Je! tembo wa kale wa sufu wanaweza kuishi tena duniani? Hivi ndivyo inavyopendekezwa na kundi la wanasayansi na wafanyabiashara, ambao tayari wamepokea dola milioni 15 za Marekani kufanikisha kazi hiyo.
Kampuni ya Colossal inataka kukuza teknolojia za uhandisi wa kijenetiki kwa bajeti hiyo ili kuunda kosafu kati ya tembo wa kale (Mammoth) na tembo wa Asia, ikikaribia iwezekanavyo kwa tembo wa kale ambao waliwahi kukaa sayari yetu.
Mara tu lengo hili litakapofanikiwa, hatua inayofuata itakuwa kujaza sehemu za Siberia na wanyama hawa, kutafuta usawa wa mazingira.
“Hiyo italeta mabadiliko ulimwenguni,” alisema mwanabaiolojia George Church, kutoka Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Harvard, huko Marekani, katika mahojiano na gazeti la Marekani The New York Times.
Kwa miaka minane iliyopita, Church ametumia wakati wake mwingi kusimamia mradi huo na washirika wengine wa wazo hilo.
Sehemu ya mwanzo ya kazi yake ni nyenzo za jeni za mabaki yaliyohifadhiwa ya tembo wa kale ambao walikufa miaka elfu iliyopita.
CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Lakini pia kuna wale ambao wanapinga wazo hilo, wakitoa mfano wa matatizo ya kimaadili katika kuokoa wanyama wakubwa kutokana na kutoweka.
Kuna wasiwasi pia kuhusu mammoth hawa watakavyokuwa duniani leo.
“Kuna shida nyingi sana ambazo utakutana nazo njiani,” Beth Shapiro, mtaalamu wa stadi za viumbe wa kale katika Chuo Kikuu cha California, pia aliiambia The New York Times.
Chanzo cha wazo
Wazo la kurudisha tembo wenye sufu lilitolewa kwanza na Bw.Church mnamo 2013.
Wakati huo, watafiti walikuwa wakisoma vipande vya DNA vilivyopatikana kwenye mabaki ya zamani, katika jaribio la kuunda tena genome za spishi zilizotoweka.
Bw. Church, ambaye anasoma njia mpya za kusoma na kuhariri DNA, alijiuliza: inawezekana kufufua spishi iliyotoweka kwa kurekebisha genome ya jamii iliyopo leo?
Alizingatia tembo hao ni bora kwa sababu wao ni viumbe wa kale wa karibu na ndovu wa Asia – wana asili ya spishi moja ya kale iliyoishi miaka milioni 6 iliyopita.
Pia, DNA ya tembo wa kale inaweza kupatikana kwa urahisi huko Siberia.
Mtaalamu wa biolojia anaelezea kuwa tembo wa kale pia anaweza kusaidia kurudisha usawa wa ikolojia: ongezeko la joto ulimwenguni limesababisha kuongezeka kwa joto katika tundra (tambarare pana isiyo na miti) ya Siberia na Amerika ya Kaskazini, ambayo imesababisha kutolewa kwa kasi kwa idadi kubwa ya hewa ya ukaa.
CHANZO CHA PICHA,AVERAGE PA
Katika tundra ya leo ya Siberia, sehemu kubwa imefunikwa na kuvumwani (moss), lakini katika nyakati za tembo wa kale, kulikuwa na nyasi.
Wanabiolojia wanaamini kuwa mammoth aliwahi kuwa mlinzi wa mfumo huu wa mazingira, kudumisha nyasi, kusafisha kuvumwani, kuvunja miti, na kuacha kinyesi tele ambacho kilirutubisha udongo.
Ikiwa wanyama hawa wangerudi, yote haya yangeweza kupatikana na yana uzalishaji wa hewa ya ukaa, wanasema.
Mawazo ya awali ya mwanasayansi huyo yalivutia waandishi wa habari, lakini sio wawekezaji; mwanzoni, aliweza kukusanya dola za Kimarekani 100,000 tu kwa utafiti wake.
“Kusema kweli, nilikusudia kufanya kazi kwa kasi ndogo,” Church alisema.
Lakini mwaka 2019 alikutana na Ben Lamm, mwanzilishi wa kampuni ya teknolojia ya Texas, AI Hypergiant. Akisoma habari kuhusu mradi huo, alivutiwa kusaidia kumuokoa mnyama huyo mkubwa.
“Baada ya kukaa siku moja kwenye maabara na kutumia muda mwingi na George, tulifurahi sana,” anakumbuka Lamm, ambaye kuanzia hapo alianza kuunda kampuni kubwa.
CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Wanyama waliopotea wanaweza kufufuliwa kwa njia mbili: uumbaji na uhandisi wa maumbile, yaani mchakato wa kutumia teknolojia ya DNA kubadilisha muundo wa maumbile wa kiumbe.
Njia ya kwanza inajulikana sana kutoka kwa mfano wa kondoo wa Dolly, aliyeumbwa mnamo 1997. Katika mchakato huu, DNA ya mnyama mmoja huingizwa ndani yai lililorutubishwa la mnyama mwingine wa kisha yai hupandikizwa kwa “mama anayekusudiwa kuzaa.” (Surrogate)
Miaka mitatu baada ya kutoweka kutoka kwa uso wa Dunia, ngozi iliyohifadhiwa ya mnyama ilitolewa na DNA yake ilibuniwa. Mbuzi aliyebeba mimba alizaa mbuzi, wa kwanza kufufuliwa au spishi iliyotoweka.
Kwa bahati mbaya, pia ilikuwa kesi ya kwanza ya kutoweka mara mbili, kwani iliishi tu kwa dakika 7.
Hapa ndipo njia ya pili ya ufufuo inaweza kusaidia, kinachojulikana kama teknolojia ya uhariri wa jeni ya CRISPR.
Ndani yake, jeni maalum ambazo ziliruhusu mammoths kuishi katika latitudo za juu huingizwa kwenye jenome ya jamaa yao wa karibu zaidi, tembo wa Asia.
CHANZO CHA PICHA,GETTY IMAGES
Jenome iliyobadilishwa kisha hupandikizwa ndani yai la tembo lililorutubishwa, ambalo hupandikizwa kwa mama aliyemzaa tembo. Kutoka hapo, mseto wa tembo na mammoth unatarajiwa kuzaliwa.
Kwa kweli, kuna shida kubwa, kama ukweli kwamba wanasayansi hawajui ni jeni gani zinahitajika kuishi katika bara Aktiki.
Wanajua kwamba mnyama lazima afunikwe na manyoya, awe na fuvu la mviringo na safu nyembamba ya mafuta ya ngozi.
Hivi sasa, karibu aina milioni ya mimea na wanyama wako katika hatari ya kutoweka.
Kwamujibu wa Lamm, ikiwa mradi wa Colossal umefanikiwa, utafungua njia ya “kuokoa jeni” za spishi mbalimbali.
Inamaanisha mchakato wa kuongeza utofauti wa maumbile wa spishi zilizo hatarini kupitia uundaji wa uumbaji au uhandisi.
Lamm anasema mradi wa mammoth ni aina ya “jaribio.”
Kwa hivyo, mradi wa kufufua tembo wa kale unaweza kuonekana kama aina ya incubator kwa maendeleo ya uhandisi wa maumbile na miliki, ambayo labda ni rahisi kuliko kuona mammoth hai ya sufu akizaliwa.
CHANZO CHA HABARI BBC