Thursday, January 16

TANZANIA moja ya nchi iliyokuwa kidemokrasia kuliko nchi nyengine  Afrika Mashariki

MRAJIS wa Jumuiya zisizo za kiserikali Zanzibar, Ahmed Abdulla, akifungua mdahalo wa siku tatu wa kubadilishana mawazo ili kuimarisha maarifa, taaluma, ujuzi na weledi kuhusu wajibu wa pamoja wa wadau wa kisiasa katika kujenga na kusimamia utekelezaji wa misingi ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania katika hoteli ya Abla Mtoni

TANZANIA ni moja ya nchi iliyokuwa kidemokrasia kuliko nchi nyengine zilizokuwepo Afrika Mashariki kutokana na kukua kwa uhuru, usawa na kushirikisha wananchi katika kutoa maamuzi kwa mujibu wa katiba.

Mrajis wa Jumuiya zisizo za kiserikali Zanzibar, Ahmed Abdulla, aliyasema hayo wakati akifungua mdahalo wa siku tatu wa kubadilishana mawazo ili kuimarisha maarifa, taaluma, ujuzi na weledi kuhusu wajibu wa pamoja wa wadau wa kisiasa katika kujenga na kusimamia utekelezaji wa misingi ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania katika hoteli ya Abla Mtoni.

Alisema Tanzania inapiga hatua kubwa ya demokrasia kwani ni nchi yenye amani, umoja na mshikamano na watu kuwa na uhuru wa kufanya shughuli zao kwa kufuata sheria za nchi ambayo ndio demokrasia.

Aidha alisema muitiko wa serikali kwa wananchi wenyewe juu ya kushirikiana na serikali yao, viongozi wanavyoshuka kwa wananchi kusikiliza kero zao na inayojitajidi kutatua kero hizo kwa kushirikiana na asasi za kiraia.

“Tumeona jinsi serikali kuu zinavyoshuka kwa wananchi kusikiliza kero zao na kupata mashauriano hata Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kuanzisha mfumo wa sema na Rais Mwinyi ambao una dhana katika kuwafikia wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa kuendeleza demokrasia, kufaidi masuala la utawala bora na kupata maendeleo ya nchi yao,” alibainisha.

Akizungummzia lengo la mdahalo huo alisema una umuhimu mkubwa katika kutathmini mwenendo wa nchi katika hatua za maendeleo na serikali inavyojitahidi katika kukuza demokrasia nchini.

Mrajis aliipongeza tasisi ya Mwalimu Nyerere Tanzania kwa kuamua kufanya mdahalo huo ambao unawapa hamasa ya uwajibikaji katika kuteleleza shughuli zao mbalimbali za maendeleo.

Tunapokaa na kushauriana tunajenga mustakabali mzuri wa kuendeleza yale mazuri ambayo yapo katika nchi kwa upande wa Zanzibar na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa kweli Tanzania ni moja ya nchi iliyopiga hatua kubwa kimendeleo tulipo sasa sio tulipotoka,” alisema.

Aliwaomba wananchi kuendeleza umoja, amani na mshikamano uliopo nchini ili nchi yao iendelee kupiga hatua za kimaendeleo kwani Amani, umoja na mshikamano ndio chachu kubwa ya kuendeleza demokrasia nchini Tanzania.

Hata hivyo, aliahidi kuwa Ofisi ya Mrajis wa Jumuiya zisizo za kiserikali wataendelea kushirikiana ili kuhakikisha wanaendeleza juhudi hizo za kuwapa wananchi taaluma na kujenga mustakabali mzuri kwao.

Mbali na hayo, alisema ni imani yake kwamba washiriki wa mdahalo huo watatumia nafasi hiyo itakayoweza kuleta matukio chanya ambayo yatakayoendeleza umoja, mshikamano, demokrasia na mambo mengine.

Mkurugenzi Mtendaji na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Tasisi ya Mwalimu Nyerere Tanzania Joseph Warioba Butiku alisema mdahalo huo unalego la kuendeleza mazungumzo yanayohusu mfumo uliopo Tanzania wa kuendesha taifa kidemokrasia na hakika kwamba wananchi ndio wanaoamua kuhusu nchi yao iendeshwe vipi na nani na utaratibu gani.

Alisema Tanzania ina taifa huru liloanzishwa na wasisi wawili akiwemo Mwalimu Julias Kambarage Nyerere kwa Tanzanzia bara na Mzee Abeid Aamni Karume kwa Zanzibar ambao wote walitumia vyama vya siasa TANU na ASP na baadae kuwa chama kimoja.

“Wote walikuwa na lengo moja na ewalikuwa wakieleza bayana kwamba wanashughulika na wananchi wawe huru, wajitawale wenyewe ambao ndio msingi mkuu,” alibainisha Warioba.

Nae, Ofisa Miradi kutoka Shirika la Kijerumani (FES) Amon Petro alisema mdahalo huo ni muendelezo wa kupata maoni ya wadau mbalimbali kupata maoni yao ili kuendeleza na kuboresha mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania.

Alisema lengo ni kuwa na mfumo ambao unakuwa endelevu na tija kwa taifa.

Hata hivyo alibainisha kuwa kimsingi Tanzania ni nchi inayoendelea kukua hasa katika masuala ya demokrasia kutokana na watu kupata fursa ya kutoa mawazo yao na kuwasilisha kero zao mbrele ya viongozi wa nchi.

Nao, washiriki wa mdahalo huo walisema demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini Tanzania una faida kubwa kwani imekuwa ikishirikisha watu kutoka vyama mbalimbali katika serikali.

Hata hivyo, walibainisha kuwa kuwepo kwa umoja, amani , mshikamano na ushirikishwaji wa wananchi katika mambo ya kitaifa ni kukuwa kwa demokrasia.

Waliiomba Tasisi ya Mwalimu Nyerere kuendelea kutoa mafunzo hayo ya mfumo wa vyama vingi vya demokrasia katika kila ngazo ili wananchi wote waweze kufahamu dhana ya demokrasia.

Katika mdahalo huo mada mbalimbali zilijadiliwa ikiwemo mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania na kutumika kwa mifumo ya asili (jadi) ya Afrika kama nyenzo ya kukuza utawala wa kidemokrasia.

MWISHO