Thursday, January 16

Skuli ya Wesha yakabidhiwa Tsh milioni 9,000,000/=.

NA ABDI SULEIMAN.

MWAKILISHI wa Kuteuliwa Viti maalumu kupitia wasomi Mkoa wa Kusini Pemba Lela Mohamed Mussa, amekabidhi shilingi Milioni tisa (9,000,000/=) kwa uongozi wa skuli ya Wesha kwa ajili ya ukarabati wa banda moja lenye vyumba vitano vya kusomea wanafunzi skulini hapo.

Banda hilo kwa sasa limekuwa ni mtihani mkubwa kwa wanafunzi kuendelea kusoma, kutokana na kuchimbuka kwa sakafu yake, pamoja na bati kupasuka na kutoboka, hali inayowafanya wanafunzi kuchanganywa kwenye madarasa mengine.

Hafla ya makabidhiano ya Fedha hizo, imefanyika huko katika skuli ya Wesha Wilaya ya Chake Chake, mara baada ya kukagua banda hilo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake katika kuinua sekta ya elimu ndani ya Mkoa huo.

Alisema ubovu wa madarasa hayo yalivyo kwa sasa hayaridhishi, kwa wanafunzi na walimu hivvyo suala la upatikanaji wa elimu bora linaenda sambamba na uwepo wa mazingira bora ya miundombinu madarasa.

“Kiukweli haya madarasa hayako rafiki kwa vijana wetu katika suala la upatikanaji wa elimu, tuangalieni yalivyo chafuka chini na huko juu bati zimetoboka na mvua inaponyesha yote inaishia humu ndani”alisema.

Mwakilishi huyo ambaye pia ni Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, alisema uwepo wa miundombinu bora na salama inapelekea hata wanafunzi kusoma kwa bidii na kuleta mabadiliko makubwa kwa skuli yao.

Akizungumzia suala la changamoto, alisema changamoto zipo nyingi na zitatuliwa kidogo kidogo, kwanza amelazimika kulifanyia ukarabati kwa kuezekwa upya na kutiwa sakafu nyengine na kuwafanya watoto waweze kusoma bila ya matatizo.

Hata hivyo alisema lengo la serikali ni kuona kila mtu anatekeleza majukumu yake kikamilifu, kwa kuhakikisha elimu bora inapatikana.

Mwalimu mkuu wa skuli hiyo Mafunda Soud Saburi, alishukuru kupatiwa msaada huo kwani banda hilo linakaribu miaka 10 sasa, huku wakitumia wanafunzi wa msingi na sekondari kusomea kutokana na uhaba wa vymba kwa skuli hiyo.

Alisema skuli ya Wesha ni miongoni mwa skuli kongwe katika wilaya hiyo, vyumba haviko katika mazingira rafiki hali inayopelekea hata wanafunzi kuwachanganya katika darasa moja.

“Wanafunzi wa darasa la Tatu, sita na kidato cha kwanza wote wanatumia madarasa haya, hali hiyo inaweza kuwasababishia hata maradhi wanafunzi bila ya kujuwa”alisema.

Hata hivyo alisema skuli ya wesha ni miongoni mwa chimbuko la skuli ya Ndagoni, Pondeani na birikau, kutokana na kuanzishwa tokea mwaka 1969, ambapo sasa inawanafunzi 1019 msingi na 339 wanafunzi wa Sekondari.

Akitoa neno la shukurani Sheha wa shehia ya Wesha Haji Mohamed Ali, alimshukuru mwakilishi huyo kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa vitendo katika kuinua sekta ya elimu.

Hata hivyo mwakilishi huyo alipata nafasi ya kuzunbgumza na Kamati ya uokozi shehia ya wesha na kamati ya mazingira shehia hiyo.