Ufunguzi wa michezo ya Olimpiki ya Walemavu Tokyo 2020 siku ya Jumanne itaadhimisha miaka 60 (kinadharia 61 kutokana na janga la corona) tangu michezo hiyo ilipozinduliwa kwa wachezaji mahiri na kusaidia kuleta mabadiliko halisi kwa watu wenye ulemavu.
Huku maandalizi ya michezo hiyo ikiendelea, BBC ilizungumza na washindani kutoka maeneo tofauti duniani na ambao waliwakilisha nchi zao kwa kiwango cha juu zaidi kwa miongo kadhaa.
Kubadilisha maisha
CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
“Nadhani [michezo ya olimpiki ya walemavu] ilipata ufanisi mkubwa, iliwaleta pamoja watu kutoka kila pembe ya ulimwengu hatua ambayo haikuwa ikifanyika mbeleni,” anasema Baroness Masham wa Ilton, ambaye aliiwakilisha Uingereza katika Michezo ya kwanza ya Olimpiki ya walemavu mjini Rome mwaka 1960.
“Nadhani wamefanya tofauti kubwa.”
Kufuatia ajali ya kuanguka kutoka kwa farasi mwaka 1958 iliyomfanya kutumia kiti cha magurudumu, alitibiwa na na mtu ambaye alimsaidia kupata michezo ya Olimpiki ya Walemavu, Dkt Ludwig Guttmann.
“Mtu alipojipata kwenye kiti cha magurudumu, michezo ilikuwa sehemu ya uponaji,” anasema. “Ilikuwa sehemu ya maisha. Ilikuwa sehemu ya mfumo wake.”
Dkt Guttmann alianzisha michezo ya Stoke Mandeville nchini Uingereza (ilipewa jina la hospitali ambapo ilikuwa ikitibu tatizo la uti wa mgongo) baadaye michezo hiyo ilibadilishwa kuwa Michezo ya Olimpiki ya watu wenye ulemavu
Kwa Baroness Masham, ambaye alikuwa anapenda michezo hata kabla ya kupata ajali, kushiriki katika michezo ya kwanza ilikuwa fursa ya kusisimua.
“Kushiriki ilikuwa jambo zuri, lakini ilikuwa raha zaidi kwamba ilikuwa ya kimataifa,” anasema. “Nilipendelea sana kukutana na watu kutoka sehemu tofauti duniani.”
Kukosa medali
Zama zake katika michezo ya Olimpiki ya walemavu mjini Rome, na kisha michezo iliyofuata ya Tokyo na Tel Aviv, alipata ufanisi mkubwa – kushinda medali za kuogelea na tennisi ya kwenye meza, ijapokuwa sio zote zilifika nyumbani.
“Tulikwenda kwenye mkahawa karibu na Chemichemi ya Trevi huko Roma,” alisema.
“Mtu fulani aliomba kuona medali zangu, nikamuonesha na baadaye nikaziweka kando ya kiti changu cha magurudumu, kwa bahati mbaya moja ya dhahabu ikaanguka na kupotea.”
Chombo kimoja cha habari katika eneo hilo kilipata taarifa hiyo na kusisimuliwa sana maelezo (yasio sahihi) ya tukio hilo na kusema kwamba alitupa makusudi medali yake katika chemi chemi hiyo maarufu.
“Ukweli ni kwamba si kufanya hivyo, lakini sikupewa nyingine,” aliongeza kusema. “Niliudhika sana.”
Kuvuka mipaka
CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Kushindana katika mashindano ya Olimpiki pia ini jambo ambalo lilikuwa na athari kubwa kwa maisha ya Anne Wafula Strike.
“Kwangu mimi michezo ilinipatia mwanzo mpya maishani.”
Alianza kutumia kiti cha magurudumu tangu alipopata ugonjwa wa kupooza yani polio akiwa mtoto mdogo, lakini alianza kushiriki katika michezo akiwa na miaka 30.
“Michezo iliniwezesha kujitambua tena – Naweza kuwa uwanjani, katika ukumbi wa mazoezi, na kutangamana na wengine ambao hawana ulemavu. Nilihisi kuwa sawa na kujistahi kwangu kulianza kukua. “
Anne aliiwakilisha Kenya katika Michezo ya mwaka 2004 mjini Athens.
Cha kushangaza, licha ya eneo la Afrika Mashariki kupata ufanisi mkubwa katika riadha alikuwa mtu wa kwanza kushiriki mbio za kutumia kiti cha magurudumu kutoka eneo hilo kushindana katika michezo ya Olimpiki.
“Nilikuwa katika mazingira ya ulemavu na watu katika kijiji chetu walinitenga”.
“Kutoka kutengwa na jamii hadi kusimama kwenye jukwaa na kupeperusha bendera – Hiyo ndio nguvu ya michezo.”
Anne pia aliiwakilisha Uingereza katika mashindano ya kimataifa, ambako alianza michezo hiyo na kuhamia baada ya kuolewa.
Lakini huko pia amesikitishwa juu ya kasi ya mabadiliko kwa watu wenye ulemavu – alipokea fidia kufuatia kesi maarufu dhidi ya kampuni ya treni ya Uingereza kwa ukosefu wa upatikanaji wa choo cha walemavu kwenye treni.
“Ninafadhaika wakati taifa lililoendelea haliongozi ulimwengu ipasavyo.”
Baada ya kubadili mkondo kutoka uwanjani amefanya kazi kama mkurugezi wa Riadha wa Uingereza na pia kama mwanaharakati wa kupigania haki michezoni kwa wachezaji wa Jumuia ya Madola, na kutunukiwa tuzo ya MBE.
“Mimi ndiye mtu wa kwanza mweusi kwenye bodi ya michezo inayofadhiliwa kitaifa [nchini Uingereza] na hiyo inakuonyesha wazi jamii iko wapi na jinsi tunavyohitaji kujinyanyua.”
Kutoka vitani hadi michezoni
CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Murlikant Petkar alikuwa mwanariadha mwanzilishi wa nchi tofauti – India.
“Kuwa mpokeaji wa nishani ya kwanza ya dhahabu katika mashindano ya Paralimpiki ilikuwa wakati wa furaha zaidi na ambayo haitasahaulika maishani mwangu,” anasema.
Murlikant alijeruhiwa vibaya katika shambulio la angani wakati wa Vita vya mwaka 1965 kati ya India na Pakistan. Hatua yake ya kuamua kuogelea kulileta mabadiliko makubwa kuelekea uponaji wake.
Ndio, kuwa mtu mlemavu mwanzoni ilikuwa sehemu ya kukatisha tamaa na kusikitisha sana maishani mwangu, ambayo nilichagua kuiacha wakati nilipofahamu nafasi yangu kama mwanariadha kwangu na kwa taifa langu.
“Kama nisingecheza kwenye Michezo ya Walemavu nilingekuwa nimezongwa na majonzi ya kutoweza kufanya chochote.”
Kutokana na mafanikio yake, ambayo pia yalijumuisha kushindana kwenye Michezo ya mwaka 1968, Murlikant alipewa tuzo ya Padma Shri na India – moja ya heshima kubwa zaidi nchini.
Anadhani wanariadha wengi wa India watapata ufanisi katika mashindano ya Tokyo.
Kufanya mabadiliko
Washiriki wote wanatazamia michezo ya Olimpiki ya Walemavu mjini Tokyo, ambayo yaliahirishwa kutokana na janga la Corona.
“Nashukuru michezo hii inafanyika, kwa sababu ya maandalizi na mazoezi iliyofanyika – Natumai kila kitu kitaenda sawa,” anasema Baroness Masham.
Anne pia anafarijika kuwa baada ya hali sintofahamu iliyokuwepo hatimaye Michezo ya Olimpiki ya Walemavu itaendelea Jumanne kama ilivyopangwa.
“Nafurahi sana Michezo hii itafanyika. Hebu tafakari hali ya wanariadha walifanya mazoezi kwa miaka kadha?
Anaamini wachezaji wako tayari kukabiliana na changamoto zote ili kufikia malengo yao.
“Wakati kila mtu anahisi kuwekwa majaribuni sisi tunaoishi na ulemavu tunategemea uwezo wetu wa kuhimili changamoto zinazotukabili, na tunafanya hivyo kwa sababu tuna vizingiti vingi vilivyowekwa mbele yetu.