vinaitwa Adenovirus na ni aina inayoathiri sokwe mtu. Chanjo ya Sputnik-V imetengenezwa pia kwa kutumia teknolojia hii.
Chanjo ya AstraZeneca, haijaidhinishwa kwa sasa Tanzania lakini inatumika katika nchi nyingi Afrika.
Tarehe 1 Agosti, Gwajima alionekana kuwa radhi kupokea baadhi ya chanjo ambazo kwa kweli ndizo zinazotumia teknolojia ya m-RNA hasa.
Alisema: “tena inapoongezewa inasemwa ni Johnson & Johnson, ndio naona mmm, mtu angesema angalau Moderna [au] Pfizer ningesema ehee, sawa sawa [lakini] J& J? Ah, nakuwa na wasiwasi, na huwezi kunikataza kuwa na wasiwasi.”
Chanjo ya corona haikuzuii kupata corona
Mhubiri huyo amekuwa akipuuzilia mbali umuhimu wa chanjo ya corona kwa kushangaa umuhimu wake iwapo haitamzuia mtu kupata Uviko-19.
“Nimekuuliza, nikichanjwa sitavaa barakoa? Unijibu kwamba utavaa. Sawa sawa, nimekuelewa. Nikichanjwa sitaambukiza? Unaniambia utaamukizwa. Ah, nimekuelewa. Nikichanja sitaambukiza? Utaambukiza. Je, nikichanja, wimbi lingine likija, aina nyingine [ya kirusi] ikija, huyo hatanipata? Atakupata. Sasa, chanjo ya nini?” amekuwa akisema mara kwa mara.
Anaonekana kutoelewa jinsi chanjo za corona zinavyofanya kazi na umuhimu wake.
Chanjo hizo umuhimu wake mkubwa ni kumzuia mtu kulemewa na makali ya virusi hivyo iwapo ataugua na si kwamba inamzuia kuambukizwa.
Mataifa ambayo yamefanikiwa kuwachanja watu kwa wingi yamefanikiwa kupunguzwa idadi ya watu wanaolazwa na kufariki baada ya kupata virusi hivyo.
Na ndiyo maana watu wanashauriwa kuendelea kuchukua tahadhari hata baada ya kuchanjwa.
Chanjo ya corona haikufanyi uwe na sumaku
Mhubiri huyo amedai kwamba watu wanapochanjwa miili yao imekuwa ikishika sumaku. Amedai, bila ushahidi wowote, kwamba kwenye chanjo watu wanawekwa vitu vidogo vidogo visivyoweza kuonekana kwa macho.
“Ndio maana ulikuwa unaona watu wanatushuhudia kwamba nimechanjwa halafu baadaye inashika sumaku. Wewe unajiuliza si ni maji, maji yanashikaje sumaku?” alisema.
“Unashangaa wengine nimechanjwa lakini nawaka taa, kuna vitu vimefanywa vidogo vidogo vidogo vidogo halafu mtu anaingizwa ndani ya mwili vikaudhibiti mwili.”
Madai hayo yanapotosha kwani chanjo zote hakuna chanjo iliyo na chuma inayoweza kumfanya mtu awe na nguvu ya sumaku.
Baadhi ya chanjo zina viwango vidogo sana vya chuma aina ya aluminiamu lakini madini hayo hayana nguvu ya sumaku. Viwango hivyo ni salama kwa mwili.
“Matundu ya sindano zinazotumiwa ni madogo mno, na hata kama ungeweza kumchoma mtu na kitu kilicho na kiwango cha juu sana cha sumaku, kitu hicho kitakuwa kidogo sana kiasi kwamba nguvu zake haziwezi kuifanya sumaku ikanata kwenye ngozi,” anasema Eric Palm, mwanafizikia anayetafiti kuhusu sumaku zenye nguvu.
Anasema ni rahisi sana kuifanya kwa mfano sarafu kunata kwenye mwili wako. Kwa kutumia fizikia kwa kuwa kuna mafuta kwenye ngozi na mvutano wa nafasi pia.
Inawezekana pia kufanya mazingaombwe, ambapo mtu anapaka kitu kama nta au gundi kwenye ngozi kisha kudai mwili wake unanata vitu kama sumaku.
Chanjo hazina vifaa vya kuwafuatilia watu
Katika baadhi ya video, Gwajima amedai kwamba chanjo zina kifaa chenye nambari ya utambulisho ambacho kitatumiwa kiwafuatilia watu.
Alida pia kwamba yupo mtu mmoja mtaalamu wa chanjo ambaye hakumtaja jina aliyemdokezea kwamba chanjo zina kifaa ambacho kwa Kiingereza kinaitwa ‘chip’ ambacho watu wanawekwa na kwamba kitatumiwa kuwadhibiti watu.
“Bado si chanjo, ni kifaa cha kimatibabu. Sio tu kwamba hiyo ni chanjo, ni kitu kinaingia ndani ambacho una nambari maalum ya kwamba huyu wa kwanza huyu wa piliā¦” alisema.
Mtu aliyeugua corona bado anahitaji kuchanjwa
Mhubiri huyo amedai pia kwamba mtu aliyeugua Uviko-19 hahitaji kuchanjwa lakini si kweli kwa mujibu wa wataalamu.
“Kwa sababu tayari umeshaugua na baada ya kuugua, ule mwili wako ukapambana na wale virusi ukajenga kinga kwa hivyo wewe tayari una kinga hutakiwi kuchanjwa,” alisema.
Anasema kwa kawaida mtu akiugua corona na akapona mwili hutengeneza kinga, ambapo ni kweli.
Lakini bado haijulikani kinga hii ya kupatikana kwa njia ya kawaida inadumu kwa kipindi gani na ina uwezo kiasi gani dhidi ya aina mpya za virusi.
Ndio maana wataalamu kwa sasa wanashauri hata waliopata virusi hivyo kuchanjwa.
“Kuna ushahidi unaojitokeza unaoonyesha kwamba watu wanapata kinga bora zaidi kupitia kuchanjwa kikamilifu ukilinganisha na kupata Uviko-19,” kinasema Kituo cha Udhibiti Magonjwa cha Marekani (CDC).
Walio na virusi vya corona hata hivyo wanashauriwa kusubiri hadi wapone kabla ya kupokea chanjo.
Mbona chanjo za corona zimetengenezwa kwa muda mfupi?
Gwajima amekuwa pia akitilia shaka, bila msingi, usalama wa chanjo za corona kwa kuwa zimetengenezwa kwa ‘kipindi kifupi’.
“Chanjo zingine zote zinachukua miaka 10 mpaka 15 ikamilike. Hii ya miezi minne imekamilikaje?” ameuliza.
Yapo mambo kadha ambayo yamechangia chanjo kuandaliwa kwa haraka lakini kasi hii haijaathiri usalama wa chanjo na taratibu zinazofuatwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), baadhi ya sababu hizi ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali na wadau wengine. Rasilimali nyingi zilielekezwa kwa juhudi hizo.
Teknolojia mpya ambazo zimekuwa zikifanyiwa kazi kwa miaka mingi pia zilisaidia kuharakisha shughuli hiyo.
Ingawa wengi wanaweza kudhani ni geni, teknolojia ya m-RNA imefanyiwa kazi kwa miongo kadha. Imejaribiwa katika magonjwa kama Zika, kichaa cha mbwa na mafua. Teknolojia ya kutumia adenovirus ( ambayo ilitumiwa katika Johnson & Johnson na AstraZeneca) imejaribiwa pia kwa kipindi cha karibu miaka 20 hivi iliyopita katika virusi kama vile vya Ebola na SARS ambayo vinakaribiana na virusi vya corona.
Viwango vya juu vya maambukizi viliifanya rahisi kufanya majaribio yake kwenye watu, na pia kulikuwa na ushirikiano mkubwa miongoni mwa watafiti na mamlaka mbalimbali.
Chanjo si ajenda ya mfumo mpya wa dunia
Gwajima amekuwa akidai kwamba sababu halisi ya kuwepo kwa chanjo ni kwamba lipo kundi la watu wanaopanga mfumo mpya wa dunia.
Kwamba mataifa yataangamia na mfumo mpya kuibuka.
“Ili uzae ulimwengu mpya, lazima uwadhibiti wenye akili kwa sababu wenye akili watakupinga. Unapowadhibiti wenye akili, unawaingizia vitu ambavyo mwisho wao baada ya muda mrefu utadhibiti fikira zao,” amekuwa akisema. Kwa fikira zake, anaamini kuna nguvu za giza au shetani ambaye ndiye anayeongoza juhudi hizi.
Nadharia hii imekuwepo kwa kipindi kirefu, lakini kufikia sasa hakuna ushahidi wowote.
Baadhi ya walioanzisha nadharia hii walitumia pia video ya Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau akiwa kwenye Umoja wa Mataifa aliposema kwamba janga hili lilikuwa limetoa fursa ya “kuanza upya”.
Gwajima amedai pia kwamba kila taifa kuu duniani lina chanjo yake kwa kuwa hawaamini chanjo zinazoandaliwa na mataifa mengine. Hilo si kweli kwani yapo mataifa yasiyo na chanjo za corona zinazotengenezewa huko kwa mfano Canada na Ufaransa.
CHANZO CHA HABARI BBC