Spika wa Baraza la Wawakilishi mhe Zubeir Ali Maulid akiwaongoza Waheshimiwa wawakilishi katika kufanyia mazoezi ya matumizi ya tablets katika kuelekea baraza mtandao, mfumo ambao unatarajiwa kuanza kutumika kuanzia katika Mkutano wa nne wa baraza la wawakilishi unaotarajiwa kuanza Septemba.
Mwanasheria mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dr Mwinyi Talib Haji wakijadiliana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Dr Khalid Salum Mohammed kuhusu mfumo mpya wa Baraza mtandao.
Na Massoud Hamad, BLW
Baraza la Wawakilishi linatarajiwa kuanza kutumia mfumo wa baraza mtandao kupitia tablet katika shughuli za uendeshaji wa vikao vya baraza na kazi za kamati kuanzia mkutano wa nne wa baraza la kumi unaotarajiwa kuanza mwezi Septemba.
Hatua hiyo imekuja baada ya kukamilika taratibu zote za makabidhiano ya Tablet hizo yaliyoambatana na mafunzo ya utumiaji wake yaliyofanyika Chukwani.
Akizungumza wakati akifungua mafunzo hayo Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe Zubeir Ali Maulid amefahamisha kuwa matumizi ya mtandao katika kuongoza Baraza yatasaidia kuokoa gharama kubwa ambayo ilikua ikitumika katika matumizi ya nyaraka za karatasi.
Akikabidhi Tablets hizo Katibu wa Baraza la Wawakilishi Raya Issa Msellem amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa matumizi ya karatasi katika shughuli za Baraza na kuwarahishia Waheshimiwa Wawakilishi kupata nyaraka zote mbali mbali kwa njia ya mtandao kupitia tablets zao.
Nao Waheshimiwa wameipongeza hatua ya ofisi ya Baraza la Wawakilishi kuwapatia Tablets huku wakisema kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa vitendo maelekezo ya Mhe Rais katika kuimarisha mifumo ya kisasa ya kidigitali wakati akizindua Baraza la kumi la Wawakilishi ambapo unalenga kurahisisha shughuli zao.