NA ABDI SULEIMAN.
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema kuwa inathamini juhudi zilizoonyeshwa na wachezaji wa zamani wa mpira wa miguu Unguja na Pemba, katika kuhakikisha wanaitangaza Zanzibar.
Kauli kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wizara ya habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar Fatma Hamad Rajab, katika hafla ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa Veterani wa Pemba, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa uwanja wa michezo Gombani.
Alisema serikali imedhamiria kuinua viwango vya michezo, hivyo wachezaji hao wanapaswa kusaidia serikali katika hilo, kwa lengo la kuwa na timu moja ya maveterani kwa Zanzibar.
“Kwa sasa tunatarajia kufika kwa wachezaji wa zamani, ili kuona serikali inawathamini sana wachezaji hao, kutokana na mchango wao mkubwa waliouonyesha”alisema.
Aliwataka wachezaji hao kuhakikisha wanavisaidia vilabu vya Zanzibar pamoja na viongozi wao, ili kuona ligi itakayokuja itakua imara zaidi, kwani nia na nguvu zipo katika suala zima la michezo.
Makamu Mwenyekiti wa maveterani wa Pemba Omar Mjaka Ali, alisema tayari wameshacheza michezo mbali mbali ya kirafiki na veteran wenzao, kwa lengo la kuwakumbusha majukumu yao katika kuhakikisha thamani yao inaonekana katika soka la Zanzibar.
Alisema kisiwa cha Pemba kimejaaliwa kuwa na vipaji vingi vya wachezaji mbali mbali, huku akiipongeza Wizara kwa kazi kubwa walioifanya ya kuhakikisha soka la Zanzibar linarudi katika hadhi yake.
Kocha wa timu ya Mavetereni Pemba Hafidhi Muhidini, aliitaka wizara kujipanga kikamilifu kwa kuhakikisha wanaandaa mashindano ya maveterani na kuwathamani kama ilivyo michezo mengine.
Abdalla Ali Kidali aliitaka wizara kuona juhudi zilizochukuliwa na wachezaji wa zamani katika kuitangaza Zanzibar kimichezo kupitia mpira wa miguu.