Thursday, January 16

TAASISI yashauriwa kutumia vyuo vya elimu ya juu nchini kutoa elimu ya Demekrasia na Uzalendo

MKURUGENZI Mtendaji na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Tanzania Joseph Warioba Butiku akitoa maelezo juu ya mdahalo wa kubadilishana mawazo, ili kuimarisha maarifa, taaluma, ujuzi na weledi kuhusu wajibu wa pamoja wa wadau wa kisiasa katika kujenga na kusimamia utekelezaji wa misingi ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania katika hoteli ya Abla Mtoni.(PICHA NA AMEIR KHALID)

TASISI ya Mwalimu Nyerere Tanzania, imeshauriwa kutumia vyuo vya elimu ya juu vilivyokuwepo nchini Tanzania kutoa elimu ya demokrasia na uzalendo ili kuwasaidia wanafunzi watakaopata nafasi za uteuzi serikalini wawe tayari wameiva katika utekelezaji wa majukumu yao.

Kaimu Mkurugenzi wa Shada za Juu, Utafiti na Ushauri Elekezi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar SUZA Dk. Abdalla Ibrahim Ali wakati akichangia mada ya majukumu ya tasisi za serikali pamoja na asasi za kiraia katika kendeleza demokrasia ya vyama vingi katika ukumbi wa Abla Sharifumsa.

Alisema hatua hiyo itasaidia sana kuwajenga wanafunzi kujua demokrasia iliyokuwepo nchini kwao kwani wanafunzi wengi hawajui demokrasia iliyokuwepo nchini kwao.

Alibainisha kuwa wamegundua kuwa wanafunzi wengi wanaoandaliwa katika vyuo vikuu ambao ndio viongozi wa baadae hawana taaluma ya demokrasia ambayo sio kwa vyama vya siasa pekee bali ni utekelezaji wa majukumu ya kiongozi katika tasisi yake kuitekeleza kwa mujibu wa haki na usawa.

“Vyuo vikuu ndio vinavyozalisha viongozi wa nchi yetu katika tasisi za serikali na sizizokuwa za kiserikali, demokrasia inakwenda sambamba na uzalendo, ukiangalia hawasimamii mfumo wa denokrasia ya vyama vingi kutokana na kutoijua demokrasia,” alibainisha.

Haya hivyo, alibainisha kuwa kama viongozi wanaoandaliwa katika vyuo vikuu hawana elimu ya demokrasia katika majukumu yao ya kazi ndio inayopelekea kuwa na viongozi ambao ufanisi wao sio mzuri.

“Hapa utakuta tuna viongozi ambao wanatamaa ya mali za umma na serikali kuzitumia binafsi, ubadilifu na wanaotoa maamuzi kwa njia ya upendeleo katika tasisi zao ambayo hayamo katika sheria za nchi ambazo walitakiwa wawe nazo na kuzifahamu na kutoa maamuzi sahihi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa,” alisema.

Abdalla ambae pi ni Mhadhiri Mwandamizi SUZA, aliiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuangalia upya mtaala wa somo la historia katika maskuli ili watoto na vijana waweze kujua demokrasia na siasa ambayo itaweza kujenga nchi katika misingi inayotakiwa.

“Ukiangalia mtaala wa historia ninaoukumbuka ni wa mwaka 1970 na 1980 ambao tulikuwa tunasomeshwa historuia na somo la siasa na uzalendo lakini sasa tunasoma historia ya dunia kuijua Tanzania, Benbella, Beit al Ajab, Mwalimu Nyerere na Karume walikuwa vipi lakini historia hasa na uzalendo wa siasa tuliyokuwa tukisomeshwa zamani haipo ndio maana utakuta vijana wa sasa wengi wao historia ya nchi yao hawaijui,” alisema.

Kwa upande wake Mrajis wa Jumuiya zisizo za kiserikali Zanzibar, Ahmed Abdulla, alisema kuna umuhimu mkubwa wa somo hilo katika vyuo vikuu kwani suala la demokrasia na utawala bora lina umuhimu mkubwa nchini katika kuwandaa wahitimu kufahamu masuala ya utawala bora na hata katika kuangalia sheria mbalimbali za nchi ili ziweze kuwasaidia pale wanapopata teuzi serikalini.

Alisema unapojua demokrasia basi unatambua malengo hasa ya serikali ya kukuza demokrasia na muitikio wananchi katika kuhitaji demokrasia na utawala bora ambavyo ni vitu muhimu kuvijua kwa viongozi.

Mkurugenzi Mtendaji na Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Tasisi ya Mwalimu Nyerere Tanzania Joseph Warioba Butiku aliahidi kulifanyia kazi ombi hilo ambalo litasaidia kuwajenga wanafunzi wa vyuo vikuu nchini kuwa na elimu ya kujitegemea na kuwa wazalendo na nchi yao.

Akiwasilisha mada ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania, Mkufunzi Abrahman Mnoga, alisema demokrasia ni mfumo wa serikali ambao wananchi wote ni sawa mbele ya sheria na wanashiriki katika kufanya maamuzi ya kitaifa juu masuala ya umma.

Alisema demokrasia makini ni mbegu ya maendeleo kupitia mgawanyo sahihi na linganifu wa rasilimali za taifa na mbegu ya amani, umoja na mshikamano ndani ya nchi yao.

Aidha akizungumzia faida na umuhimu wa uongozi wa kidemokrasia alisema ni pamoja na amani, mshikamano katika jamii na maendeleo yenye tija kwa watu wote.

Alitumia muda huo kuviomba vyama vya siasa na wadau mbalimbali kuielimisha jamii juu ya umuhimu wa kujua katiba yao na wananchi wana wajibu wa kuifahamu katiba ya nchi yao kama chombo na msingi imara wa demokrasia nchini.