Katika mashamba makubwa ya Cox’s Bazar Bangladesh ndipo eneo ambalo FASO imeweka mtambo wake wa nishati ya jua au sola kwa ajili ya kumwagilia mashamba hayo, kwa muda mrefu wakulima katika eneo hili wamekuwa wakitumia miatambo isiyo bora ambayo ilikuwa ikitumia mafuta kisukuku ambayo sio tu ilikuwa ikiharibu mazingira na kuchangia mabadiliko ya tabianchi bali pia iliathiri maisha ya wakulima.
Lakini sasa FAO kwa kushirikiana na wakulima kuboresha mifumo ya umwagiliaji na uzalishaji wa mazo kwa kutumia mitambo hii mipya ambayo itasaidia kuondoa tatizo la uhaba wa maji, kuongeza uzalishaji wa chakula na kuokoa gharama za nishati kwani inatumia jua badala ya mafuta. Mohammad Islam baba wa watoto watatu na mkulima wa biringanya, kabichi na na maharage ni miongoni mwa wakulima walionufaidika kwa kuwekewa mtambo mpya ya umwagiliaji kutoka FAO
“Hapo kabla tulikuwa tunaacha ardhi kubwa ya shamba bila kulimwa kwani haikuwezekana kulima mbogamboga na mpunga, sasa kwa mitambo ya umwagiliaji ya sola tumeanza kulima katika ardhi hizo tena.”
Kwa mujibu wa afisa wa FAO mitambo hii ya kutumia nishati ya jua ni ya kuaminika, n ani ya gharama nafuu hususan vijijini ambako gharama ya mafuta kisukuku ni kubwa kwa wakulima wengi kumudu. Rajib Mahamud ni afisa mtaalam wa misitu wa FAO Cox’s Bazar, “Hapa, tumetumia mfumo wa umwagiliaji wa nishati ya jua ambao umejumuishwa na bomba lililofukiwa. Kwa hivyo, lengo lilikuwa kutumia umwagiliaji wa nishati ya jua ili kupunguza utegemezi wa mfumo wa kawaida ambao unategemea pampu za mafuta ya kisukuku na unachangia mabadiliko ya tabianchi na uzalishaji wa hewa ukaa. ”
Ameongeza kuwa mitambo mingine saba ya umwagiliaji itaanza kufanyakazi hivi karibuni na kila mtambo unauwezo wa kumwagilia ekari 50 na kuwanufaisha wakulima 100, na kwa sasa umeanza Cox’s Bazar lakini lengo ni kuwafikia wakulima wa nchi nzima Bangladesh.