Thursday, January 16

MABADILIKO  ya tabia nchi dunia inashuhudia  idadi ya siku ambazo nyuzi joto ni zaidi ya selsiasi 50

Idadi ya siku za joto kali kila mwaka wakati joto hufikia selsiasi 50 zimeongezeka mara mbili tangu miaka ya 1980, utafiti wa BBC umebaini.

Pia sasa hivi hili ni tukio ambalo hutokea katika maeneo mengi zaidi ulimwenguni kuliko hapo awali, ikitoa changamoto ambazo hazijawahi kutokea mbeleni, kwa afya ya binadamu na jinsi tunavyoishi.

Jumla ya siku ambazo nyuzijoto ni zaidi ya selsiasi 50 zimeongezeka katika kila kipindi cha miongo minne iliyopita.

Kati ya mwaka 1980 na mwaka 2009, kiwango cha joto kilipita selsiasi 50 karibu siku 14 kwa mwaka kwa wastani, na siku hizo zikaongezeka hadi 26 kwa mwaka kati ya 2010 na 2019. Katika kipindi hicho hicho, joto kiwango cha selsiasi 45 na zaidi likashuhudiwa kwa wastani wa wiki mbili za ziada kwa mwaka.

“Ongezeko hilo linaweza kuhusishwa kwa asilimia 100 na uchomaji wa makaa ya mawe,” anasema Dkt. Friederike Otto, mwanasayansi anayeongoza katika utafiti wa hali ya hewa.

Wakati ulimwengu wote unaposhuhudia joto, uwezekano wa joto kuwa kali zaidi unazidi kuongezeka.

Joto kali linaweza kuwa hatari kwa mwanadamu na uasilia, na kusababisha matatizo makubwa katika majengo, barabara na mifumo ya umeme.

Joto la nyuzi 50 hutokea sana katika maeneo ya Mashariki ya Kati na Ghuba.

Na baada ya joto kuvunja rekodi ya nyuzijoto 48.8 za selsiasi huko Italia na nyuzi 49.6 huko Canada msimu huu wa joto, wanasayansi wameonya kwamba siku za kuwa na nyuzi joto zaidi ya 50 zitaongezeka katika sehemu zingine isipokuwa ikiwa tutasitisha uzalishaji wa nishati ya mkaa ya mawe.

“Tunahitaji kuchukua hatua haraka. Kadiri tunavyopunguza kasi ya uchafuzi wa mazingira, ndivyo tutakavyokuwa salama,” anasema mtafiti wa hali ya hewa Dkt Sihan Li.

“Kwa kuendelea na uzalishaji wa hewa chafuzi na ukosefu wa kuchukua hatua, sio tu kwamba matukio ya joto kali yatazidi kushuhudiwa mara kwa mara, lakini mwitikio wa haraka na kukabiliana na hali hii itakuwa changamoto zaidi,” anaonya Dk Li.

Uchambuzi wa BBC pia uligundua kuwa katika muongo mmoja wa hivi karibuni, kiwango cha juu cha joto kiliongezeka kwa kiwango cha 0.5 za selsiasi ikilinganishwa na wastani wa muda mrefu kutoka mwaka 1980 hadi mwaka 2009.

Lakini ongezeko hili halijahisiwa sawa kote ulimwenguni: Ulaya Mashariki, kusini mwa Afrika na Brazil kulishuhudiwa kiwango cha juu zaidi cha joto kilichoongezeka kwa zaidi ya selsiasi 1, huku sehemu za Arctic na Mashariki ya Kati zikirekodi ongezeko la zaidi ya selsiasi 2.

Wanasayansi wanatoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za dharura kutoka kwa viongozi wa ulimwengu katika mkutano wa UN wa Novemba, ambapo serikali zitaombwa kujitolea kuhakikisha zinafikia lengo jipya la kupunguzwa kwa uzalishaji wa hewa chafuzi ili kupunguza ongezeko la joto duniani.

Athari za joto kali

Uchambuzi huu wa BBC ulizindua mfululizo wa makala inayoitwa ‘Life at 50C’ yaani ‘Maisha katika hali ya nyuzijoto 50’ ikichunguza jinsi joto kali linavyoathiri maisha ulimwenguni.

Hata chini ya nyuzijoto 50, joto kali na unyevuunyevu unaweza kusababisha hatari kubwa za kiafya.

Watu wengi kama bilioni 1.2 duniani wanaweza kukabiliwa na hali ya msongo wa mawazo kwasababu ya joto kali ifikapo mwaka 2100 ikiwa viwango vya sasa vya ongezeko la joto ulimwenguni vitaendelea, kulingana na utafiti wa Chuo Kikuu cha Rutgers uliochapishwa mwaka jana.

Hiyo ni angalau mara nne zaidi kuliko wale walioathirika leo hii.

Watu pia wanakabiliwa na ugumu katika machaguo wakati mazingira yanayowazunguka yanabadilika, kwani joto kali linasababisha ukame na kutokea kwa moto wa msituni.

Sheikh Kazem Al Kaabi ni mkulima wa ngano kutoka kijiji cha katikati mwa Iraq, ambacho hushuhudia joto kali kila mwaka.

Ardhi iliyomzunguka kuna wakati ilikuwa na rutuba ya kutosha kumtosheleza yeye na majirani zake, lakini pole pole imekuwa kavu na sasa haifai kwa kilimo.

“Ardhi hii yote ilikuwa ya kijani kibichi, lakini yote sasa imekuwa kavu. Ni jangwa, ukame.”

Karibu watu wote kutoka kijiji chake wamehama kutafuta kazi katika majimbo mengine.

“Nilimpoteza kaka yangu, marafiki wapenzi na majirani waaminifu. Nilishirikishana nao kila kitu, hata kicheko changu. Sasa hakuna mtu anayeshirikisha chochote nami, naangaliana tu na ardhi isiyo na chochote.”

Dunia hatarini kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa, wasema wanasayansi

Mbinu iliyotumika

Nyuzijoto ilikuwa ni zaidi ya selsiasi 50 katika eneo langu, kwanini halikuangaziwa?

Ripoti za kiwango cha joto iliovunja rekodi kawaida hutoka kwa vipimo vilivyochukuliwa katika kituo cha hali ya hewa na mtu binafsi.

Lakini data tuliyotumia inawakilisha maeneo makubwa kuliko yale yaliyotumika na kituo kimoja.

Kwa mfano, Hifadhi ya Kitaifa ya Death Valley kusini mwa California ni moja wapo ya maeneo yenye joto jingi zaidi Duniani.

Joto katika sehemu fulani za hifadhi mara nyingi kiwango chake cha joto hupita nyuzijoto 50 wakati wa kiangazi.

Lakini wakati unataka kuwa na kiwango cha joto la juu cha wastani kwa eneo pana, ukitumia vyanzo kadhaa tofauti, takwimu chini ya nyuzijoto 50 hufikiwa.

Je data hizi zimetolewa wapi?

BBC imetumia kiwango cha juu cha joto la kila siku kutoka kwa data ya azimio la dunia ya ERA5 ya kiwango cha juu, iliyotolewa na Huduma ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa ya Copernicus.

Takwimu hiyo mara nyingi hutumiwa kuchunguza mwenendo wa mabadiliko ya hali ya hewa duniani.

ERA5 inachanganya uchunguzi halisi wa hali ya hewa kutoka vyanzo vingi, kama vile vituo na satelaiti, na data kutoka kwa modeli za kisasa za utabiri wa hali ya hewa.

Mchakato huu unajaza udhaifu uliojitokeza kwasababu ya ufikiaji duni wa kituo cha hali ya hewa katika sehemu nyingi za ulimwengu na husaidia kuelewa mabadiliko ya hali ya hewa.

Je ni tathmini gani ambazo tumefanya?

Kwa kutumia kiwango cha juu cha joto kwa kila siku kutoka mwaka 1980 hadi mwaka 2020, tuligundua ni mara ngapi joto lilizidi nyuzijoto 50.

Tulihesabu idadi ya siku na maeneo yenye joto la juu la nyuzi 50 au zaidi kwa kila mwaka, kuamua mwenendo wa hali ya hewa kwa muda.

Pia tuliangalia mabadiliko katika kiwango cha juu cha joto.

Tulifanya hivyo kwa kuangalia tofauti iliyopo kati ya wastani ya kiwango cha juu cha joto katika ardhi na baharini kwa muongo mmoja wa hivi karibuni (2010-2019) ikilinganishwa na miaka 30 kabla yaani mwaka (1980-2009).

Wastani wa angalau miaka 30 mfululizo hujulikana kama elimu ya utabiri wa hali ya hewa.

Elimu ya utabiri wa hali ya hewa ya miaka thelathini hutumiwa kuonyesha jinsi vipindi vya hivi karibuni vilivyokuwa ikilinganishwa na wastani wa hali ya hewa.

Tuna maanisha nini kwa ‘eneo’?

Kila eneo ni karibu kilomita 25 za mraba au karibu kilomita 27-28 za mraba kwenye ikweta.

Gridi hizi zinaweza kujumuisha maeneo makubwa na zinaweza kuwa na aina tofauti za mandhari.

Gridi ni mraba wa latitudo ya digrii 0.25 na urefu wa digrii 0.25.

Utambuzi wa waliofanikisha makala hii

Mbinu iliyobuniwa na kutumika ni kwa usaidizi wa kutoka kwa Dkt. Sihan Li wa Shule ya Jiografia na Mazingira, Chuo Kikuu cha Oxford, na Dkt. Zeke Hausfather wa Berkeley Earth. Mapitio ni kutoka Kituo cha Uropa cha Utabiri wa Hali ya Hewa (ECMWF). Shukrani za pekee ni kwa Profesa Ed Hawkins wa Chuo Kikuu cha Reading pamoja na Profesa Richard Betts na Dkt. John Caesar katika Ofisi ya Hali ya Hewa.

Uchambuzi wa data na waandishi habari ni Nassos Stylianou na Becky Dale.

Ubunifu ni kwa Prina Shah, Sana Jasemi na Joy Roxas. Maendeleo ya matukio na Catriona Morrison, Becky Rush na Scott Jarvis. Uhandisi wa data na Alison Benjamin. Matukio yaliyofanyiwa uchunguzi ni kwa Namak Khoshnaw na Stephanie Stafford. Mahojiano na Dkt. Otto na Monica Garnsey. Taswira ya hali ya hewa na Profesa Ed Hawkins na Chuo Kikuu cha Reading.

 

BY: Na Becky Dale & Nassos Stylianou (BBC/SWAHILI)

MWISHO