Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, tarehe 22 Septemba, 2021 ameshiriki mkutano wa pamoja kati ya wafanyabiashara wa Tanzania na Marekani na kuhimiza kuimarishwa kwa biashara kati ya mataifa hayo mawili ili kuwa na faida kwa pande zote.
Mhe. Rais Samia amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa kwa sasa biashara zinazofanyika kati ya Tanzania na Marekani ni ndogo ikilinganishwa na fursa zilizopo.
Amesema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2019, Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 241na kuuza bidhaa zenye thamani ya dola za kimarekani milioni 46. Kwa upande mwingine Marekani imewekeza Tanzania Dola za Kimarekani bilioni 5.55 na kuajiri watu 44,118 wakati Tanzania imewekeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni moja tu ambacho ni kiasi kidogo ikilinganishwa na ukubwa wa uchumi wa Marekani duniani na fursa zilizopo Tanzania.
Mhe. Rais Samia amewaeleza wafanyabishara hao kuwa angependa kuona biashara inaongezeka kwa kuwa Tanzania ni mwanachama katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na pia Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo zinatoa fursa za wawekezaji na wafanyabishara wa Marekani kwa soko la watu milioni 450, hivyo kuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji.
Aidha, Mhe. Rais Samia pia amewaeleza wafanyabiashara hao kuwa Tanzania imesaini mkataba wa Biashara Huru Barani Afrika (AfCFTA) ambao umelegeza masharti ya biashara na kuunganisha soko la watu bilioni 1.3.
Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya (EU) Mhe. Charles Michel ambaye amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kukutana nae na kueleza kuwa lengo lake ni kutaka kupata maoni ya Mhe. Rais Samia kuhusu mambo manne ya kipaumbele kwa Umoja wa Ulaya kwenye mahusiano yake na Afrika na utayari wa Umoja wa Ulaya kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo hayo.
Mambo hayo ni UVIKO 19, Mabadiliko ya Tabia Nchi, Hali ya Usalama nchini Msumbiji na Mapinduzi ya Kidijitali.
Kwa upande wake Mhe. Rais Samia ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa ushirikiano wake na kuelezea hatua ambazo Tanzania inachukua katika kukabiliana na UVIKO 19, hasa ikizingatiwa kuwa ugonjwa huo umeathiri sekta nyingi ikiwemo sekta ya utalii.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Rais Samia ameeleza hatua mbalimbali ambazo Serikali inachukua katika kusambaza miundombinu ya afya ingawa bado kuna changamoto katika upatikanaji wa vifaa tiba na rasilimali watu na hivyo kuukaribisha Umoja wa Ulaya kuangalia namna ya kushirikiana na Tanzania katika maeneo hayo.
Kuhusu Mabadiliko ya Tabia Nchi, Mhe. Rais Samia amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoathirika na Mabadiliko ya Tabia Nchi na inalipa kipaumbele suala hilo katika kukabiliana nalo.
Pia, Mhe. Rais Samia amehudhuria Mkutano wa kuadhimisha miaka 20 ya Tamko la Durban kuhusu kupinga ubaguzi wa rangi na aina zote za unyanyasaji.
Kesho tarehe 23 Septemba, 2021 Mhe. Rais Samia atahutubia Mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa unaoendelea hapa New York nchini Marekani.