NA ZUHURA JUMA, PEMBA.
“UONGOZI ni heshima, ikiwa unajielewa huwezi kwenda kinyume na heshima uliyopewa na watu”, ni maneno ya Aisha Hussein Abdalla mwenye miaka 29 mkaazi wa shehia ya Mtemani Wete.
Ni Makamo Mwenyekiti Baraza la Vijana Wilaya ya Wete, aliejipatia nafasi hiyo katika kinyang’anyiro cha kuwania uongozi katika uchaguzi ulifanyika mwaka huu.
Mshindani mwenzake Aisha katika nafasi hiyo ya Makamo Mwenyekiti alikuwa mwanaume, inagawa alipata nafasi ya pili kwa kura 17 kati ya kura 44.
Nafasi ya kwanza alichukua mwanaume kwa kupata kura 23, lakini kutokana na Katiba yao inavyoeleza, Aisha alibahatika kushika nafasi hiyo.
“Katiba yetu inatoa ulazima kwamba, Mwenyekiti akiwa mwanaume, Makamo wake awe mwanamke hata kama ameshindwa kwa kura”, anasimulia.
Amewahi kugombea nafasi mbali mbali za uongozi, ingawa ya na Makamo Mwenyekiti ndio ya kwanza aliyofanikiwa kuipata.
Ni msichana ambae alijiamini na kusimama kidete katika kuhakikisha anakuwa kiongozi na kuweza kuzitatua changamoto bila ubaguzi.
“Sikukata tamaa kwa sababu niligombea mara ya kwanza nikakosa, mara ya pili pia nikakosa na hii niliyofanikiwa ni mara ya tatu, hivyo nilijiwekea matumaini ya kwamba ipo siku nitafanikiwa”, anasimulia msichana huyo.
KIPI KILICHOMVUTIA AISHA KUWA KIONGOZI?
Wakati akiwa msichana mdogo sana alikuwa anasikia kwamba kwenye uongozi hakuna uadilifu na kwamba mtu akishapata hawezi kusaidia wengine.
Alikuwa anasikia kwamba, kinachotendeka huko ni rushwa, kukosekana kwa uadilifu na ndio maana aliamua kupigania, ili kuhakikisha anaingia kwenye uongozi, kwa lengo la kuondoa mambo ambayo hurudisha nyuma maendeleo.
Anajisemea kuwa, yeye anaweza kuongoza pasipo kufanya mambo mabaya ambayo alikuwa akiyasikia.
Tayari sasa ameonyesha hilo kwa vitendo, kwani amekuwa akiongoza kwa uadilifu, uwazi na anaependa mashirikiano kwa wale anaowasimamia na jamii iliyomzunguka.
“Uongozi ni dhima na tutakwenda kuulizwa mbele ya Mwenyezi Mungu jinsi tulivyoitekeleza dhima hiyo, kwa hiyo ni lazima tusimamie watu kwa uwadilifu na uwazi”, anasema Makamo huyo.
Kichomsukuma Aisha kuwa kiongozi ni kuwasaidia vijana, jamii na wanawake wengine ambao wanasita kugombea nafasi za uongozi, kwamba inawezekana.
Makamo Mwenyekiti huyo anaamini kuwa, mwanamke anapokuwa kiongozi ni mfano bora wa kuihamasisha jamii, hivyo wasibaki nyuma.
KITU ANACHOKIFANYA KWA SASA AKIWA MAKAMO
Anawashawishi vijana kuanzisha miradi ya kimaendeleo kwa lengo la kujikomboa kiuchumi na kwa sasa linaonekana ndani ya jamii, kwani vijana wengi ni wajasiriamali.
Wanatengeneza miradi mbali mbali kupitia Serikalini, ili kuwapa msukumo vijana waweze kukidhi mahitaji yao ya kila siku na kuepuka kujiingiza katika makundi hatarishi.
Anasimamia majukumu aliyopewa kwa uwadilifu, kushirikiana na anaowasimamia kwa lengo la kuleta ufanisi zaidi katika kazi zao.
MIKAKATI YAKE NI IPI KWA VIJANA?
Kuhakikisha amani, umoja na mshikamano kuhakikisha unadumu, ili kupata maendeleo.
Atahakikisha vijana wanafikia malengo waliyojiwekea sambamba na kuwapatia elimu ya mambo mbali mbali yaliyomo ndani ya jamii.
“Tutahakikisha wanakuwa vijana wazuri watakafanya kazi za halali na kuepukana kujiingiza katika makundi hatarishi ya madawa ya kulevya na udhalilishaji”, anasefahamisha.
Anaeleza kuwa, hawatafumbia macho na baraza haliko tayari kuwa pamoja nae, yeyote ambaye atafanya mambo mabaya katika jamii.
JE UKIWA KIONGOZI KITU GANI NI MUHIMU?
Aisha anasema, ile kufikia kuitwa kiongozi, tayari kuna heshima inayojengeka, hivyo ni vyema viongozi wasiende kinyume na heshima wanayoipata.
“Ikiwa unajielewa huwezi kwenda kinyume, kwa sababu kila wakati unajua kuwa, jamii unayoisimamia inakuamini na inakutegemea, hivyo ni vizuri kujiheshimu”, anaelezea.
“Unaweza kujiuliza nikifanya hivi je nitaleta taaswira gani kwa jamii iliyonizunguka?, hivyo mara nyingi utajikinga na aibu na kashfa”, anasema.
Jambo lolote unalotaka kulifanya ni vyema kumtanguliza mungu kwanza na usilazimishe matakwa yako binafsi, kwani yatakugharimu na hatiame utaingia katika dimbwi la maovu.
“Unapoamua kufanya jambo lako, usilazimishe matakwa yako yasiwe sawa sawa na anavyotaka Mungu, kwani hutofikia mbele.
Anafahamisha, ikiwa mtu atajidhalilisha kwa lengo la kupata uongozi au kitu chengine asitarajie kuheshimiwa, kwani tayari ameshavunja maadili.
CHANGAMOTO ALIZOKUMBANA NAZO WAKATI WA KUSAKA UONGOZI
Mwanzo alipoanza kuingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania uongozi, jamii ilimuona hafai na wala hawezi, hivyo ilikuwa ni vigumu kumkubali, ingawa kwa sasa wanamuaminia.
“Kwa sasa wananikubali ile mbaya, hasa kwa vile nimewaonyesha ujasiri wangu na sikuwahi kurudi nyuma licha ya vikwazo vilivyokuwa vikinikabili”, anasema.
Hata wazazi wake walimchukulia kwamba hawezi kupambana, ingawa baada ya kuona zile jitihada zake, wakaamini kwamba anaweza kufika pale alipopakusudia.
Anasema, wakati unapotaka kugombea wajumbe wanashindwa kukufahamu pale unapojielezea, lakini hiyo ni kwamba wanakuwa na mtazamo hasi.
“Wanahisi atakaekuja ndo wale wale ambao sio waadilifu, dhamira yangu ni kuwasaidia vijana, kwani unapomtengeneza kijana unatengeneza Taifa bora zaidi”, anasema.
Changamoto nyengine ni kwamba anaangaliwa mtu anapotoka na sio yeye mwenyewe, jambo ambalo linaweza kuwa kikwazo kwa mwanamke mwenye nia ya kugombea.
ANA WITO GANI KWA WANAWAKE, VIJANA NA JAMII
Wanapogombea wasienende kinyume na maamrisho ya dini, silka na tamaduni za nchi sambamba na kujali familia na waume zao.
Anawataka wanawake wenzake wasikate tamaa, waendelee kuingia majimboni kusaka uongozi, kwani hiyo ni haki yao kikatiba na kisheria.
“Kila mmoja anapopewa uongozi ajue kwamba amepewa jukumu zito, hivyo afanye uadilifu, awe muwazi, muwajibikaji na ashirikiane na watu wake, ili kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi”, anafahamisha.
Makamo Mwenyekiti huyo anasema ni vyema mtu akipata nafasi ya kuongoza, ajilinde na ajiheshimu, kwani hayo mambo ni ya kupita, ila utu na heshima yako itabaki.
Anawashauri wanawake wenzake kujiamini na kujua kwamba wanaweza pasipo kukiuka maadili katika jamii, ili kuepuka kujishusha thamani.
AISHA NI NANI
Ni msichana wa miaka 29 mwenye elimu ya Diploma ya Usimamizi wa Kumbu Kumbu na Nyaraka aliyoipata kwenye chuo cha Utawala wa Umma (IPA) katika tawi lake lililopo Chake Chake Pemba.
Alipata elimu ya msingi katika skuli ya Jadida Wete na kumalizia Sekondari katika skuli ya Ufundi Kengeja Wilaya ya Mkoani Pemba.
Aisha ni mtoto wa mwisho kuzaliwa katika familia ya watoto sita, ambapo bado hajaolewa.
Uongozi ni ndoto yake Aisha tangu akiwa skuli, kwani aliwahi kuongoza kwenye Serikali ya wanafunzi na hatimae sasa anaongoza vijana wa Wilaya.
WATU WA KARIBU WANAMZUNGUMZIAJE?
Maryam Ali Rashid mkaazi wa Kisiwani kwa Binti Abeid Pemba anamuelezea Aisha kuwa, ni mzalendo na anajitahidi kwenye masuala ya uongozi.
“Ameshagombea nafasi mbali mbali mpaka kufikia mshindi wa tatu, sehemu nyengine yupo mwanamke peke yake lakini hakati tamaa, lengo lake ni kuingia kwenye vyombo vya kutoa maamuzi”, anasifia.
Anamshauri, aendelee kufanya vizuri kwa nafasi aliyonayo, kwani ndio itakayomtengeneza kufika mbele zaidi kule anakokutaka na pia azidishe ushirikiano kwa wananchi.
Ibrahim Mustafa Mussa ambae ni mtu wa karibu wa Aisha anafahamisha, ni mpambanaji na anapenda maendeleo chanya katika jamii.
Anasema, licha ya kupitia changamoto mbali mbali katika kugombea nafasi za uongozi, hakurudi nyuma aliendelea kupambana na hatimae alifanikiwa.
“Kwa kweli ni mwanamke mpambanaji na asiekata tamaa, kwa sababu aligombea kila nafasi na alipokosa hatukumuona kuvunjika moyo, aliendelea na kwa sasa ni kiongozi tena shupavu”, anafahamisha.
Aliwataka wanawake wengine kufuata miguu ya Aisha katika kugombea nafasi za uongozi, kwani yeye maneno ya watu hayakumfanya asiendelee kupambana.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Wete, Seif Salim Mussa anamfahamu Aisha kuwa ni mtendaji mzuri, anaemsaidia katika kazi na kumshauri vitu vya msingi.
“Ni mfuatiliaji, yuko vizuri, mzalendo na anapenda sana maslahi ya vijana, ni msawa, muwazi na mwaminifu, kwa kweli nimefarajika kupata makamo huyu, wanawake wanaweza”, anasema.
WANAHARAKATI/ JUMUIYA
Mratibu anaesimamia chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa upande wa Pemba, Fat-hiya Mussa Said anasema, wamekuwa wakiwajengea uwezo wanawake kwa kuwapa elimu, ili wajiamini, wasimame imara katika kuhakikisha wanashika nafasi za uongozi katika vyombo vya kutoa maamuzi.
Nassor Kassim Maalim ambae ni mratibu wa Umati Pemba anasema, wamekuwa wakiwapa elimu ya uongozi vijana wakiwemo wanawake ambao hata katika ofisi yao wanashika uongozi kenye nafasi mbali mbali.
“Tunawapa elimu ya uongozi, namna ya kujitambua, kujiwekea malengo, afya ya uzazi na ujasiriamali na sasa wameanzisha vikundi ambavyo kuna viongozi wanawake”, anaeleza.
Mratibu huyo anawashauri wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi kuanzia kwenye taasisi, hiyo itawasaidia kujiamini na hatimae wataweza kuingia majomboni.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwenye kifungu cha 12 (1), sura ya tatu imeeleza kuwa ‘Watu wote na sawa mbele ya sheria’, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake ana wajibu wa kuwa kiongozi katika nchi.