Thursday, January 16

Wizara ya Ujenzi SMT na Wizara Ujenzi SMZ wafanya ziara kwa pamoja kisiwani Pemba.

KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi SMT Gabriel Migire akisikiliza swali kutoka kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari, juu ya ziara yao ya mashirikiano baina ya watendaji kutoka wizara ya Ujenzi na Uchukuzi SMT na Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar.(PICHA NA ABDI SULEIMAN, PEMBA)

 

NA ABDI SULEIMAN.

WIZARA ya Ujenzi na Uchukuzi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imesema kuwa itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi ya Zanzibar, ili kuona Kisiwa cha Pemba kinapiga hatua kubwa kimaendeleo kupitia bandari zake.

Hayo yameelezwa na katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kutoka SMT Gabriel J.Migire wakati alipokua akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kumaliza ziara ya mshikamano kati ya wizara ya Ujenzi SMT na Wizara Ujenzi SMZ, huko katika bandari ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Alisema wameshuhudia kuona shuhuli mbali mbali zinazofanyika katika bandari ya Wete, ikiwemo kushusha abiria na mizigo kupitia meli zinazofunga gati katika bandari hiyo.

Alifahamisha kwamba bandari inaendelea kufanya kazi kazi zake vizuri, hivyo wataendelea kushirikiana ili kuona bandari hiyo inaboreka zaidi na kuweza kukusanya mapato kwa wingi.

“Ziara yetu hii sisi watendaji ni muhimu sana, tumeweza kujifunza mambo mengi yanayofanywa na wenzetu wazanzibar kwa upande wa Pemba”alisema.

Aidha Katibu Mkuu Gabriel, alisema kisiwa cha Pemba kinafursa nyingi za kuzitangaza, ikiwemo maeneo huru ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji mbali mbali ndani nan j e ya nchi kuwekeza.

Akizungumzia kuhusu mnara wa kuongozea meli Kigomasha, alishauri Wizara Ujenzi mawasiliano na uchukuzi Zanzibar, kuujengea ngazi ya nje itakayoruhusu wananchi kupanda juu na kulipia fedha kutokana na umuhimu wa mnara huo.

“Huu ni mnara wa kuingizwa katika histori zaidi ya mika 100 sasa upon a unafanya kazi, sasa tusiruhusu watu kupita kwa ndani vizuri kutumia kwa nje huko”alisema.

Kwa upande wake katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Amour Hamil Bakari, alisema lengo la ziara ni kuongeza mashirikianao baina ya watendaji wa wizara ya Ujenzi SMT na SMZ, ili kuona jinsi gani kazi zinafanikiwa.

Aidha alisema katika ziara hiyo mapungufu yote yaliyotokea wako tayari kuyapokea, kwani ndio utendaji kazi na yataweza kuwasaidia katika kazi zao.

“Katika maeneo ya Bandarini na Masuala ya Hali ya hewa, hapa kuna mambo wenzetu wataweza kutueleza na sisi tupo tayari kuyatekeleza kwa vitendo, pale watakapotushauri ili kufikia maendeleo waliofikia wao”alisema.

Kwa upande wake Mkurugebziu Mkuu wakala wa shirika la Meli Kaimu Abdi Mkeyenge, alisema kitu kizuri walicho kiona katika bandari ya wete ni ushushaji wa abiria, pamoja na gari za mizigo jambo ambalo litaweza kuongeza mapato kwa Shirika hilo.

Aliitaka Wizara kuhakikisha kuboreshwa kwa mifumo ya uwendeshaji, ili mapato yaweze kuongezeka pamoja na upatikanaji wa vifaa vya kisasa katika bandari hiyo.

Kwa upande wa Mnara wa kuongezea meli Kigomasha, Kaimu mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Kepteni Abdulla Mwingamno, alisema mnara huo sio kwa meli zinazoingia Zanzibar tu bali hata meli zote zinapopita katika eneo la nje ya Kisiwa cha Pemba huutumia kwa ajili ya kujuwa wapi walipo.

“Huu mnara unasaidia sana meli za kimataifa zinazopita katika maeneo ya bahari, lazima meli kufuata mnara huo na kujuwa walipo na ndio waendelee na safari zao”alisema.

Naye mkurugenzi Mkuu wa shirika la Bandari Zanzibar Nahat Mohamed Mahfoudh, alisema mnara wa kigomasha ni moja ya minara muhimu kwa Serikali, kwani unalazimika kufanya kazi masaa 24 katika kuongoza meli zote zinazopita katika eneo la ndani nan je ya kisiwa cha Pemba.

Alisema changamoto kubwa uvamizi wa eneo la mnara huo kwa makaazi ya wananchi, jambo ambalo limepelekea Wizara kuwekea uzio mnara huo ili kudhibiti suala hilo.