NA ABDI SULEIMAN.
HARAKATI za ujenzi wa barabara kongwe Kisiwani Pemba Wete – Chake Chake, yenye urefu wa kilomita 22 imeanza kwa kikao cha pamoja cha kujadili utekelezaji wa mradi huo, utakaokuwa mkombozi wa kiuchumi kwa wananchi wa maeneo yatakayopitiwa na mradi huo.
Kiako hicho cha kwanza kilichowashirikisha wakuu wa Mikoa, Wilaya za Pemba, uongozi wa wizara ya ujenzi mawasiliano na uchukuzi Zanzibar na watendaji kutoka kampuni ya MECCO iliyopewa dhamana ya ujenzi wa mradi huo na kufanyika Mjini Wete.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi zanzibar Amour Halim Bakar, alisema ubovu wa barabara hiyo unaleta changamoto kubwa kwa wananchi wa maeneo hayo na kudumaza maendeleo yao ya kiuchumi.
Alisema sasa wakati umefika wa kuondosha changamoto hizo, kwani kukamilika kwake barabara hiyo itaweza kurahisha maendeleo kwa kuwafanya wafanyabiashara kupeleka mazao yao sokoni bila ya hofu yoyote.
Aidha alifahamisha kuwa taratibu zote za ujenzi wa barabara hizo zimeshakamilika, hivyo bila ya mashirikiano ya pande zote mbili ujenzi huo hautokamilika.
“Wenzetu hawa MECCO ndio waliopewa jukumu la ujenzi wa barabara hii, leo tumekuja hapa kutokana na ujenzi wa barabara hii kuingia katika mikoa yote miwili ipo upande wa Kusini na ipo upande wa kaskazini, vizuri viongozi tukawapa mashirikiano wenzetu hawa katika ujenzi”alisema.
Akizunguzmia suala la hifadhi ya barabara alisema ni jambo ambalo linahitaji umakini mkubwa katika kuona wananchi hawaendelei kujenga nyumba zao karibu na barabara kwani wakati wa ujenzi unapofika ulipaji wa fidia ndio changamoto kubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, alisema kujengw akwa barabara hiyo, itaweza kutoa furasa za kiuchumi kwa wananchi wa maeneo ambayo barabara inapita kusafirisha bidhaa zao kwa wakati.
“Binafsi leo nimefarajika sana kusikia na kuona kama barabara hii sasa inataka kujengwa, sote tunakumbuka wananchi juzi walivyosema mbele ya Rais juu ya kilio chao kwa barabara hii, sasa jambo hili ni la faraja na kupongezwa kwa serikali kuanza ujenzi wake”alisema.
Aidha aliutaka uongozi wa Wizara ya Ujenzi kukutana na wananchi kabla ya ujenzi kuanza, kwa ajili ya kuwafahamisha masuala mbali mbali, ikiwemo kupatiwa elimu juu ya Covid 19 na Ukimwi, kwani miradi kama hii baada ya kumalizika huacha madhara kwa wananchi”alisema.
Hata hivyo alishauri kufanyika kwa vikao vya mara kwa mara juu ya kujua changamoto zinazoikabilia barabara hiyo, wakati wa ujenzi wake pamoja na kujuwa maendeleo ya mradi huo.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, aliwataka wananchi kuipa mashirikiano ya dhati kampuni hiyo, wakati wa ujenzi wa barabara ili iweze kukamilika kwa wakati.
Alisema upatikanaji wa huduma na uimarishaji wa miundombinu ya barabara, itaweza kurahisisha maendeleo kwa wananchji wa maeneo hayo, sambamba kuzitaka taasisi za ZECO, ZAWA kuhakikisha wanaondosha vitu vyao iliujenzi uweze kuanza mara maoja.
Mkurugenzi Muendeshaji wa kampuni ya MECCO Abdulikadir Mohammed, alisema kampuni yao iko tayari kukamilisha ujenzi huo kwa wakati, lakini changamoto kubwa ni ulipaji wa fidia kwa wananchi, uwepo wa miundombinu ya utowaji wa huduma za umeme, maji na mkonge wa taifa.
Hata hivyo aliwaomba viongozi hao kuhakikisha wanashirikiana na kua bega kwa bega ili kuona ujenzi huo unaanza na kumalizika kwa wakati.