Thursday, January 16

Wanawake wahimizwa kupendana ili waweze kushinda katika nafasi mbali mbali za uongozi.

NA ABDI SULEIMAN.

KATIBU Tawala Wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki, amewahimiza wanawake kupendana wakati fursa za uongozi zinapotokea, ili wawe na sauti ya pamoja ya kuingia katika nafasi mbali mbali za kuiongoza jamii.

Alisema wenyewe wanashinda kupendana na kuwa kitu kimoja wakati nafai za uongozi zinapotokea, hali inayopelekea kuwapa nafasi kubwa wanaume.

Katibu huyo aliyaeleza hayo katika hafla ya uzinduzi wa kamati ya uhamasishaji wanawake kuweza kudai haki zao za uongozi, ulioandaliwa na jumuiya ya PEGAO kupitia mradi wa ushirikishaji wanawake, katika uongozi unaotekelezwa kwa masirikiano na jumuiya ya PEGAO,ZAFELA na TAMWA chini ya ufadhili wa ubalozi wa Norway.

Alisema kitendo kusema kuwa mwanamke hawezi kuongoza, kimepitiwa na wakati na kwamba kinachohitajika kwao ni kujiamini na kujitayarisha, kielimu ili wawe na uwezo mkubwa wa utowaji wa maamuzi.

“Tukiamua kuanzisha faragasi katika majumbani wetu basi hakuna mwanamme yoyote anayeweza kutuzuwia, hata kwenye mambo haya ya uongozi ndio hivyo hivyo, sasa masuala ya kuwaonea wanawake kwamba hawawezi kuongoza yamepitwa na wakati”alisema.

Alisema ili kuwajenga wanawake kuwa viongozi wazuri wa baadae, lazima wanawake wenyewe wawe tauari kusaidia kujiamini na kuwa kitu kimoja wakati wote.

Kwa upande wake mratibu wa mradi huo Dina Juma, aliwataka wanawake kuitumia fursa iliyowekwa na serikali, ili kuongeza idadi ya viongozi katika ngazi za maamuzi na kufikia malengo ya meleniam ya kuwa na usawa wa kijinsi katika nyanja tofauti.

Alisema Mradi huu umekuja na lengo la kuja kuwajengea uwezo wanawake 6,000 Unguja na Pemba, kudai haki zao za uongozi kuanzia ngazi ya chini, kwani mwanamke anapoandaliwa kuwa kiongozi kuanzia nafasi ya chini, itamuwezesha kukua na hata atakapopewa nafasi kubwa itakuwa ni rahisi kumudu kusimamia majukumu yake.

Mapema Mkurugenzi wa jumuiya ya PEGAO Hafidh Abdi Said, alitowa rai kwa jamii kuwachagua wanawake katika nafasi za uongozi, kwani wanasifa ya kuongoza na waaminifu katika kazi zao.

“Katika masakata yote yanayotokea juu ya Rushwaa na mambo mengine ya ubadhilifu wa mali za uuma, mwanamke humuoni katika matukio hayo hii ni kuonyesha kuwa wanawake ni watu waaminifu sana”alisema.

Wakitoa maoni yao katika mikutano hiyo, Mohamed Ali alisema wanawake wanapaswa kujiamini wakati wanapotaka kuingioa katika nafasi za uongozi, ili waweze kushindana na wanaume kwani PEGAO kazi yao ni kutoa elimu hadi vijijini.

Alisema wapo wanawake baadhi yao wako vizuri katika kuwania nafasi za uongozi, hushindana na wanaume kwenye majimbo na wanaume kushindwa kutokana na umakini wake.