Friday, January 17

Dkt Mwinyi, awatoa hofu wananchi wa Wilaya ya Micheweni kuhusu ahadi zake.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi akizungumza na wakulima wa mwani pamoja na wavuvi eneo la Shirikani wilaya ya Micheweni ikiwa ni sehemu ya ziara ya siku 4 kiswani Pemba

MWANDISHI WETU

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekitiwa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dkt, Hussein Ali Mwinyi, amewatowa hofu wananchi wa Wilaya ya Micheweni Pemba, kwa kusema kuwa yale yote aliyowaahidi katika kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa 2020-2025 atayatekeleza hatuwa baada ya hatuwa.

Aliyasema hayo huko katika kijiji cha Kiuyu Mbuyuni Wilaya ya Micheweni mara baada ya kupokea malalamiko mbali mbali ya wananchi hao ikiwemo kilimo cha mwani na kuwa anatambuwa tatizo walilonalo wakulima wa mwani  kutokana na kazi hiyo kuwa kubwa lakini kipato chao ni kidogo.

Dk, Mwinyi alifahamisha kuwa lipo katika maeneo matatu Elimu ya upandaji lazima wakulima wafundishwe vyema, mbegu yenyewe ijuilikane yenye thamani kubwa ndio waitumie, mtaji kwa wakulima kwani wakulima hawana fedha za kufanyia kazi ili waweze kupata tija, Soko la kuuzia mwani hakuna .

Alisema hali hiyo matokeo yake wanakuja watu wanataka wawauzie kwa bei ya Shilingi 500 , hayo hayakubaliki  kwakweli , ahadi ni kwamba Serikali italisimamia jambo hilo kwa kutafuta  mitaji kwa wakulima hao pia na soko zuri ambalo litatowa bei ya haki.

Alieleza kuwa ilikuwa Serikali inakusudia kujenga Kiwanda ambacho kitasarifu mwani ili bei iongezeke na kuwainuwa wakulima , kutokana na matatizo aliyaambiwa yapo  ZSTC na bado  hayajakamilika jambo ambalo
haliridhishi hata kidogo lakini aliwahakikishia Wananchi bado Azma hiyo kwa Serikali ipo pale pale.

Dkt, Mwinyi aliwahakikishia wakulima wa Mwani kuwa Serikali bado inatafuta  njia ya kuleta mageuzi ya Kilimo hicho kwa kujenga Kiwanda katika eneo hilo ili waweze kuuza mwani kwa  bei mzuri ,kwani nia ya Serikali ni kuona wananchi wake wanaondokana na hali ya Umaskini.

Akizungumzia shughuli za uvuvi alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, itaendelea kufanya mpango wa kuwakomboa na umaskini kutokana na sekta hiyo kwa kuwapatia vifaa vya kisasa sambamba na kuwatafutia soko la
uhakika kwa kuwanzishia Viwanda vya kuchakata Samaki ili kupata maslahi mazuri na kupatikana ajira kwa wananchi.

“ Tayari tumeshafanya mazungumzo na wawekezaji wa kujenga kiwanda cha Boti katika eneo hilo kwa ajili ya kuwapatia Wavuvi  sambamba na kujenga kiwanda cha kuchakata mwani jambo ambalo litatowa ajira kwa wananchi wetu,”alisema.

Alifahamisha kuwa haiwezekani hadi sasa wavuvi waendelee kuvua katika njia za kienyeji hali ambayo inatowa kipato kidogo , lazima kuwepo na uvuvi wa kitaalamu  ili tija zaidi iweze kupatikana kwa faida ya wananchi wote na kupata fedha za kujikimu.

Alisema ni lengo la Serikali  la kuwataka wavuvi wajikusanye  vikundi na kupatiwa zana za kisasa za uvuvi  ili wafike katika bahari kuu na kuvua kwa na kupatiwa Soko,kupata kipato kikubwa kwani uvuvi wa sasahivi wa kupata samaki kilo mbili mbili hautowi tija kwa wavuvi hao.

“ Nawaomba Wavuvi kuwa watulivu  na wavulimivu wakati mipango hii ikiendelea kutekelezwa ili tuweze kupata viwanda vya uhakika ili tuwawezeshe wananchi wetu kwa zana za kisasa, tunatambuwa kuna akinamama wanajishuhulisha na kimo cha mwani lazima nao usarifiwe hapa ili tupate bei mzuri,”alisema.

Akizungumzia changamoto za Elimu Dkt, Mwinyi alisema  Serikali inazielewa ikiwemo uhaba wa madarasa machache, matundu ya Vyoo na uhaba wa Walimu lakini kila jambo lina mipango sio kuwa kila jambo litatekelezwa mara moja Serikali ina mipango maalumu na muda  wa uendelezaji wa Elimu ya msingi  na Sekondari  ikiwa lengo na madhumuni ni kujenga madarasa mengi zaidi.

Alisema anajuwa ili elimu iwebora kila darasa liwe na watoto sio zaidi ya wanafunzi 45,kuwepo madarasa manane kwa wanafunzi zaidi 2000 bila shaka hapo elimu itakuwa duni Serikali inatambuwa na inajipanga kuwa na mpango maalumu wa kujenga matundu ya Vyoo , madarasa  na kuajiri walimu wakiwemo wa Hisabati na Sayansi.

“ Habari nilizozipata ni kwamba Wizara ya Elimu imepata mfadhili kutoa Qatar ikishirikiana na UNICEF watakuja kukamilisha madarasa 100 kutoka yale yalioanzwa na wananchi na Serikali inajipanaga hata kwa kutafuta mikopo ili tuweze kukamilisha azma hiyo,”alisema.

Hata hivyo Dkt, Mwinyi aliwashukuru Walimu mbali mbali wanaojitolea kwa miaka mingi  maskulini kwani kila anapopita anawaona walimu hao hivyo ametowa agizo pale Wizara itapotowa ajira wawazingatie kwanza wale walimu wanaojitolea katika maskuli yao.

Alisema ameshapata kilio kuwa zinapotokea ajira wale wanaojitolea huachwa  na kuchukuliwa wengine hii  iwe marufuku wale wanaojitolea wachuliwe mwanzo haifai kuwaacha hao wakachukuliwa wengine kulikuwa na changamoto za kielimu baada ya kuwa na ugatuzi lakini Halmashauri hazikuwa na uwezo .

Alifahamisha Halmashauri zilitegemewa zijenge madarasa, Vyoo, ifanye mambo mengi yanayohusu Elimu, kilimo na Afya na kunataarifa kuwa fedha zinazokwenda kwa miradi ya wananchi ni asilimia 15 kutoka Halmashaur na ndio ikaamuliwa Elimu irudi Serikali kuu.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Dkt , Hussein Ali Mwinyi aliagiza kushirikishwa wananchi na kushiriki  katika shughuli zote za kimaendeleo sambamba na kulipwa fidia pale wanapoharibikiwa na raslimali zao panapopita miundo mbinu ya maendeleo.

“ Nawaomba wananchi muwe tayari kutowa maeneo yenu pale ambapo yanahitajika kupitishwa miundombinu ya maendeleo kwani linalofanyika hapo ni kwa maendeleo yenu wenyewe,”alisema.

Kwa upande wa ajira alieleza bado ni changamoto hasa za Serikali , lakini Serikali itaendelea kuwahamasisha wawekezaji kusaidia upatikanaji wa ajira binafsi kutokana na kuekeza viwanda vya aina tafauti tafauti ili .

Hata hivyo aliagiza pale zinapotoka ajira basi izingatiwe wale ambao wanajitolea katika taasisi husika kwanza ndio zitolewe kwa watu ambao hawajitolea kwani hali hiyo itaondosha malalamiko kwa wananchi.

Alisema  ili tatizo la ajira liweze kuondoka nilazima kuwe na Viwanda vya aina mbali mbali ili viweze kutoa ajira na kuondokana na wimbi kubwa la kusubiri ajira kutoka Serikalini ambazo ni chache lakini kukiwa na viwanda ajira nyingi zitapatikana.

Sambamba na hayo alisema, hakuna haja kwa wananchi kuwa na wasi wasi wa kumalizika kwa barabara ya micheweni kwani hivi sasa anafanya mazungumzo na kampuni ya kuwapatia mkopo wa kujenga barabara kilomita 220 Unguja na Pemba.

“Na katika mkopo huo na barabara hii imo kwa hio nataka kukuhakikishieni kwamba ujenzi wa barabara ndio kuleta maendeleo kwani wale wenye mazao yao hapa na ardhi zao musiwe na wasi wasi ninachoagiza kila mwenye stahiki alipwe fidia yake” alisema.

Alisema, Serikali ya awamu ya nane jambo ambalo imefanikiwa ni kudumisha amani upendo na mshikamano hivyo, aliwataka wananchi wote kuendelea kudumisha na kuhubiri amani na umoja ili kuweza kuleta maendeleo ndani ya nchi yao.

Akizungumzia suala la Afya alisema, haifai wananchi kuwepo Micheweni lakini wanapoumwa kupelekwa sehemu nyengine hivyo, aliagiza Wizara ya Afya kumrejesha Daktari wa upasuaji aliekuepo hospitali ya Micheweni
ama kutafuta mwengine ambae atakuepo kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

Adha Dkt, Mwinyi aliwaagiza viongozi wa ngazi zote ikiwemo Madiwani, Mkuu wa Mkoa, Wilaya, Wabunge na Wawakilishi wanapotaka kufanya shughuli zote za kimaendeleo kuwashirikisha wananchi ili kufanikisha shughuli zao.

Wakati huo huo Rais Mwinyi ameipandisha hadhi Hospitali ya Micheweni Pemba kuwa Hospitali ya Wilaya kutoka Hospitali ya kawaida.

Mapema akiwa katika ziara hiyo alipokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo  za mkoa  wa Kaskazini Pemba kuanzia July 2020 hadi july 2021 iliosomwa na mkuu wa mkoa huo Salama Mbarouk Khatib.

Salama , akisoma ripoti hiyo alisema mkoa huo umefanikiwa kwa asilimia 79.5 katika maendeleo kwani wananchi wake wameondokana na chuki na uhasama na wanashirikiana pamoja katika harakati za kuuletea maendeleo
mkoa huo.

Alizitaja shughuli zinazowapatia kipato wananchi wa mkoa huo ni Kilimo, uvuvi,Karafuu , Mwani na kusema kwamba bado yanaathiri mashamba ya wakulima wampunga na kusema kwamba mabadiliko  hayo yanaathiri  wakulima .Alieleza kuwa mbali na mafanikio walioyapata katika kipindi hicho pia ukosefu wa wataalamu ni tatizi kubwa ambalo linarejesha nyuma maendeleo ya Wakulima na hivyo kukosa mavuno tarajiwa.

Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa wananchi wa mkoa huo wanaiomba Serikali kuharakisha na kumaliza ujenzi wa kiwanda cha kusarifu  Mwani kwani wanayo mategemeo makubwa ya kuongezeka kwa bei ya zao hilo ambayo wananchi itawakombowa kiuchumi kutokana na kwamba asilimia kubwa wamejiingiza katika kilimo hicho.

Hata hivyo  alieleza Wananchi wa mkoa huo wanamuomba Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk, Hussein Ali Mwinyi kuwainuwa wajasiria mali ili mkoa huo upate maendeleo zaidi yatakayo wainuwa
kiuchumi.