Wednesday, January 15

Watumiaji dawa za kulevya, makaka, madada poa namna wanavyosambaza Ukimwi.

NA KHAMISUU ABDALLAH

UMASIKINI, kutopata elimu kutokana na wazazi wangu kushindwa kunisomesha ndio imenipelekea kuingia katika kazi hii ya kuuza mwili wangu ili niweze kujipatia pesa kwa ajili ya kuihudumia familia yangu.

Hayo ni maneno ya mmoja wa mwanamke mkaazi wa Morogogoro aliekuja Zanzibar kwa ajili ya kuuza mwili wake.

Eliza Jacson ambae sio jina lake halisi anasema yeye alianza kujiuza akiwa na umri wa miaka 18 baada ya kuondoka kwao kwa ajili ya kuja Zanzibar kutafuta maisha na kuangukia katika kazi hiyo.

Anasema sasa ana umri wa miaka 32 na anaendelea na kazi yake ambayo kwa kiasi kikubwa inamuingizia kipato.

Anasema kwa siku anaweza kufanya kitendo cha mapenzi na wanaumme wasiopungua 10 mpaka 12.

“Mimi kwa siku naweza kufanya mapenzi na wanaumme wasiopungua kumi mpaka 12 kwa wewe utaona wengi lakini kwangu ni kidogo sana na tunakuwa tunamakubaliano maalum akitaka kwa kondom bei inapungua bila ya kondom bei inazidi,” anasema.

Anasema pamoja na kuwa kondom inawalinda kupata maradhi ikiwemo maambukizi ya Virusi vya Ukimwi lakini anavaa kulingana na mteja anavyotaka mwenyewe.

Akizungumzia kupima VVU anasema amekuwa akipima mara kwa mara na mpaka sasa anashukuru bado hajapata maambukizi hayo.

Nae Aisha Suleiman anasema yeye ameanza kufanya biashara hiyo akiwa na umri wa miaka 23 akitokea kwao Kigoma kuja Zanzibar kwa ajili ya kutafuta maisha na alipofika alipata shoga akamwambia ipo biashara ya kuuza mwili na alikubali kwa vile alikuwa hana kazi ya kufanya.

Anasema kazi hiyo kwa kiasi kikubwa imeweza kumpatia faida ikiwemo kujenga nyumba ya kuishi nyumbani kwao wanapotoka, kuhudumia familia na hata kusomesha ndugu zake.

Abeid Haji ambae ni mwanamme anaefanya mapenzi ya jinsia moja anasema yeye alianza kufanya hivyo baada ya kufanyiwa kitendo hicho na mwalimu wake wa chuoni akiwa na umri wa miaka 9.

Anasema mpaka sasa amekuwa amekuwa akiendelea kufanya hivyo pamoja na kuacha mara kwa mara lakini amekuwa akirejea kutokana na kufuata vishawishi,

Anabainisha kuwa mara nyingi amekuwa akitumia kumbi za starehe kwa ajili ya kutafuta watu ili waweze kumfanya kitendo hicho.

“Mara nyingi mimi nakuwa natafuta watu na kuwalipa pesa maana ukishaanza kitendo hichi ni vigumu kuwacha na ninapomaliza tu basi najisikia vizuri,” anasema.

Akizungmzia upimaji wa VVU anasema yeye alipima wakati alipokuwa akiumwa na alipopelekwa hospitali aligundulika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

“Siku nilipoambiwa kuwa na maambukizi nilishituka sana lakini nilipata ushauri nasaha na mpaka sasa nipo na naendelea kutumia dawa,” anabainisha.

Hata hivyo, anasema yeye amepata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kutokana na kunywa pombe za kubakishiwa katika kumbi za starehe na hata akifanya mapenzi alikuwa hatumii kinga ya kondom.

Sambamba na hayo anabainisha kuwa kwa hivi sasa amekuwa akiwaambia wateja wake kuwa na maambukizi na pale anapofanya hitendo hicho amekuwa akitumia kinga kwa lengo la kuwakinga wengine ili asiendelee kuwambukiza.

HISTORIA YA UKIMWI BARANI AFRIKA        

Aidha Tanzania ni miongoni mwa nchi iliyokuwepo katika bara la Afrika ambayo imekubwa na kuwa na maambukizi ya VVU katika jamii inayozunguka.

Ukimwi ni ugonjwa hatari sana katika maisha ya binadamu kwa kuwa husababisha vifo (yaani kupotea kwa uhai wa watu hao) ambapo kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, kufikia mwaka 2014 ugonjwa huu umeua watu milioni 39, hasa kati ya wanaoishi barani Afrika upande wa kusini mwa jangwa la Sahara huku mwaka 2015 pekee wamefariki watu milioni 1.2 na kati yao wengi wao ni watoto.

HISTORIA YA UKIMWI ZANZIBAR

Historia ya visiwa vya Zanzibar inaeleza kuwa ugonjwa huo uligundulika mwaka 1986 ambapo kesi tatu za kwanza ziligundulika katika hospitali ya Rufaa Mnazimmoja.

Baada ya kujitokeza hali hiyo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilichukua hatua ya kuanzisha kitengo maalum cha Ukimwi chini ya Wizara ya Afya na kupewa jukumu la kuhakikisha maradhi hayo yanadhibitiwa hapa Zanzibar na hayawi tatizo katika jamii.

Tume ya Ukimwi ilianzishwa mwaka 2002 kwa lengo la kuratibu shughuli zote zinazohusu Ukimwi.

TUME YA UKIMWI ZANZIBAR

Inaeleza kuwa tafiti mbalimbali zinazofanyika Zanzibar imebainika kuwa vijana wengi ndio wanaoongoza katika maambukizo mapya ya VVU kutokana na kutokubali kubadili tabia zao.

Pia Imeelezwa kuwa vijana hao wamekuwa wakipata maambukizi hayo kutokana na kutotumia ipasavyo huduma za kinga na tiba.

Kwa Zanzibar maeneo yanayoongoza na maambukizi ya VVU kwa Unguja na Mkoa wa Mjini Magharibi na kisiwa cha Pemba ni wilaya ya Wete.

Akizungumza na Mwandishi wa makala haya Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Uhamasishaji na Utetezi kutoka Tume ya Ukimwi Zanzibar, Sihaba Saadat Haji, Saadat, anasema utafiti uliofanyika  unaonesha kuwa wilaya ya mjini inaongoza kwa asilimia 1.1 kutoka na wingi wa watu kuwa na maambukizi ya VVU ikifatiwa na wilaya ya Kati ambayo ina kasi ya maambukizi ya asilimia 1.5.

Anasema kwa upande wa Kaskazini ‘B’ maambukizo yapo kwa asilimia 1.2 huku Kisiwani Pemba yakiwa kwa asilimia 0.5 kutokana na vijana wengi kutokubali kubadili tabia zao na kuendekeza ujana.

Anasema mwaka 2017 kwa Mikoa na Wilaya ya Kisiwa cha Unguja hali ya maambukizi inaonesha kuwa kwa Kaskazini ‘A’ jumla ya watu 12,781 walichunguzwa VVU ambapo kati ya hao 62 waligundulika kuwa na maambukizi sawa na asilimia 0.5 ya wenye VVU.

Kwa Kaskazini ‘B’ anasema watu 7,247 walichunguzwa na 87 waligundulika kuwa na VVU sawa na asilimia 1.2, Mjini waliogunguzwa walikuwa 33,727 ambapo 355 waligundulika kuwa na VVU sawa na asilimia 1.1.

Anafahamisha kuwa kwa Magharibi jumla ya watu 59,920 walichunguzwa ambapo kati ya hao 601 waligundulika kuwa na VVU sawa na asilimia 1.0 huku wilaya ya kati waliochunguzwa walikuwa 10,779 kati ya hao 159 waligundulika kuwa na maambukizo sawa na asilimia 1.5 huku Kusini waliochunguzwa walikuwa 6,012, 62 waligundulika kuwa na VVU sawa na asilimia 1.0.

Kwa kisiwa cha Pemba anasema jumla ya watu 8,856 walichunguzwa katika wilaya ya Wete watu 46 waligunduliwa kuwa VVU sawa na asilimia 0.5 na  Micheweni waliochunguzwa walikuwa 5,009  ambapo 33 waligundulika kuwa na maambukizi sawa na asilimia 0.7.

Katika wilaya ya Chake Chake walichunguzwa walikuwa 9,920 ambapo 55 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU sawa na asilimia 0.6 huku wilaya ya Mkoani waliochunguzwa walikuwa 5,460 ambapo watu 30 waligunduliwa kuwa na maambukizi sawa na asilimia 0.5.

Anasema makundi ambayo yanaathirika zaidi na ugonjwa huo ni makundi maalum ikiwemo kina dada wanaojiuza ambapo wateja wao wanachangia kuleta maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi katika jamii, vijana wanaotumia madawa ya kulevya, wanaumme wanaofanya mapenzi ya jinsia moja na vijana kati ya umri wa miaka 15 hadi 24.

Akizitaja tabia hatarishi kwa vijana Saadat anasema ni pamoja na kufanya mapenzi na watu wegi, kufanya mapenzi kinyume na maumbile huku vijana wenye umri miaka 15- 24 wanafanya mapenzi na wanaume wenye umri mkubwa ambao wengi tayari wana maambukizi  ya VVU.

Tabia nyengine anasema ni wanawake na wasichana wengi wanakosa uwezo wa kushawishi wanaume kutumia kinga salama wakati wa kujamiiana hali ambayo inapelekea kuambukizwa.

Sambamba na hayo anasema mambo yanayochangia vijana kujiingiza katika tabia hatarishi za maambukizi ya VVU ni kutokana na umaskini, shindikizo rika, kuporomoka kwa mila na desturi na tofauti za kijinsia.

Anabainisha kuwa, kwa mujibu wa utafiti unaofanywa kila baada ya miaka miwili kwa mama wajawazito ambapo mwaka 2006 ilikuwa asilimia 0.87  mwaka 2008/ 2010/ 2014 takwimu ilikuwa asilimia 0.6.

Aidha anasema, kwa utafiri wa makundi maalum unaofanywa kila baada ya miaka mitano mwaka 2007 wanaumme wanaofahnya mapenzi jinsia moja walikuwa asilimia 12.3 na mwaka 2012 ilishuka na kufikia asilimia 2.6.

Kwa kinadada wanaojiuza miili yao anasema takwimu ilionesha kuwa mwaka 2017 takwimu zilifikia asilimia 10.8 na mwaka 2012 ilifikia asilimia 19.3 huku kwa watu wanaotumia madawa ya kulevya kwa mwaka 2007 ilikuwa asilimia 16 na mwaka 2012 ilikuwa asilimia 11.3 kiwango ambacho kimeonekana kupanda.

Anasema takwimu hizo zinatoka katika vituo vinavyotoa huduma za upimaji na ushauri nasaha ambapo kwa Zanzibar ina jumla ya vituo 128 vinavyotoa huduma hizo.

Aidha anasema kwa wanawake wanaofanya mapenzi ya jinsia moja pia wamo hatarini kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi lakini huwezi kulinganisha baina ya wanaofanya mapenzi wanaumme kwa wanaumme.

Akitaja maeneo yanayoongoza kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa Zanzibar alisema kwa upande wa visiwa vya Unguja ni Mkoa wa Mjini Magharibi na upande wa kisiwa cha Pemba ni Wete.

Kaimu Saadat, anasema lengo la serikali kupitia tume ya ukimwi Zanzibar ni kuhakikisha ikifikia mwaka 2020 iwe imefikia 90 tatu ambapo asilimia 90 ya watu wanaoishi na virusi vya ukimwi wanajitambua, asilimia hiyo ya wanaoishi na virusi wawe wameanzishiwa dawa, na asilimia 90 wawe virusi vyao vionekane vipo chini wale ambao tayari wameshanzishiwa dawa.

Alifahamisha kuwa, hali ya maambukizi ya VVU kwa Zanzibar ipo chini kwani utafiti uliofanyika mwaka 2015/2016 umeonesha kuwa upo chini ya asilimia moja ambapo ifikapo 2030 Zanzibar haina tena janga la ukimwi na kufikia asilimia 0.

Aidha, anasema kwa Zanzibar kiwango cha watu wanaoishi na virusi vya ukimwi hadi sasa ni kimefikia asilimia 0.4 hadi asilimia 1 kutokana na jitihada mbalimbali zinazochukuliwa ikiwemo kupungua kwa maambukizi na kuweza kudhibitiwa kwa maambukizi mapya huku asilimia hiyo ikionesha kuwa wanawake wanaoambukizwa virusi vya ukimwi ni wengi kuliko wanaumme.

Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo, Ahmed Mohammed Khatib, anafahamisha kuwa kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka 2020 jumla ya wanawake 31,906 wamejitokeza kupima virusi vya Ukimwi kwa Unguja na Pemba.

Anasema kati ya hao Unguja ni 26,133 ambapo 259 sawa na asilimia 0.9 waligundulika kuwa na maambukizi ya VVU huku kisiwani Pemba ni 5,773 kati ya hao 20 waligundulika kuwa na maambuki sawa na asilimia 0.3

Kwa upande wa wanaumme waliopima anasema jumla ni 25,927 kati ya hao Unguja ni 21,445 ambao waligundulika kuwa na virusi vya Ukimwi ni 152 sawa na asilimia 0.7 na Pemba ni 4,482 huku waliogundulika kuwa na maambukizi ni 17 sawa na asilimia 0.4.

Anasema hadi Disemba mwaka jana jumla ya watu 7,020 wanaishi na Virusi vya Ukimwi ambapo uwiano wa wanawake wanaumme wanaoishi na Virusi vya Ukimwi na wanatumia dawa za ARVS kwa wanawake ni 4,774 na wanaumme ni 2,166.

Mkurugenzi huyo anabainisha kuwa asilimia 55 ya wanaumme Zanzibar ndio wanaojua hali zao za maambukizo na asilimia 64 tu ndio wanaojitambua kuishi na VVU na wanatumia dawa.

Hata hivyo anasema kuwa pamoja na jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na ZAC lakini bado changamoto ipo katika makundi maalum kwani maambukizi yapo kwa kiwango kikubwa kutokana na kutokukubali kubadili tabia zao ambapo utafiti wa mwisho imefikia asilimia 11.3.

Sambamba na hayo, alibainisha kuwa bado tume yao itaendelea kuelimisha jamii kujikinga na maambukizi mapya ya VVU na kutoa tiba sahihi kwa wale watakaogundulika kuwa na virusi ya Ukimwi.

KITENGO SHIRIKISHI, HOMA YA INNI, KIFUA KIKUU NA UKOMA

Akizungumza na Zanzibar leo Mratibu wa Huduma za Ukimwi kwa Vijana na Watu wa makudi maalum Zanzibar kutoka Kitengo Shirikishi, Homa ya Ini, Kifua Kikuu na Ukoma Wizara ya Afya Zanzibar Shaaban Hassan Haji anasema Januari hadi Disemba mwaka 2020 jumla dada poa wanaouza miili yao 2,735, wanaumme wanaofanya mapenzi ya jinsia moja ni 1,469 na wanaojidunga 2,149 wamefikiwa katika huduma za HIV, Afya ya uzazi na stadi za maisha kwa Unguja na Pemba.

Anasema kati ya hao dada poa waliopimwa Virusi vya Ukimwi walikuwa 2,470, wanaumme wanaofanya mapenzi ya jinsia moja ni 952 na wanaojidunga ni 1,911 kati ya hao waliokutwa na maambukizi dada poa wanaouza miili yao 87 wanaumme wanaofanya mapenzi ya jinsia moja 25 na wanaojidunga 14 waligundulika kuwa na maambukizo ya Virusi vya Ukimwi.

Sambamba na hayo alibainisha kuwa kwa ujumla jumla makundi maalum waliofikiwa walikuwa 6,353 kati ya hao 5,333 wamepimwa virusi vya Ukimwi na 126 wamegundulika kuwa na maambukizo sawa na asilimia 2.4 kwa Zanzibar.

Hata hivyo anasema kwa wanaotumia madawa za kulevya kwa njia ya kujidunga 90 ya kwanza wapo asilimia 47.5 wanajitambua, 90 ya pili wapo asilimia 88.1 na 90 ya tatu wapo asilimia 97.6.

Kwa upande wa wanawake wanaokodisha miili yao anasema wapo asilimia 72.5 wanajitambua, waliokuwa wanatumia dawa ni asilimia 94.3 na 90 ya tatu wapo asilimia 87.0 huku kwa upande wanaumme wanaofanya mapenzi ya jinsia moja ni asilimia 59.7 wamajitambua, asilimia 92.9 wapo kwenye dawa na 90 ya tatu wapo asilimia 97.9.

Anafahamisha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya kwa makundi maalum na jamii kwa ujumla ikiwemo wanaumme katika kuhakikisha wanapima Virusi vya Ukimwi ili kupambana na maradhi hayo yasiendelee kuambukiza.